Siyo serikali ya Burundi wala ya Tanzania wanataka kusema aliko, Sauti yake yasikika Redio ya Taifa, risasi zarindima jijini Bujumbura.
Shirika la Habari la Kimataifa la China (CRI), lilimkariri Rais Nkurunziza akitoa maagizo hayo kupitia redio ya Taifa na kusifu vikosi vya usalama na jeshi ambavyo havikujiunga na jaribio la mapinduzi hayo lililoongozwa na Meja Jenerali Godefroid Niyombare.
Taarifa hizo zilisema, jeshi la serikali lilidhibiti tena Ikulu, uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bujumbura, jengo la Bunge, makao makuu ya chama tawala cha CNDD-FDD, Televisheni na Redio ya Taifa vilivyokuwa mbioni kutekwa na vikosi vilivyofanywa jaribio hilo la mapinduzi.
Mashirika kadhaa ya habari ya kimataifa yaliripoti kuwa vikosi vya serikali katika mikoa mingine vilikuwa njiani kuelekea jijini Bujumbura. Awali, milio mikubwa ya mabomu na risasi iliripotiwa jana jijini Bujumbura, jana ikiwa siku moja baada ya Jenerali Niyombare kuendesha jaribio la mapinduzi wakati Rais Nkurunziza akiwa jijini Dar es Salaam akihudhuria mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ulioitishwa mahususi kujadili hali ya usalama ya Burundi. Juzi Jenerali Niyombare aliyekuwa Mkuu wa zamani wa usalama wa Taifa hilo, alitangaza kumpindua Rais Nkurunziza, akitumia maandamano yaliyodumu kwa wiki kadhaa yakipinga maamuzi ya chama cha CNDD-FDD kumteua tena Nkurunziza kuwania urais kinyume cha makubaliano ya Arusha yaliyohitimisha vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Kwa mujibu wa Sauti ya Amerika (VOA), bado kulikuwapo na utata kuhusu kundi lipi ambalo lilikuwa likiidhibiti nchi hiyo.
Hata hivyo, Mkuu wa Majeshi ya Burundi Jenerali Prime Niyongabo, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa mapinduzi yaliyofanywa na Jenerali Niyombare yalikuwa yamezimwa. “Jeshi la Taifa la Burundi linatoa wito kwa askari waasi kujisalimisha wenyewe,” alisema Jenerali Niyongabo katika taarifa yake.
Wanaomuunga mkono jenerali huyo muasi, walikanusha taarifa hiyo ya mkuu wa majeshi.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi, Edourd Nduwimana, aliiambia idhaa ya VOA Afrika ya Kati kuwa wanajeshi watiifu kwa Rais Nkurunziza walikuwa wakishikilia Ikulu, Redio na Televisheni ya Taifa (RTNB), na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bujumbura.
Alisisitiza kuwa Rais Nkurunziza alikuwa amerejea nchini humo, ingawa hakueleza sehemu aliko. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon, alitoa wito kwa Taifa hilo kuacha amani na subira vitawale, akisema kwamba Taifa hilo lilipitia kipindi cha miaka 13 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoisha mwaka 2006.
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa walitarajiwa kufanya mashauriano ya dharura jana, na kisha kuwa na mkutano kwa njia ya video na mjumbe wa UN katika Kanda ya Maziwa Makuu. Kwa upande wake, Ikulu ya Marekani ilitoa wito wa kumalizwa kwa machafuko ndani ya Taifa hilo na kuzitaka pande zote kuweka silaha chini.
Msemaji wa Ikulu hiyo, Josh Earnest, alipongeza pia juhudi zinazoendelea kufanywa na viongozi wa kanda ya Afrika Mashariki ya kurejesha amani na umoja ndani ya nchi hiyo.
Marekani imewataka Warundi kuweka silaha chini na kwamba bado inamtambua Nkurunziza kuwa kiongozi halali wa Burundi, lakini inamshinikiza kuheshimu katiba ya Taifa hilo na mikataba ya amani iliyofikiwa mwaka 2000 kwa kutogombea muhula wa tatu.
MILIO YA RISASI MITAANI
Mwandishi wa VOA ,Gabe Joselow, aliyeko jijini Bujumbura, aliripoti kusikika kwa milio ya risasi siku nzima, baadhi ikitokea karibu na kituo cha taifa cha utangazaji kilichokuwa kimezingirwa na askari watiifu kwa Rais Nkurunziza.
Profesa wa sheria wa Kibelgiji, Filip Reyntjens, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya ukanda wa maziwa makuu, aliiambia VOA kuwa Jenerali Niyombare, katika majukumu yake kama mkuu wa usalama wa nchi hiyo, alimuonya Rais Nkurunziza mapema mwaka huu kupitia andiko lake asigombee muhula wa tatu.
Nalo gazeti la Uingereza la The Guardian liliripoti jana kuwa, mapigano makali yalizuka kati ya majeshi yanayopingana katika eneo la utangazaji la Taifa.
Kwa mujibu wa maofisa wa jeshi na mashuhuda, makundi yanayopingana ndani ya jeshi la Burundi, kati ya wale walio watiifu kwa Rais Nkurunziza na wanaomuunga mkono jenerali aliyefanya jaribio hilo, walipambana vikali kwenye eneo linalozunguka RTNB.
Walisema RTNB kilishambuliwa mapema asubuhi baada ya mkuu wa majeshi kutumia redio ya Taifa kutangaza kuwa jaribio hilo limeshindwa.
Mwandishi mmoja aliyekuwa ndani ya jengo hilo, alithibitisha kutokea kwa mapigano makali mapema asubuhi yaliyochagizwa na silaha kali, kama maroketi.
Aidha, Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), lilisema kuwa Rais Nkurunziza alishindwa kurejea nchini humo kutoka katika mkutano wa viongozi wa EAC, baada ya ndege yake kugeuza kurejea ilikotokea. Lakini kwa mujibu wa idhaa ya Kiswahili ya Redio Deutche Welle (DW) ndege hiyo ilitua Uganda.
Ofisa huyo wa ngazi ya juu wa Uganda ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema ndege iliyokuwa imembeba Rais Nkurunziza ilitua katika uwanja wa Entebbe, Uganda, lakini hakutaka kuthibitisha iwapo yuko nchini humo au alirejea Tanzania. Naye Rais Nkurunziza alitangaza kupitia akaunti yake ya twitter kuwa mapinduzi hayo yamefeli, baada ya jeshi kuingilia kati na kudhibiti hali ya mambo.
TANZANIA KIMYA
Serikali ya Tanzania ambayo ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa juzi wa kujadili hali ya Burundi, imesema haijui alipo Rais Nkurunziza.
Kadhalika, imesema Mawaziri wa EAC watakutana Jumatatu ijayo kujadili yali ya Burundi ambayo bado ni tata.
Imesema mkutano huo itafanya tathmini ya hali halisi ya Burundi katika siku mbili tatu tangu kuwapo kwa jaribio la mapinduzi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliyasema hayo jana alipotakiwa na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi wa utata uliopo nchini juu ya mahali alipo Rais Nkurunziza. “Sitaweza kuzungumzia jambo jingine lolote, kuanzia sasa hadi Jumatatu jioni tutakapokutana kama Baraza, hapo ndipo tutajua mambo ya kuzungumza,” alisema na kuongeza:
“Naomba niwataadharishe Watanzania, hali ya Burundi ni tete, lolote linalosemwa wewe unadhani ni dogo, lakini linaweza kugharimu maisha ya mtu, naomba mnielewe na mkae kwa haya niliyowaeleza mengine tusubiri Jumatatu, wenzetu wanayo matatizo, ni vyema tukavuta subra, badala ya kulitangaza tangaza, kila uhai wa mtu uko kwenye hali mbaya.”
Alipobanwa na waandishi kuhusu madai kuwa Rais Nkurunziza alishindwa kutua uwanja wa Ndege Bujumbura kutokana na wanajeshi waliotangaza mapinduzi kuimarisha ulinzi kwenye uwanja huo, alijibu: ”Sijui na siwezi kujibu swali hilo.”
Alisema kwa sababu ya utete wa hali ya Burundi, viongozi hao walikutana kwa nia ya kujadili na kuangalia namna ya kurejesha amani na kuwaomba wananchi wa nchi hiyo kuacha kufanya ghasia na watulie kama nchi nyingine na kuchagua viongozi wao kwa njia ya amani.
Membe alisema nchi za Afrika hazitaki tena nchi yoyote kuhalalisha au kuchukua madaraka kwa nguvu kwa njia ya mtutu wa bunduki.
Alisema hali ya Burundi ni tete na kwamba viongozi wa EAC walikutana kujaribu kurejesha hali ya amani katika nchi hiyo.
Juzi, viongozi wakuu wa EAC, walitoa maazimio matatu ambayo ni kuwataka waliofanya mapinduzi warudishe nchi katika utawala wa kisheria.
Uchaguzi mkuu uliokuwa ufanyike mwezi ujao nchini Burundi, usifanyike hadi hapo hali ya amani itakaporejeshwa na kwamba uchaguzi huo lazima uzingatie makubalinao ya mwaka 2005 yaliyofikiwa Arusha.
Rais Jakaya Kikwete akisoma maazimio hayo, alisema viongozi wakuu wa nchi hizo watakutana tena Dar es Salaam, baada ya wiki mbili ili kuangalia kama hali ya amani imerejea Burundi.
Hata hivyo, juzi usiku NIPASHE ilipata taarifa za kiusalama kuwa ndege ya Rais Nkurunziza iliondoka jijini Dar es Salama majira ya saa 11 jioni, na ilipofika katika anga ya Bujumbura takribani dakika 45, iligeuza na kurejea Dar es Salaam.
Hali ya usalama iliimarishwa alipowasili kiongozi huyo kwani alikuwa mikononi mwa vyombo vya usalama vya Tanzania, na kuna taraifa kuwa alifanya mazungumzo na mwenyeji wake, huku maofisa wengi wa msafara wake wakiwa hoteli ya Serena wakisubiri hatima ya kiongozi wao.
CHANZO: GUARDIAN ON SUNDAY
No comments :
Post a Comment