Na Elias Msuya, Dar es Salaam
CHIFU wa kabila la Wazanaki, Japheth Wanzagi ametaja sifa za rais ajaye akisema, anapaswa kuwa ni mtu wa haki.
Hata chifu huyo amesema ni kitendawili kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa na mtu mwenye sifa hiyo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na MTANZANIA Sinza Kijiweni mjini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Chifu Wanzagi alisema kwa kuwa Watanzania walio wengi ni masikini, hivyo rais ajaye anapaswa kutenda haki.
“Kitu kinacholeta taabu kwa sasa ni haki. Haki sasa inanunuliwa, watu wengi ni masikini na utakuta ndiyo wanaoshindana na matajiri na wanashindwa. Hilo ndilo litakalokisumbua chama tawala.
“Ukitembea barabarani utaona vijana wengi wakiuza maji biskuti na bidhaa nyingine. Utakuta kijana anakuuzia bidhaa kwa bei ya chini kwa sababu hawana fedha…Ukifika uchaguzi mkuu vyama vinapita na kuwaaminisha vijana kwamba shida hizo zinaletwa na CCM…kwa hali hii huwezi kusema kuwa CCM itarudi madarakani au wapinzani wataingia madarakani,” aliongeza Chifu Wanzagi.
Alisema hivi karibuni alipokutana na Rais Jakaya Kikwete, wakati wa uzinduzi wa meli vita mbili za doria katika bahari kuu TNS Msoga na TNS Mwitongo,Chifu Wanzagi alisema alimhakikishia rais bora atapatikana.
“Rais Kikwete alisema hilo ni jukumu lake kupata rais mwenye sifa bora… Aliposema ‘sasa meli zimezinduliwa,” mvua kubwa ikanyesha. Nina imani uchaguzi utakuwa wa amani,” alisema.
Akichambua zaidi juu ya mwenendo wa kisiasa ndani ya CCM, Chifu Wanzagi alisema kwa sasa kinatawaliwa na vijana wengi wasiojua chimbuko lake, huku wapiga kura wengi wakiwa vijana.
“Kwa sasa CCM ina sura mpya, watu waliokijua chama wamepungua mno, waliopo wanafanya mapokeo tu. Hata wapiga kura nao wengi ni vijana wasiojua misingi ya chama, hiyo ni changamoto,” alisema.
Makongoro na urais
Akizungumzia tetesi za mtoto wa Mwalimu Nyerere, Makongoro Nyerere kugombea urais, Chifu Wanzagi alisema kwa sasa familia haina maandalizi yoyote kwa ajili yake.
Alisema hata kama Makongoro atajitosa, bado hajafikia uwezo wa kuvaa viatu vya Mwalimu Nyerere.
“Hatuna maandalizi yoyote kwa Makongoro, kila mtu ana siri yake mwenyewe, lakini hatuna maandalizi rasmi,” alisema.
Hata hivyo, alisema ni jambo jema kwa familia ya Mwalimu Nyerere kuwa na mrithi wa kiti cha urais, huku akieleza jinsi anavyomlinganisha Makongoro na baba yake .
“Ni jambo zuri na la kupendeza kuwa na mrithi wa kiti cha urais, lakini si vizuri kulisemasema. Baba yangu alikuwa mkulima, mimi nimekuwa chifu japo si cheo. Mwalimu Nyerere alikuwa mwanasiasa na mkulima, itapendeza kama atapata mrithi wake,” alisema na kuongeza:
“Mwalimu Nyerere alikuwa na nguvu kubwa, huwezi kumlinganisha na Makongoro. Makongoro anaweza kuingiza mguu tu katika kiatu cha mwalimu, lakini hakiwezi kumtosha hawezi kufikia nguvu ya mwalimu.”
Aisifu Chadema
Akizungumzia mwenendo wa vyama vya upinzani nchini, Chifu wanzagi alisema kwa sasa hakuna ubishi kwamba Chadema ndiyo chama kilichosimama ikilinganishwa na vyama vingine vya upinzani.
“Nimewafahamu zaidi Chadema kwa ndani ya miezi miwili, wamefanya ziara pale Butiama katika makundi tofauti. Alianza Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalim. Ukimsikiliza vizuri, kweli utaona ndani yake yuko vizuri,” alisema na kuongeza
“Walikuja pia vijana wa Chadema kutoka Mwanza ambao walitembea kwa miguu, walikuwa na ujumbe wa kupiga vita mauaji ya albino. wao waliiga hatua ya Mwalimu Nyerere ambaye alitembea kutoka Butiama hadi Mwanza.
“Tulimjulisha mama (Maria Nyerere) aliyekuwa Dar es Salaam, akasema hao siyo wa kununulia nyama buchani, wachinjiwe ng’ombe kabisa na sisi tukafanya hivyo,” aliongeza,” alisema.
Alizungumzia pia ujio wa Naibu Katibu Mkuu Chadema (Bara), John Mnyika. “Kwa hizi ziara tatu, nasema Chadema wako vizuri,” alisema.
Msomaji usikose toleo la kesho la gazeti hili, kuhusu uadilifu wa Mwalimu Nyerere.
http://mtanzania.co.tz/?p=4033
Hili blog ni kuhusu Tanzania na dunia nzima kwa ujumla. Pita kila siku kwa habari moto moto. (This blog is about Tanzania and the world as a whole. Pass-by everyday for breaking news). ***********************KARIBUNI NYOTE / YOU ARE ALL WELCOME!***********************
No comments :
Post a Comment