- Wataalamu wanasema kujifungua kwa upasuaji siyo njia wanayoipendekeza sana labda iwe ni katika mazingira yasiyo salama kwa njia ya kawaida.
- 19% Waliojifungua kwa upasuaji mwaka 2000.
- 1,000 Kwa kila idadi hiyo ya watu waliofanyiwa upasuaji, hatari imeongezeka mara tatu.
Wakati idadi ya wanawake wanaojifungua kwa upasuaji ikizidi kuongezeka nchini, utafiti mpya umeonyesha kuwa migogoro baina ya wahudumu wa afya ya uzazi imechangia ongezeko la wajawazito wanaofanyiwa upasuaji bila kuwapo sababu za lazima.
Utafiti huyo uliowahusisha wanawake 13 waliojifungua kwa upasuaji hivi karibuni, madaktari 18 na wakunga 14 jijini Dar es Salaam, umebaini kuwa baadhi ya wahudumu wa afya ya uzazi huwafanyia upasuaji wajawazito kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu, kutoka Chuo Kikuu cha Uppsala cha nchini Sweeden, Helena Litorp anasema, migororo na ‘presha’ ya kazi ni moja ya sababu za ongezeko la wanawake wanaojifungua kwa upasuaji.
Akizungumza kwa kujiamini, Litorp anasema pamoja na ukweli kwamba wanawake wanaogopa kujifungua kwa njia ya upasuaji wakihofia kifo, huku baadhi ya wahudumu wa afya nao wakiamini kuwa njia hiyo siyo salama kwa wajawazito ikilinganishwa na njia ya kawaida, makundi yote mawili yanakubali kufanyika upasuaji huo kwa lengo la kumwokoa mtoto anayezaliwa.
Hata hivyo, anasema matokeo ya utafiti huo uliofanyika mwaka jana, yanaonyesha kuwa kati ya mwaka 2000 na 2002 asilimia 19 ya wajawazito walijifungua kwa upasuaji huku kiwango hicho kikipanda hadi kufikia asilimia 49 kati ya mwaka 2009 na 2011.
“Tuligundua kuwa madaktari vijana ambao wamepewa jukumu la kuzalisha kwa njia ya upasuaji wanakosa msaada kutoka kwa viongozi wao jambo ambalo wakati mwingine husababisha migogoro baina yao. Madaktari na wakunga wote walisema wanaogopa kulaumiwa kwenye vikao kwa uzembe, hivyo wakati mwingine wamejikuta wakilazimika kuzalisha kwa upasuaji bila kuwa na sababu ya lazima,” anasema.
Madaktari na wakunga wanasema ongezeko la wanawake wanaojifungua kwa upasuaji linatokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao. Wanawake hufikishwa katika hospitali zisizo na vifaa vya kutosha. Pia, wengine wanachelewa kwenda kupata huduma kutokana na elimu na ndogo, lakini wapo baadhi yao ambao hutaka kujifungua kwa upasuaji.
Hata hivyo, anasema kuwa idadi kubwa ya vifo vilivyotokana na uzazi vilisababishwa na shinikizo la damu wakati wa ujauzito/kifafa cha mimba na kupoteza damu nyingi muda mchache baada ya kujifungua, lakini wamebaini kuwa sehemu kubwa ya vifo hivyo (7 asilimia .9), na vifo (asilimia 13) vinahusiana moja kwa moja na kujifungua kwa upasuaji.
“Tulipiga hesabu kwa kila operesheni 1,000 na kubaini kwamba hatari imeongezeka mara tatu zaidi katika hospitali ya mkoa kuliko ile ya chuo kikuu. Changamoto nyingi zilitokana na utoaji wa nusu kaputi ama dawa ya usingizi kwa njia ya uti wa mgongo na uambukizi wa vimelea katika kovu la upasuaji.
Tuliyatafsiri matokeo hayo kama ushahidi wa ongezeko la kujifungua kwa upasuaji katika maeneo yenye vifaa vya huduma vichache, hasa katika hospitali ndogo na pia kuna haja ya kuongeza ubora wa huduma hasa huduma za utoaji dawa za usingizi.
Vilevile, Litorp anasema katika utafiti huo walitaka kubaini iwapo wanawake wenye makovu yaliyotokana na upasuaji wapo katika hatari zaidi ya kupoteza maisha yao au watoto wao. Matokeo yameonyesha kuwa hakuna uhusiano wowote kati ya mambo hayo mawili, badala yake wanawake hao walijifungua salama.
“Matokeo yanatofautiana na vitabu kadhaa vilivyoandikwa awali, lakini yanaweza kuwa hivyo kutokana na kwamba wanawake waliowahi kujifungua kwa upasuaji huangaliwa kwa makini wanapopewa huduma ya afya. Kwa sababu hiyo hutakiwa kuja hospitali mapema wanapokaribia kujifungua, mara nyingi hupelekwe kwenye hospitali zenye huduma bora zaidi,” anasema.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Uuguzi MNH, Dk Agnes Mtawa anasema, operesheni hizo zimeongezeka kwa asilimia 31 katika kipindi cha miaka 11 iliyopita.
“Ongezeko la ghafla la idadi ya kina mama wanaojifungua kwa operesheni kutoka asilimia 19 mwaka 2000 hadi asilimia 50 mwaka 2011 linatisha na linahitaji kufanyiwa utafiti wa kina,” anasema Mtawa.
Mtawa anaeleza kuwa pamoja na kwamba kujifungua kwa njia ya upasuaji ni njia ya kuokoa maisha, utaratibu huo umegeuka tishio kwa wajawazito na jamii kwa ujumla.
Anasema hali hiyo imefika hapo ilipo kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo miundo mbinu hafifu ya afya, uhaba wa rasilimali watu, ukosefu wa vifaa na wafanyakazi kukosa motisha.
“Ninafurahi kutambua kwamba zipo tafiti zinazoendelea kufanywa kuhusu uzazi kwa njia ya upasuaji na kueleza mtazamo wa watoa huduma za afya kuhusu upasuaji huo. Nina hamu ya kusikia matokeo ya tafiti hizo,” anasema.
Hata hivyo, anasema pamoja na wajawazito wanaojifungua kwa upasuaji kuongezeka, vifo vya kinamama hao vimepungua kwa kiasi kikukwa katika miaka 10. Hivi sasa takwimu zinaonyesha kuwa wanafariki wajawazito 478 kati 100,000 wanaokwenda kujifungua.
Mkurugenzi huyo anasema pamoja na mafanikio hayo, Tanzania haijaweza kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia yanayotaka kuwe na vifo chini ya 200 kwa kila wajawazito 100,000. Pia, anasema idadi kubwa ya wajawazito hufariki dakika 30 tangu wamefika hospitalini kutokana na kuchelewa.
Mkunga katika hospitali hiyo, Gloria Mkusa anasema kwa mwaka anazalisha wanawake wengi wanaojifungua kwa upasuaji kuliko wanaojifungua kwa njia ya kawaida.
“Zaidi ya nusu ya wamama tunawapokea wanajifungua kwa upasuaji. Sababu zinategemeana, mara nyingine inakuwa sababu ni mtoto, mara nyingine ni mama,” anasema na kuongeza kuwa mwaka 2014 hospitali hiyo ilipokea wajawazito zaidi ya 11,000.
Hata hivyo, Mkunga na Mhadhiri wa Ukunga wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili, Dk Sebalda Leshabari aliwahi kunukuliwa na gazeti hili, akisema kuwa upasuaji si jambo zuri kwa wajawazito.
“Upasuaji siyo jambo zuri kabisa katika muktadha wa uzazi na ndiyo maana watu huita ni kujifungua kusiko kwa kawaida,” anasema.
Anataja madhara yanayowapata wajawazito wengi baada ya kujifungua kwa upasuaji kuwa ni pamoja na maziwa kutotoka kwa siku kadhaa baada ya kujifungua.
“Maziwa yasipotoka ina maana mtoto anakosa yale maziwa ya kwanza ya mama ambayo huwa na virutubisho vyote,” anasema.
Anaongeza kuwa wajawazito wengi wanaofanyiwa upasuaji hulalamika kupata maumivu ya kichwa kwa muda mrefu pamoja na maumivu ya uti wa mgongo. Pia, anasema baadhi ya wanawake hutaka kujifungua kwa upasuaji bila kuwa na sababu maalumu kutokana na kuwa na dhana potofu.
Taarifa nyingine zinaonyesha kuwa hospitali binafsi zina tabia ya kulazimisha wanawake kujifungua kwa njia ya upasuaji kwa malengo ya kuongeza mapato.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa kujifungua kwa upasuaji katika hospitali binafsi ni gharama inayozidi mara tatu ya ile ya kawaida.
Hii ina maana kwamba wanawake watatu wanaojifungua kwa njia ya kawaida kwenye hospitali hizo, gharama zake ni sawa na mmoja anayejifungua kwa upasuaji.
Tatizo jingine linatokana na wanawake wenyewe ambao huona taabu au karaha kujifungua kwa njia ya kawaida.
Hii inaweza ikawa ni kwa kushauriwa vibaya na jamii ama watu wa karibu. Baadhi ya watu mitaani wanadai njia hii haiathiri viungo vya uzazi vya mwanamke na wala hapati maumivu.
Ukweli ni kwamba wataalamu wanapendekeza njia ya kawaida kuwa ni bora zaidi.
No comments :
Post a Comment