Suala hilo tayari limezua mijadala katika duru za kidiplomasia hapa nchini, huku ikidaiwa kuwa Tanzania inasita kumpongeza kiongozi huyo hadharani kwa sababu anatoka katika chama cha upinzani cha All Progressive Congress (APC) na si kilichokuwa tawala cha People’s Democratic (PDP) cha Rais Goodluck Jonathan.
Msimamo huo wa Tanzania unaelezwa kufanana na ule wa Uganda ambako Rais wake, Yoweri Museveni, naye hajatuma salamu za pongezi hadi wakati tunakwenda mitamboni.
Gazeti hili linafahamu kuwa ni Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya pekee, miongoni mwa marais wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ndiye ambaye anafahamika kuwa ametuma salamu hizo kwa Buhari, ingawa inaelezwa naye alizituma “kimyakimya”.Imekuwa ni utaratibu wa kawaida kwa serikali ya Tanzania kuwapongeza viongozi walioshinda uchaguzi katika nchi mbalimbali duniani, lakini ukimya huu kwa Buhari ndiyo ambao umezua mijadala hiyo.
Mmoja wa wanadiplomasia wa Tanzania waliozungumzia suala hilo kwa masharti ya kutotaja majina, alisema hakuna uvunjaji wowote wa kisheria uliofanyika kwa kutotumwa kwa pongezi hizo, lakini kwa kutofanya hivyo nchi imejionyesha kutojali matakwa ya wananchi wa Nigeria.
“Hakuna sheria yoyote iliyovunjwa. Lakini, unapompongeza Rais mteule wa nchi rafiki maana yake ni kuwa unaheshimu matakwa na matamanio ya wananchi wa Taifa hilo. Hakuna kitu kizuri katika taratibu za uhusiano kama kuonyesha heshima hii.
“Ndiyo maana Marekani walimpongeza Buhari mapema tu mara baada ya Rais Jonathan kukubali matokeo. Inawezekana aliyeshindwa mlikuwa na urafiki naye lakini kumpongeza mshindi ni kuwapongeza wananchi waliofanya maamuzi hayo,” alisema mwanadiplomasia huyo ambaye amewahi kuiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali duniani.
Balozi huyo alitoa mfano wa serikali ya Afrika Kusini ambayo ilikuwa na matatizo na serikali ya Goodluck Jonathan lakini mara baada ya ushindi wa Buhari imetoa taarifa ya kueleza namna ilivyo tayari kuzungumza na kiongozi huyo mpya ili kuondoa tofauti hizo.
Na kwa sababu aliyeshinda ni Mkuu wa Nchi, Balozi huyo alisema salamu za pongezi zinatakiwa kutumwa na Mkuu wa Nchi na hivyo kwa Tanzania aliyepaswa kutoa pongezi hizo ni Rais Jakaya Kikwete.
Alipohojiwa na Raia Mwema kuhusu ni lini hasa Ofisi ya Rais inatarajia kutuma salamu zake za pongezi kwa Buhari, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu, alisema kwa taratibu zilizopo, suala hilo linaangukia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mkumbwa Ally, alisema angeweza kuzungumzia suala hilo jana kwa sababu muda aliopigiwa simu hakuwepo ofisini na suala hilo atalifahamu akiwa ofisini.
“Hilo la pongezi ni suala la procedure (taratibu) tu. Inawezekana limeshafanyika lakini halijatangazwa hadharani. Kwa bahati mbaya nimetoka ofisini tayari. Naomba tuwasiliane kesho kwa ajili ya kukupa taarifa kamili,” alisema.
Pamoja na utaratibu wa kawaida wa kidiplomasia, Nigeria inachukuliwa kuwa na sehemu ya kipekee katika historia ya Tanzania kwa sababu ndiyo nchi iliyotuma Jeshi lake kulinda taifa hili baada ya maasi ya Jeshi la Tanganyika ya mwaka 1964.
Tanzania na Nigeria pia ziliwahi kuingia katika mgogoro mwishoni mwa miaka ya 1960 kutokana na msimamo wa serikali ya Rais Julius Nyerere kulitambua Jimbo la Biafra lililotaka kujitenga kutoka katika serikali ya Taifa hilo.
Kutokana na uhusiano mwema uliokuwepo baina ya nchi hizi mbili; mojawapo ya mitaa maarufu katikati ya jiji la Dar es Salaam ilipewa jina la Namdi Azikiwe; ambalo ni jina la Rais wa kwanza wa Nigeria huru.
Katika eneo la Kindondoni jijini Dar es Salaam, mojawapo ya viwanja maarufu vimepewa jina la Biafra, likiashiria mshikamano ambao Watanzania kupitia serikali yao walikuwa nao na kiongozi wa waasi hao, Chukwuemeka Ojuku, ambaye hata hivyo jitihada zake zilishindwa na serikali ya Jenerali Yakub ‘Jack’ Gowon.
Nigeria ni taifa muhimu kimkakati barani Afrika kutokana na ukweli kwamba ndilo linaloongoza kwa uzalishaji wa mafuta na pia lenye idadi kubwa ya watu kuliko nchi nyingine yoyote.
Buhari anatarajiwa kuapishwa Mei 28 mwaka huu kuchukua nafasi yake mpya hiyo na Raia Mwema limeambiwa kwamba katika eneo la EAC, ni mwanasiasa mmoja tu wa ngazi za juu; Raila Amolo Odinga wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) cha Kenya, ndiye ambaye amethibitisha kuhudhuria sherehe hizo.
Jenerali Buhari aliyewahi kuiongoza Nigeria kama mtawala wa kijeshi kati ya mwaka 1983 hadi mwaka 1985, alishinda katika uchaguzi huo wa mwezi uliopita unaotajwa kuwa wa kihistoria, kwani ni mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo kwa rais kuondolewa madarakani kwa kura za wananchi.
http://www.raiamwema.co.tz/tanzania-%E2%80%98yamchunia%E2%80%99-buhari
No comments :
Post a Comment