Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Sheikh Abeid Amani Karume
Sheikh Karume aliuawa kwa risasi kwenye ofisi ya chama chake, Afro Shirazi Party (ASP) ambayo sasa ni ofisi ya CCM, Kisiwandui, wakati akicheza bao na wenzake.
Watanzania leo wanafanya kumbukizi ya miaka 43 tangu alipouawa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Sheikh Abeid Amani Karume.
Sheikh Karume aliuawa kwa risasi kwenye ofisi ya chama chake, Afro Shirazi Party (ASP) ambayo sasa ni ofisi ya CCM, Kisiwandui, wakati akicheza bao na wenzake.
Kumbukumbu za viongozi wakuu wa nchi ni jambo ambalo limekuwa likifanyika nchini tangu Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lipitishe sheria kuhusu kuwaenzi viongozi wakuu waasisi wa Taifa.
Sheria hiyo, Namba 18 ya Mwaka 2004 inayoitwa, The Founders of the Nation (Honouring Procedure) Act, ilipitishwa na Bunge, Novemba 2004 na kuanza kutumika Machi Mosi, 2005.
Ni miaka 10 tangu kuanza kutumika kwa sheria hiyo ambayo ndiyo inayotumika pia kwa kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki dunia, Oktoba 14, 1999.
Tunaungana na familia ya mwasisi huyo wa Mapinduzi pamoja na wananchi wa Zanzibar na Watanzania kwa jumla katika kumbukumbu hii, tukiamini kuwa bado inahitajika, hasa kwa kuangalia mchango wake katika ustawi wa nchi yetu.
Yumkini, alikuwa na upungufu kama ilivyo kwa binadamu wengine, lakini kimsingi, Sheikh Karume alikuwa kiongozi jasiri na kwa muktadha huo, tunapofanya kumbukumbu ya Karume, tuwe wenye mtazamo kwamba aliipenda Zanzibar na ndiyo maana ni nadra kuona kiongozi wa miaka ya ’70 aliyefanya mambo ambayo hadi leo yamebakia kitambulisho.
Kwanza, tunakumbuka mradi mkubwa wa makazi ya wananchi wa kawaida na wasio na uwezo ya Michenzani ambayo hadi leo hakuna kiongozi mwingine aliyeiga au kujaribu kujenga maghorofa kama yale.
Pili, Karume alikuwa mwanamichezo ambaye klabu mbalimbali za soka nchini, zikiwamo Yanga na Simba haziwezi kumsahau kwa jinsi alivyochangia kwa nguvu, akili zake katika kuhakikisha zinakuwa na makazi yao wenyewe.
Siyo rahisi kumsahau Sheikh Karume kila unapopita kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambako kuna uwanja umeitwa kwa jina lake au hata ukitembelea Zanzibar na kuona uwanja wa michezo wa Amaan, unatambua mchango wake.
Pia, kuna uwanja wa ndege wa Karume, Chakechake, kisiwani Pemba ambavyo ni kitambulisho kingine cha kazi nzuri ya kiongozi huyo ambaye ijapokuwa ni miaka mingi tangu auawe kikatili, lakini bado ni shujaa ambaye Zanzibar imewahi kuwa naye.
Kwa upande wa habari na mawasiliano, ni nani kati yetu atakayemsahau kirahisi Sheikh Karume, mtu aliyeanzisha televisheni ya kwanza ya rangi katika bara la Afrika ambayo inaitambulisha Zanzibar, imewafanya wananchi wa visiwa vile kupata habari za ndani na nje ya nchi kwa urahisi, jambo ambalo kwa Tanzania Bara limefanyika miaka si mingi iliyopita.
Ni kwa kutambua uongozi wake na mapenzi yake makubwa kwa wananchi, ndiyo maana tunasema kuwa inafaa Karume aenziwe kwa mchango na mapenzi yake kwa wananchi, wakiwamo wale wa kipato cha chini aliowapigania kwa nguvu, akili, utashi wake.
Tunashauri, tunapofanya kumbukumbu ya Karume, tujitathmini, tuzingatie na kuenzi misingi yake, ikiwamo ya umoja wa kitaifa aliyoipigania, aliyekubali kuachia uongozi wake akiwa rais na kuiunganisha na Tanganyika na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jambo ambalo siku hizi ni nadra kufanywa na viongozi wetu wengi.
No comments :
Post a Comment