Kashfa ya uchotwaji fedha zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imemuweka katika wakati mgumu Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja (pichani), baada ya wananchi wa jimbo lake kumuweka kiti moto wakimtaka atoe maelezo ya kina kuhusu Sh. milioni 40 alizopewa na mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd, James Rugemalira.
Ngeleja ambaye amewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, alikumbana na wakati mgumu wakati akizungumza na wananchi wa jimbo lake kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Pambalu ambao walipata fursa ya kumuuliza kihusu fedha za akaunti ya Escrow.
Katika mkutano huo ambao ulifanyika Jumanne wiki hii, mkazi wa Sengerema mjini, James John, alimuuliza Ngeleja fedha alizopewa na Rugemalira zimesaidiaje katika miradi ya Jimbo la Sengerema.
“Wakati unahojiwa na Baraza la Maadili la Viongozi wa Umma, ulisema fedha hizo baadhi uligawa katika makanisa na misikiti je, zilizobaki tueleze zimesaidia katika mradi gani kwenye jimbo la Sengerema, tutajie hata mradi mmoja,” aliuliza John.
“Wakati unahojiwa na Baraza la Maadili la Viongozi wa Umma, ulisema fedha hizo baadhi uligawa katika makanisa na misikiti je, zilizobaki tueleze zimesaidia katika mradi gani kwenye jimbo la Sengerema, tutajie hata mradi mmoja,” aliuliza John.
Ngeleja baada ya kuulizwa swali hilo, alidai kuwa fedha alizopewa ulikuwa ni msaada kutoka kwa rafiki yake Rugemalira, na kwamba alilipa kodi ya serikali Sh. 13,138,125 na kiasi cha Sh. 27,286,875 kilichobaki alichangia harambee kwenye makanisa na misikiti jijini Dar es Salaam.
Alisema fedha nyingine alichangia ofisi za vyama vya siasa majimboni, vikundi vya wajasiriamali na shughuri za maendeleo jimboni mwake huku akionyesha baadhi ya majina ya watu walionufaika na misaada hiyo.
Ngeleja aliwataka wananchi hao kuacha kusikiliza maneno ya wanasiasa ambao alidai walilenga kumchafua kutokana na kashfa ya Escrow akidai wapo viongozi waliopata mgawo katika sakata hilo na kumtaja aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kwamba hajaguswa.
"Nina vielelezo na ushahidi kuhusu Zitto Kabwe...mtakumbuka Mheshimiwa Livingistone Lusinde (Mbunge wa Mtera (CCM) alimtuhumu Zitto kupokea msaada wa zaidi ya Shilingi milioni 30 kutoka kampuni ya Pan African Power Limited, maarufu kama PAP,” alisema.
Wakati Ngeleja akijitetea baadhi ya wananchi walikuwa wakimzomea na kumweleza kuwa hawadanganyiki huku wengine wakimshangilia.
Licha ya Ngeleja kujitetea kwa takribani saa moja, wananchi hao walionekana kuchachamaa kutokana na ahadi ya upatikanaji wa maji safi na salama ambayo yamegeuka kuwa hadithi kwao.
"Naomba mnisikilize kwa makini...huyu Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hakumtaja mtu yeyote kwamba alipata fedha kinyume cha utaratibu...isipokuwa lilipofika kwenye kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), lilikuzwa...na mengine yalikuwa yakitolewa kwenye magazeti,” alisema Ngeleja.
Machi 3, mwaka huu, Ngeleja alifikishwa mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kujibu malalamiko dhidi yake ya kupokea Sh. milioni 40.4 kutoka kwa Rugemalira, kinyume cha sheria ya maadili.
Ngeleja akijitetea mbele ya Baraza hilo lililokuwa chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mstaafu Hamis Msumi, alikiri kupokea fedha hizo kutoka kwa Rugemalira, lakini alisema hazikutolewa kwake kama fadhila za kiuchumi kama malalamiko yaliyowasilishwa dhidi yake.
Alidai fedha hizo aliomba na kupewa zikiwa ni msaada, ambao hautofautiani na misaada inayopokelewa na wabunge wengine, ambayo hubarikiwa na Bunge.
Ngeleja alidai mmoja wa wabunge walionufaika na misaada ya fedha za wafadhili, ni aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ambaye kisheria ni mtumishi wa umma.
Alidai Zitto alinufaika na msaada wa zaidi ya Sh. milioni 30 na dola za Marekani 5,000 kutoka PAP na Independent Power Tanzania Limited (IPTL) alizopata kwa matumizi yake binafsi. Ngeleja alidai misaada mingine, ambayo Zitto amewahi kuipata ni pamoja na unaohusu Sh. milioni 119.9 na Sh. milioni 79, ambazo alidai kuwa aliipata kutoka Shirika la Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Alidai suala hilo kuhusu Zitto liliwahi kuelezwa na Lusinde na Mbunge wa Kishapu, Seleman Nchambi wa CCM kwa nyakati katika mikutano ya 16 na 17, bungeni, mwishoni mwa Novemba, mwaka 2014.
Februari 28, mwaka huu,viongozi watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotuhumiwa kwenye Tegeta Escrow waliondolewa kwenye nafasi za ujumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri.
Waliondolewa ni Ngeleja; aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge .
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment