Bajeti ya Serikali ya mwisho ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, jana iliwasilishwa katika Baraza la Wawakilishi kwa mwaka 2015/2016 huku ikielezwa kuwa uchumi wa Zanzibar umeendelea kukua kwa kiwango kikubwa.
Pia ilielezwa kuwa Zanzibar imeendelea kuwa na utulivu wa bei za bidhaa na huduma.
Akiwasilisha bajeti hiyo jana jioni katika baraza hilo huku wageni kadhaa waalikwa wakihudhuria wakiwamo viongozi mbalimbali wa serikali na sekta binafsi, Waziri wa Fedha, Omar Yussuf Mzee (pichani), alisema Katika kipindi cha miaka mitano (2010 hadi 2014), Pato la Taifa limekua kutoka Sh. trilioni 1.0508 hadi kufikia trilioni 2.1335.
Alisema kwa bei za kudumu, Pato la Taifa limekua kutoka Sh. bilioni 848.2 hadi Sh. trilioni 1.1154.
Alisema Pato la Taifa kwa bei za miaka husika kwa mtu mmoja limekua kutoka Sh. 856,000 (Dola 613) mwaka 2010 hadi Sh. 1,552,000 (Dola 939) kwa mwaka 2014.Alisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2010/11 hadi 2014/15, mapato ya ndani yaliongezeka kutoka Sh. bilioni 181.4 hadi Sh. bilioni 360.4 mwaka 2014/15 sawa na asilimia 98.7 kwa kipindi hicho au wastani wa asilimia 19.7 kwa kila mwaka.
“Kwa kipindi cha miezi tisa hadi kufikia Machi 2015, mapato ya kodi yamefikia Sh. bilioni 242.5 sawa na asilimia 91 ya lengo la Sh. bilioni 266.4 bilioni,” alisema Mzee.
Alisema kati ya mapato yaliyokusanywa, Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ilikusanya mapato ya kodi ya Sh. bilioni 135.7 sawa na asilimia 95 ya makadirio ya miezi tisa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya Sh. bilioni 106.8 sawa na asilimia 86 ya makadirio ya miezi tisa.
Akizungumzia deni la Taifa mpaka kufikia Machi 2015, Mzee alisema limeongezeka hadi Sh. bilioni 317.2 sawa na ukuaji wa asilimia 7.6 kulinganisha na deni lililokuwapo Machi, 2014 la Sh. bilioni 294.9.
Kwa mujibu wa Mzee, deni la nje limefikia Sh. bilioni 218 hadi kufikia Machi, 2015 ikilinganishwa na Sh. bilioni 211.8 kufikia Machi, 2014.
Alisema kati ya jumla ya madeni ya nje, asilimia 88 ilidhaminiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na asilimia12 ilidhaminiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Alisema deni la ndani hadi Machi, 2015 liliongezeka hadi Sh. bilioni 99.3 ikilinganishwa na Machi, 2014 la Sh. bilioni 83.1.
Alisema hali hiyo imetokana na kuongezeka kwa deni la kiinua mgongo, deni la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSS)F na Hati Fungani kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akieleza muelekeo wa bajeti ya mwaka 2015/2016, Mzee alisema utaendelea kuzingatia malengo makuu ya Serikali.
Aliyataja malengo hayo kuwa ni kujenga jamii iliyoelimika kwa elimu bora na inayotoa wataalamu wenye hadhi ya kimataifa, jamii yenye siha, iliyoimarika kiuchumi na inayojali umoja wa kitaifa na kufuata misingi ya utawala bora.
Alisema Serikali imekadiria kukusanya jumla ya Sh. bilioni 830.4 huku mapato ya ndani yakitarajiwa kufikia Sh. bilioni 450.5 na mapato ya nje kwa miradi ya maendeleo ni Sh. bilioni 347.1.
Aidha, alisema fedha kutokana na msamaha wa madeni yanatarajiwa kufikia Sh. bilioni 1.3 na Mfuko wa Wafadhili ni Sh. bilioni 1.5, Mikopo ya ndani inatarajiwa kufikia Sh. bilioni 30.0.
Sambamba na hayo, bajeti hiyo imeweka vipaumbele vyake ikiwamo afya, elimu, miundombinu na mahitaji ya watu wa Makundi Maalum.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment