Rais Jakaya Kikwete akizungumza jambo alipokuwa akiangalia Mto Msimbazi eneo la Jangwani jana, alipokwenda kuangalia athari za mafuriko walizopata wananchi yaliyotokana na mvua inayoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam.
- Ni wakati wa ziara yake kukagua athari ya mafuriko jijini Dar es Salaam
- Askari hao walikuwa wakiwasukuma wananachi waliotaka kumsikiliza
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete jana alionekana kukerwa waziwazi na kitendo cha polisi kuwazonga na kuwasukuma wananchi waliokusanyika eneo la Jangwani kumsikiliza.
Tukio hilo lilitokea alipotembelea maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Baada ya kufika eneo hilo saa tisa alasiri, polisi waliokuwa wakiimarisha ulinzi walianza kuwasukuma wananchi hasa kule walipokuwa wakielekea alikokuwa Rais Kikwete.
Mara kadhaa, Rais Kikwete alisikika akiwataka polisi kuacha kuwabugudhi badala yake wasogee upande wake.
Kutokana na askari hao kutotii amri yake, alimwagiza Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliyekuwapo kuwakataza askari hao.
“Jamani, waacheni waje kwa nini mnawapiga? Mbona hamsikii? Kova hebu waambie askari wako wawaache kuwasumbua,” alisikika Rais Kikwete akisema huku akionyesha mkono kwa ishara ya kuwaita wananchi wasogee upande wake.
Baada ya agizo hilo, Kamanda Kova aliwazuia askari kuwasukuma wananchi na ndipo walipoacha.
Akiwahutubia, Rais Kikwete alimwagiza Mhandisi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Eliseus Mtenga kuchukua hatua za haraka kushughulikia changamoto ya kuziba kwa Daraja la Jangwani ili kudhibiti mafuriko yanayoendelea kuathiri wakazi wa eneo hilo.
Alisema hakuna sababu ya kuagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kushughulikia changamoto hiyo kwa kuwa ni kazi ndogo inayoweza kutafutiwa ufumbuzi kwa muda mfupi.
“Huu uchafu ni wa kuondoa haraka, hakuna sababu ya kuleta wanajeshi hapa. Mvua hizi bado zinanyesha, tusisubiri hali iendelee kuwa mbaya,” alisema Rais Kikwete.
Mhandisi Mtenga aliahidi kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo haraka.
Katika hatua nyingine; mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha Shule ya Msingi Msasani kujaa maji, kuvunjika madaraja na kupanda kwa gharama za bidhaa ikiwamo chakula.
Shule hiyo imejaa maji katika vyumba vinane huku waathirika wakuu wakiwa ni wanafunzi wa darasa la saba, chekechea na wenye ulemavu wa kutosikia.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Egidius Mujunangoma alisema wanafunzi wa darasa la saba walikuwa wakijiandaa kwa mitihani ya Moko ya Mkoa wa Dar es Salaam inayotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao.
Alisema hata ofisi yake pia imejaa maji pamoja na maktaba ambako vitabu vyote vimeharibika... “Sina mahali pa kukaa, katika ofisi yangu sijafanikiwa kutoa kitu.”
Alisema licha ya kuwapo maji hayo, wanafunzi wanaendelea na masomo wakitumia madarasa yaliyobaki ambayo hutumiwa na wanafunzi wote.
Mujunangoma alisema afya za wanafunzi zipo hatarini kutokana na maji hayo kutoa harufu mbaya na kwamba chemba nyingi za eneo hilo zimefunguliwa.
Goba
Shule za sekondari Mbopo na Njechele, nazo zimefungwa kutokana na mvua hizo kukata mawasiliano kati ya eneo la Goba na Madale baada ya daraja kubomoka.
Mwanafunzi wa Mbopo, Sadick Khalfani alisema wamefunga shule kutokana na kuvunjika kwa daraja hilo.
“Shule imefungwa, tutapita wapi? Wa Goba hawawezi kwenda Madale na sisi wa huku hatuwezi kuvuka, maji ni mengi, ” alisema Khalfani.
Wakazi wanaoishi eneo la Madale wamelalamikia maisha kupanda kutokana na kuvunjika daraja hilo.
Walisema wanalazimika kununua kilo moja ya unga wa sembe kati ya Sh1,500 hadi 2,000.
Mmoja wa wakazi hao, Waitara Matiku alisema wanapata wakati mgumu kutokana na kupanda kwa gharama za maisha huku wakiwa hawafahamu lini watapata nafuu hata ya kuwekewa daraja la muda.
Mkazi mwingine, Mariamu Mrope anayejishughulisha na uchuuzi wa mboga alisema biashara imekuwa ngumu kwa kuwa wateja wake wakuu walikuwa wanatoka upande wa pili wa Madale.
Alisema wanalazimika kukodi pikipiki kwa Sh7,000 hadi 10,000 kutegemea na hali iliyopo. Kama mvua inanyesha nauli huzidi, wakifika kwenye maji hulazimika kukodi tena vijana ambao huvusha mizigo yao.
No comments :
Post a Comment