Wasio na ajira waelekeze nguvu sekta binafsi, Ajivunia kipindi chake alitoa ajira milioni mbili.
Akihutubia sherehe ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi, iliyofanyika kitaifa jijini Mwanza jana, Rais Kikwete alisema kwa sasa serikali yake haina matumaini ya kuwapa ajira wale wasio na ajira bali wanachotakiwa ni kutegemea zaidi sekta binafsi.
“Matumaini ya kupata ajira serikalini kwa sasa hakuna, bali kimbilieni katika sekta binafsi,” alisema Kikwete.
SEKTA BINAFSI
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake kinachomalizika Oktoba, mwaka huu, serikali yake ilitoa ajira zaidi ya milioni mbili, miongoni mwa hizo zaidi ya 600,000 zilitoka sekta za umma.
Alisema bado ukosefu wa ajira nchini ni tatizo kubwa na licha ya utafiti mkubwa unaoendelea ili kuangalia soko la ajira, bado wananchi wengi hawana ajira.
Alisema serikali yake ilifanikiwa kuboresha mishahara katika sekta binafsi kutoka Sh.48,000 mwaka 2005 hadi kufikia 700,000 kwa baadhi ya sekta binafsi.
Alisema serikali yake ilifanikiwa kuboresha mishahara katika sekta binafsi kutoka Sh.48,000 mwaka 2005 hadi kufikia 700,000 kwa baadhi ya sekta binafsi.
“Wapo baadhi ya waajiri wanaolipa viwango visivyokubalika mpaka sasa kwa wafanyakazi wao, ukiwauliza wanakupa visingizio vingi mara uzalishaji umepungua,” alisema. Aidha, Rais Kikwete aliwapongeza wakaguzi wa afya na usalama mahali pa kazi (Osha), kwa kufanikiwa kufanya kaguzi 56,000 pamoja na kaguzi maalum 26,000 nchini.
Alisema kutokana na kazi zinazofanywa na Osha, serikali itaiimarisha ili iweze kufanya kazi kwa utendaji ulio bora zaidi.
WALIMU
Alisema muundo wa walimu umeidhinishwa na utekelezaji wake umeanza Julai mwaka jana huku madai yao yakiwa zaidi ya Sh. Bilioni 53 kwa serikali.
“Hawa walimu ambao ni shemeji zangu, wanatudai serikali zaidi ya Sh. Bilioni 53 kwa ajili ya walimu 70,668 na tayari walimu 29,243 wamelipwa zaidi ya Sh. Bilioni 23,” alisema Rais.
Aidha, alisema madai ya walimu 30,807 ambao wanaidai serikali zaidi ya Sh. Bilioni 17, baada ya uhakiki uliofanywa majina
yalionekana yana kasoro, lakini malimbikizo ya walimu yanaendelea kufanywa na kulipwa kabla ya Agosti, mwaka huu.
Kadhalika alisema serikali inakusudia kuanzisha tume ya watumishi ya walimu ili waweze kuitumia pamoja na bodi itakayowahusu.
KODI
Kuhusu kodi, alisema serikali yake inaendelea kujitahidi kupunguza kodi ya mapato kwa wafanyakazi kama ilivyofanya kutoka asilimia 18.5 mwaka 2007 hadi asilimia 12 sasa.
“Jambo hili tunafahamu linawaumiza zaidi wafanyakazi, lakini tutajitahidi katika bajeti ya serikali ya mwaka huu kupunguza tena ili iweze kukaribia asilimia 9…serikali ijayo nayo kama itaamua kupunguza, itafanya hivyo,” alisema.
Aliwaagiza makatibu wakuu wa wizara zote kuhakikisha inawabana waajiri ambao hawajaunda mabaraza ya wafanyakazi kwa kipindi kirefu.
Alisema mabaraza hayo yanatakiwa kukutana mara mbili kwa mwaka, na wala kusiwe na kisingizio cha kutokuwa na pesa za kukutana, kwani mara nyingi pesa za vikao wanakuwa nazo.
Hata hivyo, alisema kabla hajang’atuka kutoka katika uongozi Oktoba, mwaka huu, atahakikisha anakutana na mabaraza hayo lakini pia atamshawishi Rais ajaye kuendelea na utaratibu huo wa kukutana na mabaraza ya wafanyakazi. Aliongeza kuwa changamoto za wafanyakazi nchini haziwezi kumalizika kwani hata marais waliotangulia akiwamo Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, hawakuweza kumaliza kero za wafanyakazi nchini.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Nicholas Mgaya, alisema changamoto wanazokumbana nazo wafanyakazi ni pamoja na makato makubwa ya kodi ambayo wanataka yapunguzwe hadi kufikia asilimia 9.
Mgaya alisema hali hiyo imekuwa ikiwaumiza wafanyakazi wengi hivyo inachotakiwa serikali kuangalia upya katika bajeti ya 2015/16 iweze kupunguza.
Aidha, Mgaya alisema waajiri wengi wamekuwa wakiwatisha wafanyakazi bila kuchukuliwa hatua yoyote ya kisheria, hali inayochangia kuzorotesha uchumi.
Alisema mawakala wa ajira nchini wamekuwa wakifanya mchezo kwa waajiriwa kutokana na kugeuka waajiri badala ya kazi yao, hivyo lazima waajiwa wapewe kipaumbele kazini.
Aidha, kuhusiana na ajali zilizotokea nchini katika miezi ya karibuni, Mgaya alisema serikali ichukue hatua stahiki kuweza kudhibiti ajali hizo za barabarani, kwani uwajibikaji ukiwepo lazima zitadhibitiwa.
DK. SHEIN AAHIDI KULIPA MALIMBIKIZO
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amewahakikishia watumishi wa umma kuwa serikali itawalipa malimbikizo ya madai yao yote mapema mwaka wa fedha 2015/2016.
Akizungumza na wafanyakazi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani jana yaliyofanyika katika viwanja vya Kiwanda cha Mkonyo, wilaya ya Chakechake Pemba, Dk. Shein amewahakikishia watumishi hao kuwa serikali inazifanyia kazi kasoro hizo na kuwahakikisha kuwa hakuna mtumishi atakayepoteza haki yake.
Dk. Shein alibainisha kuwa hatua zote zinazochukuliwa na serikali kuimarisha hali ya wafanyakazi, lengo lake ni kulifanya suala la kuwapatia maslahi bora watumishi wa umma liwe endelevu kadri uchumi unavyoimarika.
Miongoni mwa hatua hizo ni kupitisha sheria mbalimbali zikiwamo Sheria Na. 2 ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2011.
Dk. Shein aliwaeleza wafanyakazi hao kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha Sera ya usalama kazini ili kuweka mfumo mzuri wa afya katika maeneo ya kazi kwa lengo la kuwakinga wafanyakazi na ajali na majanga mengine katika sehemu za kazi.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment