Abo Rabbo Mansur Hadi
Saudi Arabia, ikiziongoza nchi za Kiarabu za Ghuba (isipokuwa Oman ) na nchi nyingine rafiki imekuwa ikiwashambulia kwa zaidi ya wiki ya tatu sasa kutoka angani, wanamgambo wa Kihouthi (madhehebu yao ni Zaidia- tawi la Shia) wanaosaidiwa na majeshi tiifu kwa rais wa zamani, Ali Abdullah Saleh.
Kuna baadhi ya watu wachache inapotajwa nchi ya Yemen kwa haraka huwakumbuka baadhi ya watu wa nchi hiyo wanaopenda kutafuna kwa saa nyingi majani ya miraa, wenyewe wanayaita Qat.
Mtu anapoyatafuna majani hayo huingiwa na anasa, huwa katika furaha na kuburudika. Pia, Yemen inatukumbusha zile simulizi ndani ya vitabu vitakatifu kuhusu Malkia Mrembo wa Sheba (eneo linalotajwa kuwa lilikuwa Kusini kabisa mwa Bara Arabu au Ethiopia) aliyesafiri na kumpelekea zawadi za thamani Nabii (Mfalme) Sulayman.
Hata hivyo, sasa Yemen inatajwa zaidi kwa vile imegeuka kuwa uwanja wa vita kali na madola yenye kuizunguka, ndiyo yenye usemi, kinyume na ilivokuwa hapo kabla. Marekani na nchi nyingine za Magharibi ndizo zilikuwa na kauli mwisho.
Lakini siyo kwamba mataifa hayo ya Magharibi hayajali kuhusu nini kinatokea huko. Nchi hizo pia zina wasiwasi, zikitambua kwamba mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda na wapiganaji wa ile inayoitwa Dola ya Kiislamu (ISIL), wanaweza kufaidika na mchafuko yanayoendelea Yemen.
Hali hiyo huenda ikazifanya nchi hizo za Magharibi zilipie gharama kubwa baadaye.
Tangu yalipotokea mafuko kwenye mataifa ya Kiarabu ya mwaka 2011, Yemen haijawa tulivu, imo katika vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Pia kutokana na mfumo wake wa kisiasa, kikabila na kimadhehebu siyo ajabu kwamba imegeuka kuwa meza ya mchezo wa dama, mataifa ya nje yakishikilia mpini wa panga.
Takriban watu 700 wameshauawa na mamia wamejeruhiwa, licha ya kuangamizwa miundombinu muhimu.
Rais wa nchi hiyo hadi sasa, Abo Rabbo Mansur Hadi, amekimbilia Saudi Arabia kutafuta hifadhi.
Hiyo ilikuwa baada ya Wahouthi kukamata hatamu za utawala katika mji mkuu wa Sanaa na wapiganaji wao baadaye kufika hadi mji wa kusini wa Aden alikokuwa amekimbilia mwanzoni.
Wasaudi wanadai kwamba mashambulio yanayofanywa na ndege zao yana msingi wa kisheria kwa vile wamealikwa na rais halali wajiingize na kwamba Wahouthi wametwaa madaraka kwa mabavu na wamelazimisha aondoke madarakani rais aliyechaguliwa kwa njia ya kikatiba.
Ni pale tu Wahouthi watapo kubali kurejea katika meza ya mashauriano na kuwachia serikali ya kikatiba irejee madarakani pamoja na Rais Hadi, wanashikilia Wasaudi, ndipo mashambulio hayo yatasitishwa
.
.
Pia, Wasaudi wanadai kwamba Wahouthi ni mawakala wa Iran, wanasadiwa kwa silaha na ushauri kutoka nchi hiyo ambayo Ushia ndiyo madhehebu rasmi. Iran inakanusha jambo hilo.
Hofu ya Wasaudi na Waarabu wengine wa madhehebu ya Sunni ni kwamba Iran ina lengo la kupanua ushawishi wake kwa hali na mali huko Yemen kama inavyofanya katika Syria kwa kumsaidia moja kwa moja Rais Bashaar al-Assad asipinduliwe, huko Iraq kwa kutoa ushauri wa kijeshi kwa serikali ya Kishia na pia nchini Lebanon kwa kuwaunga mkono wanamgambo wa Kishia wa Chama cha Hizbullah.
Vita vya Yemen sasa vinaelekea kugeuka kuwa ni vya kimadhehebu baina ya Wasunni, wengi wao wanaishi Kusini mwa nchi hiyo, na Washia, wengi wakiishi Kaskazini.
Pia, baina ya Saudi Arabia na Iran, kila moja ikitaka kuwa Kaka Mkubwa katika nchi hiyo na eneo la Ghuba, kwa ujumla.
Wakati wa Vita Baridi uhasama baina ya Marekani na Urusi ndiyo ulioamua ni kaka gani yu mkubwa katika eneo lipi la Ghuba. Sasa Marekani haina usemi, imehemewa.
Inashindwa kusitisha vurugu zilioko Iraq na wala haiwezi kujigamba kwamba inashinda katika vita yake dhidi ya ugaidi.
Pia, ajabu ni kwamba Serikali ya Washington inajaribu sasa kusuluhisha utawala wa mashehe wa Kishia wa Tehran.
Makubaliano ya hivi karibuni baina ya nchi hizo mbili juu ya mpango wa kinyuklia wa Iran yamezitia wasiwasi nchi za Kiarabu ambazo maisha ziliifikiria Marekani kuwa ndiyo mshirika na mlinzi wao mkubwa dhidi ya Iran.
Hivi sasa majeshi ya Iraq yanapambana na wapiganaji wa “Dola ya Kiislamu” ya ISIL yakisaidiwa na washauri wa kutokea Iran na pia kwa msaada wa ndege za kivita za Marekani.
Huu ni ushirika wa ajabu! Haujategemewa kutokea hadi miezi michache iliyopita. Pia tamko la karibuni la Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry kwamba huenda mwishowe watu watabidi wazungumze na madikteta, Bashaar al-Assad ili kuvimaliza vita vya Syria, limewafanya Wasaudi waanze kufikiria mara mbili kama kweli Marekani ni wa kutegemewa linapokuja suala la kufa na kupona kwa marafiki zake.
Zaidi ya miaka 200 iliyopita ukoo wa Kisaudi unaotawala sasa ulipigana kwa mara ya kwanza na Wahouthi juu ya nani awe na sauti. Kwa hivyo, mapiganao haya ni kama kuendeleza vile vita vya mwanzo.
Kupitia imamu wao, Wahouthi walitawala sehemu kubwa ya Yemen kwa zaidi ya miaka 1,000 hadi pale walipotimuliwa kutoka madarakani huko Kaskazini mwa Yemen mwaka 1962 kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliotangaza jamhuri katika sehemu hiyo.
Wasaudi kwa muda mrefu, wameiangalia Yemen kama ua la nyumba yao na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa ufalme huo, marehemu Sultan bin Abdul Aziz, aliwahi kuunda kamati maalumu kutunga siasa na kuendeleza ushawishi wa nchi yake katika Yemen.
Inadaiwa kwamba Saudi Arabia ndiyo iliyochangia kuingia madarakani huko Yemen ya Kaskazini Ali Abullah Saleh mwaka 1978.
Pia, Wasaudi walikuwa nyuma ya mpango uliofanikiwa wa kuziunganisha Yemen mbili- ya Kaskazini na ya Kusini mwaka 1990.
Wasaudi haohao, ndiyo waliomkaripia na kumsusia Ali Abdullah Saleh alipomuunga mkono Sadam Hussein wa Iraq alipoivamia Kuwait.
Ni hiyo hiyo Saudi Arabia iliyojiingiza katika vita ya kienyeji upande wa baadhi ya watu wa Kusini waliotaka sehemu yao ijitenge na Muungano.
Saudi Arabia pia ndiyo ilioweka mbinyo mkubwa kwa Ali Abdullah Saleh aachie madaraka. Lakini hadi sasa, rais huyo wa zamani ana ushawishi kwani vikosi vingi vya jeshi bado ni vitiifu kwake.
Hiyo yote ni mifano vipi Saudi Arabia ilivokosea kuzicheza vizuri karata zake za kidiplomasia katika nchi irani ya Yemen.
Muhimu pia isisahaulike kwamba katika vita vya kienyeji vya Yemen ya Kaskazini mnamo miaka ya sitini baina ya wanajamhuri wa kijeshi na wafuasi wa Imamu wa Kihouthi, Misri, chini ya Gamal Abdel Nasser, ilijiingiza na kupeleka maelfu ya wanajeshi wake katika vita hivyo kuwasaidia wanajamhuri.
Matokeo yake ni kwamba Yemen iligeuka kuwa uwanja wa makaburi ya mamia ya wanajeshi wa Kimisri waliokufa huko.
Hofu iliyoko ni kwamba Wasaudi huenda watajiingiza katika matope ya Yemen kwa kutuma wanajeshi wa nchi kavu.
Huenda, tusiombe, yakawapata yale yaliowasibu Wamisri zaidi ya nusu karne iliopita. Mara nyingi tunashindwa kujifunza kutoka historia.
No comments :
Post a Comment