Raia Mwema: Wewe ni mmoja kati ya wasomi waliobobea katika masuala ya siasa hapa nchini. Je, unaionaje hali ya kisiasa wakati tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwezi Octoba mwaka huu?
Dk. Bana: Kwanza niseme kwamba kwa ujumla hali ya kisiasa hapa nchini kwetu ni tete na kwenye hili siwezi kudanganya. Hali haiku kama ilivyokuwa mwaka 2010. Hapana kwa kweli na kuna viashiria kadhaa vinavyoweza kuthibitisha hilo.
Jambo la kwanza linalofanya hali ya kisiasa kuwa tete ni tabia ya wananchi kuonesha wazi kutaka mabadiliko hata kama hawajui watapata faida gani kutokana na hilo, lakini wao wanataka mabadiliko na hilo linaonekana wazi kwa yeyote mwenye macho na akili timamu.
Pili ni tabia njema ya wananchi kuonesha wazi kuchukia vitendo vya ufisadi. Hili linaweza kuleta mabadiliko makubwa katika siasa za Tanzania siku zijazo.
Ajenda hii ya ufisadi ndiyo ilimbeba Dk. Slaa (Wilbrod) mwaka 2010 na alifanikiwa kupata kura nyingi. Hii inaifanya CCM kufanya kazi ya kujibu mapigo badala ya kutoa mapigo. Ukiona chama tawala kikifanya kazi ya kujibu mapigo ujue hali ya siasa ni tete.
Pia ukiangalia kazi wanayofanya Nape (Nnauye -Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Itikadi na Uenezi) na Abdulrahman Kinana (Katibu Mkuu wa CCM) ni kama wao wameanza kukumbuka misingi ya siasa za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, lakini sasa kazi hiyo haifanywi na viongozi wengine wa Mikoa, Wilaya, Kata na vijiji. Hili nalo linaleta changamoto na hali ya siasa kuwa tete maana tulitegemea wana CCM wote wawe pamoja.
Jambo lingine linalofanya hali kuwa tete ni CHADEMA kupata nguvu zaidi na kuibuka kwa UKAWA ambayo nayo nayo imeongeza nguvu zaidi katika siasa na kusababisha mwamko zaidi.
Mfano wa nguvu ya UKAWA ni matokea ya uchaguzi wa serikali za mitaa. Wameonesha mwamko mkubwa zaidi na kutaka kushiriki uchaguzi wa mwaka huu ndio maana hata ukitazama matokeo ya serikali za mitaa mwaka huu hali ilikuwa tofauti sana, wapinzani wamepata viti vingi zaidi ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Sasa ukitafakari matukio machache yaliyotokana na uchaguzi huo wa serikali za mitaa unaona wazi kuwa hali ya siasa nchini ni tete. Pia ukumbuke kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu tutamchagua Rais mpya, hili nalo linaongeza joto la kisiasa mwaka huu hasa kwa kuzingatia kuwa ndani ya CCM kuna mwamko mkubwa zaidi na hili nalo lionaongeza msisimko.
Raia Mwema: Kuna jambo lingine linaloongeza joto la kisiasa mwaka huu mbali na hayo?
Dk. Bana: Ndio, kuna jambo kubwa hapa la Katiba Mpya ambalo pia mchakato wake umegawa taifa badala ya kutuunganisha kama tulivyozoea. Hili nalo limesababisha hali ya kisiasa kuwa tete maana kuna pande kuu mbili yaani CCM na wapinzani.
Makundi haya mawili hayana lugha moja katika suala la Katiba. CCM walikuwa wanataka Kura ya Maoni ifanyike Aprili 30 na kila mwananchi apige kura ya ndiyo, wakati wapinzani wakisema muda huo hautoshi kutoa elimu na kwamba mwaka huu kuna Uchaguzi Mkuu na hivyo suala la Kura ya Maoni liwekwe kando kwanza.
Kama unavyojua licha ya mgawanyiko huo lakini pia mchakato wa Katiba mpya umegusa Tunu za Taifa ambapo watu wamehoji muundo wa muungano wetu na kuzusha mjadala mkali kuliko hata ule wa kundi la G55.
Ilifika wakati mpaka kundi lile la UKAWA likatoka nje na kuacha kuendelea na vikao vya bunge kujadili Katiba mpya na mgawanyiko huo umeendelea kuwepo hadi leo sasa hili linaongeza joto la kisiasa nchini kwa kuwa tulitarajia Katiba Mpya ituunganishe.
Raia Mwema: Kutokana na sababu hizo na kama msomi uliyebobea kisiasa unadhani Rais wa Awamu ya Tano atatoka katika chama gani wakati wa Uchaguz Mkuu mwaka huu?
Dk. Bana: Hili ni swali la mtego bwana, lakini unajua kusema kweli pamoja na hayo yote bado CCM ina nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi mkuu ujao.
Kwa nini? Kwanza CCM ina mfumo wa kuwadhibiti wanasiasa wake hususani wale wanaoonekana kuwa na nguvu, hata wakivurugana lakini hawatoki. Kwa lugha nyingine wamejenga nidhamu ndani ya chama.
Mfumo huo unawapa nguvu ya kupambana na wapinzani wao baada ya kura ya maoni kwa kuwa wanaungana pamoja kupambana na upinzani bila kujali aliyeteuliwa ni mzuri au hafai.
Wimbi la wagombea urais ndani ya CCM linazidi kuipa umaarufu maana watu wanaona ndiko kuna demokrasia kubwa zaidi ikilinganishwa na vyama vingine.
Raia Mwema: Tumeshuhudia matatizo mengi katika kipindi cha miaka 10 ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, ili kujiweka sawa sasa tunahitaji rais wa aina gani kumrithi na twende salama huko tuendako?
Dk. Bana: Kwanza tunamtaka Rais anayetambua kuwa Watanzania walio wengi ni masikini na kukerwa na huo umasikini wa Watanzania. Akikerwa na huo umasikini wa walio wengi atatafuta dawa yake badala ya kufungamana na wachache akadhani ndio hali halisi ya nchi.
Ukienda vijijini hali ya umasikini imezidi kuliko miaka iliyopita. Hivi sasa hata Ofisi ya Serikali ya Vijiji hazipo tena, hakuna hamasa ya wana vijiji kusimamia maendeleo yao. Kuna baadhi ya vijiji walikuwa na mazao ya biashara na walikuwa na soko la uhakika kuuza bidhaa zao lakini leo hawana soko na wamezidi kuwa masikini. Mfumo wetu wa kupambana na umasiini kupitia MKURABITA, TASAF na sasa BRN bado havioneshi dalili ya kumsaidia Mtanzania wa kawaida.
Tunamtaka rais ambaye akiingia madarakani afanye ziara vijijini kabisa siyo kandokando ya miji mikuu akijionea hali halisi kisha achukue hatua upya kabisa. Pengo kati ya masikini na matajiri limezidi kuwa kubwa zaidi na hii ni hatari.
Tuna rasilimali nyingi sana bado hazijatumika vizuri kumsaidia Mtanzania masikini kuondokana na umasikini wake. Sera zipo lakini bado hazimfaidishi Mtanzania masikini. Tunamtaka rais ajaye mwenye uwezo wa kuangalia haya bila woga.
Sifa nyingine ya rais ajaye ni lazima awe msikivu, mpole, anayeamini mifumo inayoendesha nchi na kukubali kushaurika.
Lakini pamoja na hayo yote ni lazima mtu huyo kwanza apatikane kwa kupita katika mfumo rasmi uliowekwa kwanza na chama chake kisha wananchi bila konakona, yeyote atakayepita kupitia mfumo rasmi atafaa kuwa rais. Zipo kamati za maadili na uchunguzi za kupitia kila jalada la mgombea kabla ya kufikia hatua za kupiga kura.
Raia Mwema: Kati ya wanaotajwa tajwa ndani ya CCM unadhani kuna yeyote mwenye sifa hizo ulizotaja?
Dk. Bana: Wengi wametajwatajwa lakini ukiangalia kwa makini ni wazi kuwa kuna wagombea wawili tu wanaoonesha wazi kuwa wanataka kurithi kiti hicho na hao ni Lowassa (Edward) na Membe (Bernard). Hawa ndio unaona wazi wana nia ya kweli kusaka nafasi hiyo.
Mfano Lowassa unaona kabisa kila kona ukienda utakutana naye au watu wake, lakini pia anashiriki katika kila jambo ukienda makanisani yupo, kwenye misiba yupo, kwenye sherehe mbalimbali yupo pamoja na Membe naye ni hivyo hivyo hawa ni wazi kuwa wameonesha nia.
Raia Mwema : Dk. Bana, unadhani hao watu wana sifa hizo ulizotaja?
Dk. Bana: Muda wa kuwapima kama wanaweza kufaa kwa sifa hizo bado upo na isitoshe Watanzania ndio wanatakiwa wajibu kama wanazo hizo sifa mimi kama mtaalamu nadhani niishie kutaja sifa za rais tunayemtaka kisha wananchi ndio waaangalie kama wanazo.
Mfano wote hao wametumika kwa kipindi kirefu, Lowassa amekuwa mbunge na waziri kwa miaka mingi tunajua utendaji wake ni mzuri na ni mchapa kazi hodari, akisimamia jambo linafanikiwa. Membe, amekuwa hivyohivyo, lakini Watanzania ndio wanatakiwa wajibu hilo sasa. Mimi nikifanya utafiti nikatoa sifa za rais tunayemtaka na nikasema fulani anafaa na fulani hafai nadhani itakuwa si haki kwa sasa.
Raia Mwema: Hao watu wanaotajwatajwa CCM si kwamba wameanza kampeni mapema na hivyo tayari wamekiuka taratibu za chama chao?
Dk. Bana: Hapana, kupitia mfumo rasmi maana yake ni kwamba ndani ya chama chako unaweza kuweka msingi mzuri na watu wakakujua kuwa una nia gani na hilo si dhambi. Unapoonesha nia mapema pia inasaidia hata sisi wachambuzi kukufuatilia na kukutathmini. Suala la kampeni na kuonesha nia havihusiani.
Lakini pia nikiendelea kujibu swali lako, tunamtaka Rais atakayegatua madaraka kutoka juu kwenda chini kwa wananchi, hili bado ni dosari kubwa ya maendeleo ya nchi yetu. Angalia hata juzi tu wananchi wa Kahama wamepata maafa mpaka afike Waziri Mkuu ndio anatoa msaada wa maafa ya serikali. Hili halitakiwi.
Tunataka madaraka yafike kwa wananchi kila mkoa unapaswa kuwa na fungu la maafa linaloratibiwa na Mkuu wa Mkoa mwenyewe si mpaka asubiri mablanketi na mahindi yatoke Ofisi ya Waziri Mkuu. Ukiangalia Mkuu wa Wilaya hata ikitokea maafa hana cha kufanya zaidi ya kutoa taarifa sasa nchi hii ni kubwa ina watu zaidi ya milioni 45 halafu maafa yote bado ni waziri mkuu.
Tunataka rais atakayeona hili kwa jicho pana sana si kwa upande wa maafa peke yake hata kwa upande wa maendeleo ni hivyohivyo, kila kitu kinakwama wilayani kwa sababu wamepewa mamlaka lakini uwezeshaji mpaka makao makuu. Sasa fedha nyingi huko wilayani watu wanalipana posho tu kwa kuwa madaraka makubwa yako makao makuu.
Raia Mwema: Mojawapo ya sifa ya rais ajaye umetaja kuwa ni upole. Kwa hali ya nchi yetu sasa unadhani rais mpole atatufikisha popote?
Dk. Bana: Maana yangu kutaja sifa mojawapo ya upole si kushindwa kuchukua hatua kwa wakati katika masuala ya kipuuzi wala kuyafumbia macho. Hapana. Maana yangu halisi ni kwamba rais awe na uwezo wa kuzungumza na kuwasikiliza wananchi wake kwa umakini mkubwa na kwa utulivu badala ya kuridhika tu na taarifa za kumpotosha.
Raia Mwema: Unadhani wagombea ambao tayari wana tuhuma za kutumia fedha kwenye harakati hizi bado wanatakiwa kuingia kwenye kinyang’anyiro?
Dk. Bana: Kwanza hata unapozungumza tu na watu ni lazima utumie fedha kwa maana ya hata nauli au mafuta, hivyo matumizi ya fedha katika uchaguzi ni jambo la kawaida. Cha msingi ni kwamba unatumia fedha kwa sababu zipi na kwa nani? Kama ni kuhonga watu hapama hiyo ni rushwa lakini kama ni kwa halali si tatizo. Tukumbuke kuwa kila kitu ni gharama kikubwa ni kujua tu uhalali wa gharama basi.
Pia inawezekana mgombea akawa na marafiki zake wanamsaidia fedha kidogo kwa nia njema kulingana na uwezo wake ili afikie malengo yake, pia hiyo sioni kama ni tatizo.
Jambo la msingi hapa ni mamlaka husika kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa makini zaidi na Sheria. Mwaka 2010 uchaguzi uligharimu fedha nyingi sana, kuna taarifa kwamba kwa jimbo moja wagombea walitumia hadi milioni 100 kusaka kura na kwa upande wa rais hadi bilioni moja.
Fedha hizo ni nyingi sana na inatakiwa mamlaka husika utafakari upya jinsi ya kudhibiti matumizi hayo kwani kwanza yanasababisha watu wenye sifa lakini hawana fedha kukosa nafasi ya kuongoza au kuwakilisha wenzao hata kama wana uwezo, matokeo yake tunaweza kuwa na viongozi wasiofaa ilimradi tu wana fedha. Hili tatizo ni kubwa sana CCM.
Raia mwema: Umetaja chanzo kimojawapo cha fedha kwa wagombea kinaweza kuwa ni marafiki, je watazirudisha vipi wakishaingia madarakani zaidi ya kuingiza nchi katika mikataba mibovu, unyonyaji na ukwepaji kodi?
Dk. Bana: Akina Sabodo wanaosaidia CHAMADEMA na hata CCM atazirudisha vipi? Wapo marafiki kama hao ambao wanajisikia amani kumsaidia mtu si dhambi kama fedha zake ni za halali.
Dk. Bana: Ushauri wangu wa haraka haraka kwanza ni serikali kusimamia sheria za nchi bila kuangalia sura na kuacha dhana ya kulindana kupindisha sheria. Kama sheria ya BoT (Benki Kuu ya Tanzania) inamtaka kila mtu akitaka kupokea au kumpa mtu mwingine fedha inayozidi milioni 10 kupitia kwako kwanza na kujulikana ni nani basi ufanyike kwa wote.Hatutaki kusikia taarifa kama tulivyosikia Escrow kupitia benki ya Stanbic, haiwezekani mtu atoe mabilioni kisha tuanze kuchunguza aliyetoa haiji akilini hata kidogo.
Pili ili kuepusha nchi na rushwa wakati wa uchaguzi. Serikali itunze kwanza mafao yote ya wabunge waliopo bungeni sasa hadi baada ya uchaguzi mkuu. Wabunge wakilipwa mafao yao ndio hizo fedha wanazotumia kuwarubuni wananchi badala ya kunadi sera.
Ili kuwepo na haki ni vizuri mafao yote ya wabunge wa sasa yakakokotolewa kisha kuhifadhiwa baada ya uchaguzi mkuu ndio wahusika walipwe. Hii itapunguza matumizi mabaya ya fedha kwenye uchaguzi kwa sehemu kubwa sana kwa kuwa malipo hayo ndio mtaji wa rushwa kwenye chaguzi zetu. Pia iteleta haki katika uchaguzi.
Tusisahahu kuwa hata watumishi wa umma wanastafafu wanakaa muda wa miezi sita hata na zaidi bila kupata mafao lakini wanavumilia.
Jambo la tatu kukabiliana na hili ni kupiga marufuku matumizi mabaya ya fedha za mfuko wa jimbo ambalo kwa sasa unasimamiwa na wabunge. Mfano hivi sasa unashuhudia misaada ya kutoa mabati, saruji, tofali na vitu vingine vimeongezeka sana, hivi hawa wabunge walikuwa wapi mpaka uchaguzi ukaribie ndio waanze kutoa?
Kibaya zaidi wanadanganya wananchi kwamba wametoa msaada lakini kumbe wametoa fedha za umma kwenye mfuko wa Jimbo, hili halikubaliki na naiomba TAKUKURU( Taasisi na Kuzua na Kupambana na Rushwa) waingilie kati haraka.
Raia Mwema: Kama mwana demokrasia na mtaalamu wa masuala ya kisiasa, unaonaje wimbi la sasa la kila chama kuwa na kundi la ulinzi?
Dk. Bana: Hili nalo ni jambo la hatari sana na ni moja kati ya sababu zinazosababisha hali ya kisiasa kuwa tete zaidi maana hii tabia imeanza kuleta mgawanyiko kwa vijana wa Kitanzania na tunakoelekea ndio kubaya zaidi.
Ushauri wangu namwomba kwa dhati kabisa IGP (Mkuu Mkuu wa Jeshi la Polisi) apige marufuku vyama vyote kuwa na makundi haya. Itafika wakati kila kundi litataka kuonesha umairi wao hapatakalika na kibaya zaidi tumeona baadhi ya matukio ya kutumia silaha sasa hawa siku wakipata silaha itakuwaje?.
Raia Mwema: Unaonaje hali ya siasa za Tanzania na majirani zetu wa Afrika Mashariki?
Dk. Bana: Tukijilinganisha na majirani zetu wa Afrika Mashariki, Tanzania tuko vizuri sana. Sisi ndio nchi pekee ambayo bado tunakabidhiana madaraka kila baada ya miaka 10 kwa mujibu wa katiba bila vurugu.
Raia Mwema: Unatathmini vipi kipindi cha miaka 10 ya Rais Kikwete madarakani?
Dk. Bana: Katika kipindi hiki cha miaka 10 Rais Kikwete kama kiongozi amepata mapigo kadhaa ambayo yanaweza kumharibia hiba yake (legacy) huko mbele. Kwanza ndiye kiongozi wa kwanza kufanya mabadiliko ya baraza lake mara nyingi katika kipindi chake cha miaka 10 kuliko wote waliomtangulia.
Mfano kulazimika kubadilisha baraza la mawaziri mara kwa mara kwa shinikizo si kwa hiari si jambo jema. Pia kumpoteza Waziri Mkuu wako kama rais si jambo dogo .Hili ni pigo kubwa sana, hata hivyo ni fundisho kwa rais anayekuja kuwa makini zaidi na uteuzi wake.
Pigo jingine nililoliona katika awamu hii na kumpa rais wakati mgumu ni Bunge kutaka kuwa juu ya mihimili mingine. Kikatiba watu wanatafsiri vibaya, si kwamba kuisimamia serikali ni kuilazimisha kufanya matakwa ya bunge hapana ni katika hali ya kukamilishana lakini hii ya kutoa shinikizo fukuza fulani kisha wananchi nao sasa wanaunga mkono na jumuiya ya kimataifa si sahihi.
Pigo jingine ni mauaji wa wenzetu walemavu wa ngozi (ALBINO) hili jambo limetia doa sana serikali ya awamu hii na taifa kwa ujumla. Inatuumiza sana kuona vitendo hivi viovu dhidi ya wenzetu na pia imetutia aibu sana mbele ya mataifa.
Pigo jingine kwa Kikwete ni mgomo wa madaktari. Hali ilikuwa mbaya sana na naamini rais alisononeka sana maana watu walipoteza maisha kwa sababu ya ule mgomo.
http://www.raiamwema.co.tz/dk-bana-aeleza-mapigo-sita-ya-kikwete
No comments :
Post a Comment