Alisema hayo wakati akifungua kikao cha kawaida cha siku mbili cha Baraza Kuu la Uongozi wa CUF Taifa, katika ofisi kuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam jana.
“Tuna wasiwasi mkubwa na utendaji wa Tume, umadhubuti wa tume na uhuru wa tume kufanya kazi yake kwa uadilifu,” alisema Prof. Lipumba
Aliongeza: “Na tuna wasiwasi mkubwa shughuli hii ya uandikishaji, ambayo kwanza (Nec) walihitaji vifaa 15,000, lakini hawakuvipata, wakaahidiwa vifaa 8,000, lakini mpaka sasa mwezi wa nne wana vifaa 498.”Alisema wasiwasi mmojawapo walionao, uko juu ya Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva, kama anaweza kumtangaza mgombea atakayesimamishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) endapo atashinda katika kinyang’anyiro cha kuwania urais.
Prof. Lipumba alisema wasiwasi huo unatokana na Jaji Lubuva kushindwa kumueleza Rais Jakaya Kikwete kinagaubaga kwamba, kwa mujibu wa sheria, Nec ndio yenye mamlaka ya kutangaza siku ya kupiga kura ya maoni ya katiba mpya.
“Sasa ikiwa (Jaji Lubuva) anashindwa kumueleza Rais, kuieleza serikali kwamba, jamani sheria inasema sisi ndio wenye mamlaka ya kutangaza siku ya kura ya maoni, je, huyu mwenyekiti huyu mgombea wa Ukawa akashinda kuwa rais ataweza kumtangaza?” alihoji Prof. Lipumba.
Aliongeza: “Kama anashindwa jambo jepesi la kusema tu kwamba, sisi hatujatoa notisi ya siku ya kupiga kura, huyu mwenyekiti huyu anaweza kweli mgombea wa Ukawa ameshinda uchaguzi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kikwete bado ni rais, bado ni adui yetu, ataweza kweli kumtangaza kwamba, mgombea urais wa chama cha upinzani ndiye aliyeshinda kuwa rais?”
Alisema Nec, ambayo imepewa mamlaka na kifungu namba tano cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, imeshindwa kutoa notisi ya siku ya kupiga kura ya maoni na pia kuwaeleza Watanzania kuwa imefanya hivyo.
Prof. Lipumba alisema sheria hiyo inaeleza kuwa mwenye mamlaka ya kutangaza siku ya kupiga kura hiyo ni Nec kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec).
“Kwamba, wao (Nec na Zec) ndio watakaotoa notisi wiki mbili baada ya swali litakaloulizwa kwenye kura ya maoni kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali,” alisema Prof. Lipumba.
Alisema Nec walipaswa kumueleza hivyo Rais Kikwete baada ya kuamua kutangaza siku ya kupiga kura hiyo kwamba, ingekuwa Aprili 30, mwaka huu, lakini ikashindwa kufanya hivyo.
Hata hivyo, alisema baada ya Rais Kikwete kutangaza tarehe hiyo kuwa ndio kura ya maoni ingepigwa, viongozi wakuu wa vyama vya siasa walimueleza kuwa haiwezekani, kwaniwapigakura walikuwa bado hawajaandikishwa. “Wameanza majaribio mwezi Desemba katika majimbo matatu. Katika jimbo la Kawe wameandikisha katika kata mbili; ya Mbweni na Bunju. Ukitazama sensa za mwaka 2012, matokeo ya sensa yana maelezo ya watu kwa umri wao. Wapigakura wa kata hizo ni zaidi ya watu 51,000. Lakini Nec imeandikisha watu 15,000, ikasema imevuka malengo kwa asilimia sita. Kwamba, imeandikisha watu 15,000 wapigakura wako 51,000 ukitazama sensa bila kuongeza watu, ambao wanaweza kuwa wamehamia katika maeneo hayo, ambayo yako mjini,” alisema Prof. Lipumba.
Alisema pia Nec ilieleza kuwa ilihitaji vifaa 15,000 vya kuandikishia wapigakura, lakini serikali ikawapa 8,000 wakati vifaa vilivyoingia nchini na kutumiwa kwenye majaribio vilikuwa 250, huku vingine vlivyoongezeka hivi sasa vikiwa ni 248.
“Hivi sasa Aprili 14, siku moja baada ya kusherehekea uzao wa Mwalimu Nyerere, vifaa vilivyopo nchini ni 498 wakati kwa mujibu wa sensa, wapigakura nchini kote ni zaidi ya milioni 24, mpaka hivi sasa hata uandikishaji katika mkoa wa Njombe haujakamilika na katiba inazungumzia uchaguzi lazima ufanyike Oktoba 2015,” alisema Prof. Lipumba.
Aliongeza: “Sasa tunataka tustaajabu, katika hali hii, jambo ambalo tumemueleza Rais tujikite katika kuhakikisha wapigakura wanaandikishwa, yeye akasisitiza kwamba kura ya maoni ifanyike Aprili 30, tunamwambia haiwezekani hilo, wapigakura hawapo, hawajaandikishwa, wakaendelea. Hata waziri mkuu bungeni anasema kura ya maoni ni siku hiyo hiyo tarehe 30 Aprili, 2015. Sasa mwishoni wamekuja, wameona kwamba haliwezekani, wakairushia mzigo tume.
“Sasa tume haijatoa notisi, lakini ikasema kwamba, sasa kura ya maoni haiwezi kupigwa Aprili 30, 2015. Ukimuuliza (Jaji Lubuva) lini mmetoa notisi nyie kwamba, kura ya maoni ifanyike Aprili 30? Jaji Lubuva hana maelezo, anasema ndio hivyo hivyo tena, mambo yanakwenda hivyo hivyo.”
“Sasa unabaki unashituka kidogo mwenyekiti wa tume. Sheria imeeleza wazi kwamba tume ndio itakayotangaza siku na wakati wa kupiga kura ya maoni, hajatangaza, Rais katangaza, ameshindwa kusema kwamba, hapana sisi hatujatangaza, anasema tu tunaahirisha mpaka hapo baadaye.”
“Kwa hiyo, tuna matatizo makubwa, tuko kwenye mwaka wa uchaguzi. Mheshimiwa Kikwete badala ya kushughulikia mambo haya, yeye anaendelea kuwa Vasco da Dagama (msafiri, mwanasiasa na mvumbuzi wa Kireno) kuitembelea na kuifungua dunia. Mambo mazito yanayotukabili, yeye hayashughulikii,” alisema Prof. Lipumba.
Aliongeza: ‘Kwa hiyo, wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi wa Taifa, nchi yetu inakabiliwa na hali tete, hali ngumu lazima tuyajadili haya, tutoe mwelekeo na nini cha kufanya katika hali hii ilivyokuwa ngumu.”
Pia alisema uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu, wana wasiwasi kwamba, unakabiliwa na giza zito kutokana na kutokuwapo kwa daftari la kudumu la wapigakura la Nec hadi sasa.
Alisema Julai, mwaka jana, Nec iliwaita wadau na kuwaeleza kwamba, uandikishaji wa daftari hilo ungeanza mwanzoni mwa Septemba.
Prof. Lipumba alisema Nec pia ilieleza kuwa imebaini vituo 40,015 nchini kote na kwamba, kila kituo kitaandikisha wapigakura kwa siku 14.
Alisema kama Nec ilivyowaeleza, mchakato huo ulianza Septemba, mwaka jana na kwamba, lingechukua miezi minne.
Hata hivyo, alisema ilipofika Desemba, Nec ilibadilisha kauli kwa kusema kwamba, inafanya uandikishaji wa majaribio katika majimbo manne.
Alisema wakiwa viongozi wa vyama vya siasa kupitia TCD, walikutana na kufikia maamuzi kwamba, katika hali halisi iliyopo, ni vigumu sana kuendelea na mchakato wa kupata katiba mpya baada ya kuonekana kwamba, hakuna maridhiano ya kitaifa kuhusu katiba hiyo.
Prof. Lipumba alisema zaidi ya hivyo, walifanya jitihada mbalimbali, ikiwamo kukutana na Rais Kikwete mara mbili; Agosti 30 na Septemba 8, mwaka jana.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment