airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, May 15, 2015

Pinda na maneno ya mshona viatu

Image result for pinda of tanzania


Mhe PINDA
Na Rashid Abdallah.
“Don’t worry! A’m a shoemaker, there is no difference in stitching a shoe and a wound”

Miezi miwili au mitatu nyuma, nilikuwa nikiangalia tamthilia moja ya Kikorea, kuna sehemu inamuonesha mtu kapata majera ya risasi na akashindwa kuenda hospitali kwani askari walikuwa wanamuwinda, akaamua kukimbilia kwa rafiki yake mtengenezaji viatu, wakati anamshona majeraha yake, alikuwa akimwambia; Usiwe na wasi wasi, mimi ni mshona viatu, hakuna tofauti ya kushona kiatu na kushona jeraha.

Siku ya Juamatano ya tarehe 13/5 mwaka huu gazeti la Habari leo, ukurasa wa mbele kabisa ilikuwa na habari yenye anuani; “Pinda: Awamu ya Nne imefanikiwa”, habari hiyo ikiwa na maana kuwa Mizengo Pinda amesema awamu ya anne ya uongozi wa Jakaya imefanikiwa.

Pinda alipokuwa akiwasilisha mapato na matumizi ya Wizara yake juzi bungeni, alisema, kuna mafanikio makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, usambazaji wa nishati vijijini, uboreshaji wa huduma za jamii pamoja na utoaji wa mikopo kwa wananchi.

Aliongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na azma ya Serikali ya CCM ya kutaka kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye hadhi ya Kipato cha Kati ifikapo mwaka 2025.

Siku ya Alhamisi gazeti hilo hilo, likaja na tahariri chini ya anuani, “Hongera serekali ya awamu ya anne kwa mafanikio haya”. Kisha yakaelezwa mengi, huku pakinukuliwa mapato na matumizi aliyoyazungumzia Pinda bungeni.

Tahariri hii ipo mkono wa kushoto, mkono wa kulia kuna kibonzo kikimuonesha mtu aliyepachikwa jina la “Dar”, kasimama juu ya jiwe limeandikwa “mafuriko”, juu yake mkono wa kulia kumeandikwa “miundombinu mibovu” na kushoto kumeandikwa maradhi ya “milipuko”, kisha pia pembeni pameandikwa “kazi unayo mzee”.

Sasa nikapata masuali ya kujiuliza, hivi hili gazeti la Habari leo, linamdhihaki Pinda au hawakuona tahariri yao inavyokinzana na kibonzo chao? Moja kati ya mawili linawezekana, kuwa wanamdhihaki Pinda kwa kuisifia awamu ya nne kufanikiwa ilihali mafanikio ni madogo na wala si ya kujisifia, au inawezekana wamesahau kuwa maana ya tahariri na kibonzo ni kama mvua na jua.

Maneno ya kumpoza mtu na maumivu mara nyingi yanakuwa ni ya upole lakini yahakubaliani na hali halisi, yaani unamtia matumaini tu ili usimkatishe tamaa na maisha, kama yale ya mshona viatu na jeraha.
Nimeyafananisha maneno ya Pinda na yale maneno katika tamthilia ya Kikora, lakini ukweli ni kwamba kila mtu anajua ipo tofauti kubwa ya kushona kiatu na kushona jeraha, lakini rafiki yule aliamua tu kumpoza rafiki yake ili asiwe na wasisi wasi.

Pinda anatupoza kuwa serekali imefanikiwa, lakini ukweli wa mambo anajua kuwa kazi ambayo wameifanya ni ndogo sana kuliko ambayo haijaguswa, sio mafanikio ya kutueleza kuwa wamefanikiwa, ni bora angesema wamejitahidi, hata hizo jitihada basi zingekuwua ni ndogo mno kwa hali halisi ilivyo.
Hatukatai, yapo ambayo yamefanyika lakini nadhani wangeendelea kufanya zaidi na zaidi na zaidi, Pinda anakubali mwenyewe kuwa kati ya hayo ambayo anayazungumza kuwa wamefanikiwa basi yapo ambayo hayajakamilika kwa asilimia mia moja, sasa kama bado hamujakamilisha kuna haja gazi ya kutangaza mafanikio?

Ni sawa na wanajeshi waliokwenda vitani kisha wakatangaza ushindi katikati ya vita, bado mashambulizi yanawajia na kuwamaliza, kisha unawezaje kusimama kutangaza mafanikio.
Maneno haya ya kusema kuwa tumefanikiwa wakati matatizo mengi yametuandama, ndio yanayowafanya watafiti wasifanye kazi, isipokuwa hukaa na kalamu zao kesho asubuhi wanakwambia uchumi wa Tanzania umekuwa, wakati hamna kitu, shida tupu!

Ulipokuwa unaagwa mwili wa John Nyerere, wiki hii Msasani jiji Dar es Salaam, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba, amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa kupungua kwa umaskini kunakoelezwa na baadhi ya wataalamu na wasomi ni suala la kitakwimu ambalo ni gumu kulithibitisha.

Anasema kuwa kuijua hali ya uchumi imekuwa ama imeshuka ni kuangalia hali za watu wa chini, huko ndiko kunakotoa sura halisi ya uchumi wa nchi hii, na wala si makaratasi.

Pinda alitaja mambo mengi wakati wa uwasilisha wa ripoti yake, alitaja viwanja vya ndege, shule, zahanati, barabara na mengine mengi lakini ukweli ni kwamba katika sekta zote hizo alizozitaja bado kuna matatizo makubwa yanakabili, huenda wakisha jenga andio wamejenga hawarudi kuangalia kunaendeleaje, wanatangaza mafanikio.

Unajenga shule lakin baada ya mienzi michache hakuna waalimu, hakuna madawati, hakuna chaki, unajenga zahanati baada ya muda hakuna dawa, wahudumu hawatoshi, umejenga barabara baada ya siku kadhaa imenza kufanya mashimo, yote hayo hurudi kuja kuangalia, unakimbilia kutangaza mafanikio, mafanikio gani?

Awamu ya Kikwete kama imefanya yote hayo uliyoyaorodhesha basi sawa, lakini usituambie kuwa awamu ndio imefanikiwa, awamu huenda imejitahidi tu lakini hali bado mbaya, usitupoze kwa maneno matamu, mengi ambayo hayajakamilishwa hayajafika asilimia mia, maana yake hata mafanikio bado nayo hayajafikiwa.

Raisi Jakaya ondoke madarakani akiwa ameshika mkono kwenye shavu au kichwa chini kwani tatizo sugu la Watanzania limeshindwa kutatuka, nazunngumzia “umasikini”, hakuna nafuu ya tuliko toka na tulipo, sijui anaweza kuacha nchi kisha akajivunia kuwa ameipeleka nchi hatua mbele au ameirudisha nyuma? Huu ni mwendo wa mlevi, hatu mbili mbele nne nyuma, lini tutafika?

Unapopewa fimbo uwaongoze ng’mbe machungani basi ng’ombe atakaye potea lawama ni kwa mchungaji, Jakaya amepewa fimbo na kundi kubwa la watu lakini maendeleo ya watu hawa hayaonekani au ni madogo, kwanini ng’ombe hawanenepi wakati majani yapo, kwanini Watanzania hawanufaiki wakati rasilimali zipo.

Wakati Kikwete anakabidhiwa nchi mwaka 2005, dola 1 ya Marekani ilikuwa sawa na Shilingi 1,128.93, hadi miezi ya mwanzoni mwaka huu dola 1 ya Marekani ni sawa na shilingi 1778.70, uliza sasa, pesa ya madafu imeshuka hadi Tsh 2,000 kwa dola moja.

Mwandishi mmoja katika makala yake anasema: “Nina uhakika kuwa, wakati Kikwete atakuwa anaondoka madarakani mwezi Desemba mwaka huu, dola 1 ya Marekani itakuwa sawa na zaidi ya shilingi 2100 za Tanzania”

Kazi ipo, hadi nasi tufike kuwa nchi iliyoendelea, mmh! tusikate tamaa na ndio Pinda anatupa moyo maneno yake ni kama yale ya mshona viatu, lakini ukweli anajua kuwa kazi tunayo, hasa kwa serekali kama hizi za kifisadi, kujisifia lakini hamna kitu, waporaji, wizi, walafi, waroho, wachoyo, wanoko, wote wamo kwenye serekali, unadhani kuna litakalo kuwa hapo?

Mhe usitutangazie ushindi wakati kila mtu anaona kuwa bado vita vikali vinaendelea, tutakuja kubweteka tupigwe zaidi, tangaza hali halisi ilivyo, naamini siku tukishinda wala haitokuwa na haja ya kututangazia, kila mtu ataona, lakini kwa sasa bado, matumaini na maneno ya kupozana na kutiana moyo waachie wenye majeraha ya risasi, sisi wenye majeraha ya umasikini tuambie ukweli.


No comments :

Post a Comment