Waliokaa Kushoto Kwenda Kulia: Abdallah Kassim Hanga na Abeid Amani Karume
Leo hii asubuhi 12 May, 2014, katika Bunge la Bajeti Mheshimiwa Tundu Lissu kamtaja Kassim Hanga kuwa aliuliwa...
In Sha Allah tunatayarisha kitu kwa kumbukumbu ya Hanga na wenzake waliopoteza maisha baada ya kuipindua serikali ya Sheikh Mohamed Shamte...
Fuatilia ukurasa huu...
Haya hapa chini ni baadhi ya maneno aliyosema Mheshimiwa Lissu Bungeni kuhusu kuuliwa kwa Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala, Saleh Saadalla, Othman Shariff, Mdungi Ussi na Jaha Ubwa...
''Swali kuu ambalo sisi tuliozaliwa ndani ya Muungano tunataka lijibiwe kwa ukweli kabisa ni ‘waasisi’ hawa wengine wa Muungano, akina Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Saleh Saadalla Akidakwa upande wa Zanzibar; na Oscar Kambona, Bhoke Munanka na Job Lusinde kwa upande wa Tanganyika walipotelea wapi na kwanini hawatajwi katika historia rasmi ya Muungano na waasisi wake?Kassim Hanga alikuwa Waziri Mkuu na baadaye Makamu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; wakati Twala alikuwa Waziri wa Fedha wa Serikali hiyo na Saleh Saadalla alikuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi. Kwa upande wa Tanganyika, Oscar Kambona alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wakati wa Mapinduzi ya Zanzibar na baadaye wakati wa kuzaliwa kwa Muungano; Bhoke Munanka alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais mwenye dhamana ya masuala ya usalama, na Job Lusinde alikuwa Waziri wa Serikali za Mitaa. Katika Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!, Ghassany ameonyesha jinsi ambavyo akina Hanga, Twala na Saadalla pamoja na viongozi wengine waandamizi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kama vile Othman Shariff, Mdungi Ussi na Jaha Ubwa waliuawa na kuzikwa katika handaki moja katika sehemu inayoitwa Kama, nje kidogo ya mji wa Zanzibar. Sisi wa kizazi cha Muungano tunataka kujua ukweli juu ya makosa waliyoyafanya hawa waasisi wa Muungano hadi wakauawa na kuzikwa katika kaburi au handaki moja. Tunataka kujua ukweli kama walifanya makosa walishtakiwa katika mahakama gani iliyowahukumu adhabu ya kifo. Aidha, tunataka kuambiwa ukweli kwanini mchango wao katika kuzaliwa kwa Muungano umefichwa kwa muda wote wa nusu karne ya Muungano huu.''
Wakati Dk. Harith Ghassany anaandika kitabu chake, ''Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru,'' siku moja usiku kanipigia simu kutoka Washington. Wakati ule mimi naishi Tanga. Dk. Ghassany akaniuliza kuhusu Hanga nadhani katika mazungumzo yetu siku za nyuma nilipata kumweleza kuwa nikimjua Hanga katika utoto wangu. Baada ya kumpa kisa hiki sikumaliza akanikatisha na kunambia angependa anirekodi katika kinasa sauti ili atumie maelezo yangu kwenye kitabu. hapa chini ndiyo niliyosema kuhusu Hanga na ndivyo yalivyo katika kitabu:
''Mimi nikiishi na baba yangu mtaa wa Somali, namba 22. Klabu ya mwanzo maarufu ya Kilwa Jazz Band ilikuwa kwenye nyumba ya mama yake Abdu Kigunya. Mbele ya nyumba yao ikifika kama saa tisa, kumi, laasiri, wazee walikuwa wanaweka jamvi pale, wanacheza bao. Sasa hivi ukenda pamejengwa majumba ya maghorofa. Hanga akija pale mtaa wa Gogo, kona na Mtaa wa Mchikichi, nyumba ya kona barazani wazee wametandika majamvi wanacheza bao. Mimi nilimjuwa Hanga kwa sababu nikimuona kwenye magazeti. Na wakati ule mawaziri wakitembeya na yale magari meusi yakiitwa “Humber.” Sikumbuki kumuona Hanga kuja pale na gari. Basi ikapita, mapinduzi Unguja yakatokeya sisi wadogo, hatujui nini kinachotokea.
Mwaka 67 nadhani, pale Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, Anatoglou Hall, tukicheza mpira wa miguu pale. Mambo yalianza Mnazi Mmoja katika mkutano wa hadhara. Hanga katolewa jela Ukonga kaletwa pale kuadhiriwa na Nyerere. Sisi ni watoto, mambo yale na nyimbo zile lazima tujumuike. Hanga akaletwa pale. Namuona Hanga mimi kwa macho yangu ya kitoto na miwani yake ile.
Hanga alikuwa mwembamba na mrefu na alikuwa na thick hair. Alikuwa mtu mwenye kupendeza. Kaja pale na uso ulionyongonyeya. Lakini sisi hatujui kinachotendeka. Watoto wa Kiswahili miaka 14, 15, 16, ni wadogo. Hatujui kinatendeka nini. Lakini mimi najua kuwa yule pale Hanga namuona kuwa ni mfungwa. Hanga miwani iko puani uso umemparama kama jiwe la kiama, madevu yamemjaa. Anaadhiriwa! Jua la saa sita mchana linampiga vizuri. Kwa pale kukaa na kajiinamia nilijuwa kuwa mambo si mazuri. Nyerere pale anazungumza na wote wanasikiliza. Nyerere unajua. Nyerere alikuwa ni orator. Na kuna kumuuwa mtu kiungwana. Nakumbuka incident moja Nyerere anamuonyesha kidole Hanga anasema “hili, hili, hili. Hana lolote. Hakuna lolote anaweza kufanya huyu. Afadhali huyu mwanzake [Babu].” Ukitizama kwenye Tanganyika Standard, wakati ule bado halikuchukuliwa na serikali, wakati ule editor ni yule Muingereza, Brandon Grimshaw. Utakuta full page. Mimi kwa jicho langu nimeona kwa sababu baba yangu mimi akinunua lile gazeti. Picha ya Hanga iko mbele na madevu na miwani yake ile. Si mimi tu, watu wengi wanakumbuka hiki kisa. Mimi baba yangu rafiki zake walikuwa Jaha Ubwa, Twala…Wakitembeleyana zamani wakati wa Easter…baba yangu alikuwa memba wa band ya Black Birds ya Bwana Ally Sykes.
Siku Nyerere Alipomuadhiri Hanga Viwanja Vya Mnazi Mmoja Mbele ya Kibarua Bar Nyuma ya Ukumbi wa Arnatouglo Hanga Alitolewa Jela Ukonga Kuletwa Pale Makhsusi kwa Shughuli Hiyo Baada ya Siku Hii Hanga Hakuoenekana Tena
Nadhani kule ndo walikofanya urafiki na hawa jamaa wa Zanzibar. Picha yangu mimi ya Mzanzibari, wakija kule nyumbani, unamuamkia na suala lilikuwa “wewe umeshahitimu wewe.” Na ile ''sophistication'' za wake zao wakija nao pale, yale mavazi, mabuibui, uturi ule, vile vyakula wakiandaa nyumbani pale. Hi ndo picha yangu ya Mzanzibari. Palikuwa na picha pale ukutani ya marahemu father wangu na kina Jaha Ubwa. Ile picha ikapotea pale ukutani. Ikawa haionekani tena. Lakini palikuwa mzee akizungumza habari za akina Twala alikuwa akinong’ona. Nahisi mzee alikuwa ana khofu. Ile ni dalili ya woga. Kitu kibaya kimetendeka. Lakini lazima aulize. Vipi mkewe. Watoto vipi? Lakini hawezi kusema kwa sauti. Siku nilipokuja kukutana na Ali Nabwa aliponielezeya habari za Zanzibar, nikamwambia mimi baba yangu alikuwa ana masikilizano na akina Twala na yeye akaanza ku open up sasa. Nikasema duu! Alipotoka jela Ali Nabwa alikuja pale mtaa wa Narungombe na Skukuu. Pale palikuwa na baraza maarufu sana ya Saigon Football Club. Nabwa alikuwa anakuja pale. Tukitoka tukikaa pembeni tukizungumza chamber. Nilijua baadaye sana kuwa kumbe alikuwa ametoka jela. Pale ndo nilipoanza kuwaona Wazanzibari kwa sura nyingine sasa. Kumbe zile bashasha zinadanganya?
Saigon Club Katika Miaka ya 1970.Kutoka Kushoto Kwenda Kulia: Ahmed Abdallah (marehemu), Mwandishi na Boi Juma Risasi Hapa Ndipo Mwandishi Alipokuwa Akikutana na Ali Nabwa Katika Miaka ya 1970 kwa Mazungumzo.
Kuwa Hanga ndiye aliyekuwa kinara wa Mapinduzi ya Zanzibar hili si jambo lenye utata tena. Ikiwa hivyo ndivyo Hanga hatoweza kuutua mzigo wa roho zilizopotea katika mapinduzi hayo. Ikiwa Hanga atalaumiwa kwa vifo vya maelfu ya Wazanzibari nani alaumiwe kwa mauti yaliomfika Hanga tena kwa kuuliwa kishenzi kwani hapana neno zaidi ya hilo linaloweza kutosheleza kuelezea jinsi Hanga alivyouliwa. Kichekesho kikubwa ni kuwa wale waliopoteza roho na kutangulia mbele ya haki yao yalikuwa yamekwisha. Lakini kwa wale wajane na mayatima waliobakia nyuma na kuhangaika, kifo cha Hanga na wenzake katika wale waliofanikisha mapinduzi kuuliwa kwao kulikuwa miujiza ya aina yake, uchawi usioelezeka nani fundi wake. Ilikuwa vigumu kueleza. Ingeeleweka vyema endapo kisasi cha kuitoa roho ya Hanga kingetimizwa kwa mikono ya maadui zake waliopinduliwa. Haikuwa hivyo.
Wale wajane na mayatima walililipiziwa kisasi na watu waliokuwa maadui wakubwa wa hao waliopinduliwa. Vipi Hanga kiongozi mkuu wa mapinduzi aje kuwa adui wa mapinduzi yenyewe kiasi cha kuwa hukumu ya kumtosheleza haikuwa kifo tu bali kifo cha kishenzi? Fikra za Hanga zilikuwaje pale alipokuwa peke yake ndani ya selo Ukonga Prison…usiku ukimpita bila ya hata lepe la usingizi akiwaza yanayomkabili. Nini kilikuwa kikimpitikia katika ubongo wake wakati wauaji wake walipomtoa katika selo yake na yeye akawakabili ilhali akijua kuwa walikuwa wamekuja kuitoa roho yake. Fikra yake ilikwenda wapi? Ilikwenda kwa Sultan Jamshid bin Abdullah na Masultani wengine waliopita ambao wameiaga dunia mikono yao ikiwa haina damu, au kwa Abeid Amani Karume aliyeingia madarakani kwa mapanga ya Wamakonde wakata mkonge kutoka Sakura na Kipumbwi? Fikra ya Hanga ilielekea wapi? Kwa Nyerere aliyemsaliti?
Hakika ni wazi hakutegemea mapinduzi aliyoyaasisi yangemgeukia na kuwa sababu ya yeye kutolewa roho kwa kuuliwa kishenzi. Jambo la kusikitisha ni kuwa hadi pale alipokamatwa na kuwekwa jela Ukonga na kufikishwa mbele ya mkutano wa hadhara na kuadhiriwa na Julius Nyerere tayari alikuwa keshapoteza kila kitu achilia mbali dira ya mapinduzi aliyokusudia ingeongoza Zanzibar. Hanga hakuwa kamwe na uwezo wa kumfanya Karume lolote kwani Karume tayari alikuwa chini ya mbawa za Nyerere, ngome ambayo Hanga asingeweza kuitikisa achalia mbali kuibomoa. Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar ilikuwa hirizi tosha ya kumkinga Karume. Katika mkasa wa kuuliwa kwa Hanga ndipo msemaji mmoja akasema, “Maiti toka makaburini mwao walionyesha ujuzi wa kufanya miujiza na uchawi wao kwani laiti kifo cha Hanga kingesababishwa na wale waliyopinduliwa kisasi chake kingekuwa cha kutisha. Ilibidi Hanga kwa miujiza ya maiti zile auliwe na wale wale aliowaweka madarakani watu ambao hapakuwepo na sababu ya wao kumuona adui. Halikudondoka chozi kwa kifo cha Hanga. Kila aliyepata mnong’ono wa kuuliwa kwake alikuwa kimya kama vile ile taarifa ya kifo haimuhusu.”
Hebu tumsome Dk. Ghassany ameandika nini katika kitabu chake Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru kuhusu Hanga wakati yuko nyumbani kwa Oscar Kambona anajitayarisha kurejea Tanzania:
''Nnavokumbuka mimi Oscar akatwambia sikilizeni bwana. Mimi nimekwiteni hapa mje mseme na ndugu yenu na mzee wenu huyu, Abdalla Kassim Hanga amekuja hapa na anataka kurudi nyumbani. Hajataja pahala. Na mimi nimemkataza. Nimemwambia huu si wakti mzuri ni bora yeye asiende. Ama angelibaki huko huko West Africa anokotoka kwa mkewe, au abaki hapa London lakini kakataa, anataka lazma arudi. Na mie na hofu maisha yake kuwa akifika kule hatoweza kupata salama. Kwanza kuwa yeye amefikia kwangu, anajulikana yeye na mimi ni rafiki, Nyerere atajuwa zaidi/uzuri hayo kuwa mimi tangu tuko kule tunasikilizana mimi na ndugu huyu Abdalla. Kwa hali hiyo mimi namwambia. Na yeye Abdalla anasema hana ugomvi na Nyerere.
Sasa mimi nimekwiteni mzungumze naye, mseme naye. Akatuchukuwa akatupeleka kwenye chumba akasema “Abdalla, hebu zungumza nao hawa jamaa wamekuja kukuamkia.” Tukaingia sie chumbani akatuacha mimi na Ahmed [Rajab] na Abdalla. Peke yetu watu watatu. Ndivo navokumbuka mie na ndivo anavokumbuka Ahmed [Rajab].
Ahmed Rajab
Mimi sikumbuki ile nilikwenda railway station. Kile mimi sijakumbuka. Kama ulivosema, mimi nyumba nilikuwa naijuwa, sina haja ya Kasembe kunpeleka. Lakini inaweza kuwa nimekwenda mimi na Kasembe kumpokea Ahmed Rajab. Yeye Ahmed kafkiri tu na mie ni mgeni. Hajajuwa kuwa mimi na Kambona tunajuwana na jirani, na nyumba yangu mie na yake si mbali.
Ahmed Rajab ndo anosema, tumefika alofunguwa mlango ni Oscar Kambona, na akatuonyesha chumba. Hajaeleza nini Kambona katwambia. Lakini mimi nakumbuka Kambona katwambia kwanza, “semeni naye.” Yeye kazungumza moja kwa moja, sisi tumekaribishwa tumekwenda kwa Abdalla. Yeye Ahmed amekumbuka mambo mimi sijayakumbuka. Kwa sababu, kasema tulipofika Abdalla Hanga katwambia skizeni: nyinyi ni vijana, watoto kwa sasa, lakini kesho nyie ndo mtakuwa viongozi. Nna maneno nnataka kukwambieni. Tukawa sasa tumekaa tunamsikiliza nini atasema.
Anasema nataka kukwambieni juu ya habari ya mapinduzi yetu ya Zanzibar. Kuna mabaya ambayo tuliyafanya na kabla sijasema lolote nnakutakeni jambo moja muhimu mlikumbuke. Msije mkakubali kufata siasa za ukabila.4 Siasa za ukabila ndizo zinotuletea matatizo na ndizo zitozidi kutuletea matatizo. Hilo ni jambo la mwanzo ambaye yeye Hanga katwambia. Akasema mimi (Hanga) nilivoondoka Zanzibar kupelekwa Dar es Salaam, kuwa Waziri wa kule, badili ya kuwa Vice-President [Makamo wa Rais] huku na Mzee Karume, alivopelekwa bara, anasema jambo moja katika mambo aloyafanya ni kuwasaidia Wazanzibari walokimbia kutoka Zanzibar wakakaa pale, wale ambao wataalamu, kuwatafutia kazi. Akataja majina. Akamtaja Maalim Salim Sanura, na akawataja wengine, mimi siwakumbuki. Kuwatafutia kazi na wakapewa kazi serkalini. Hata ikafika akaanza kusemwa, akalaumiwa, kuwa Abdalla, mbona unakwenda kinyume sasa? Hawa si ndo tuliowapinduwa, mbona wewe sasa hapa unawasaidia? Unawapokea? Akasema bwana, hapa mimi naona ni Mzanzibari tu hapa. Hawa wote ni Wazanzibari bwana. Na hawako nchi nyengine. Wako na sisi pamoja hapa. Kwa hali hiyo yeye anasema ule ndo uzi anataka sisi tuufate. Tusibaguwane.
Jambo la pili akasema, sisi Mungu atusamehe, tumefanya mambo mengi ambayo mabaya, tumedhulumu, tumechukuwa watoto na wake za watu, na Mwenye Enzi Mungu ndiye anojuwa. Basi mimi namuomba Mweye Enzi Mungu anisamehe na ninajuta kwa haya nlioyafanya. Ahmed Rajab akamuuliza suala. Akamwambia, mzee, lakini wewe na Janab [Babu] mnaskizana vipi kisiasa? Akamwambia, mimi na Babu sote wawili ni Marxists lakini Babu si tishio kwa Karume. Mimi ndo tishio. Mimi ndo ni tishio juu ya Karume, lakini Babu is not [si tishio]. Hiyo tafauti yangu mimi na Babu, anasema. Kwa Unguja. Sasa ndio tukamuuliza, Vipi ikawa wewe ndo tishio? Yeye Ahmed Rajab ndo anamuuliza.
Rome ilijaribu kuingia kati katika ugomvi wa Oscar na Nyerere na ilishindwa. Kambona alinieleza. Hata makanisa yamejaribu. Ugomvi ulikuwa mkubwa na hiyo akijuwa yeye zaidi Kambona ndo mana akahofu Abdalla asirudi. Ile imani yake ilikuwa kubwa kuwa Nyerere hatomdhuru. Na yeye akiona watu wangapi wamepotea lakini hajafikiria atakuja kuwa yeye.
Tukasema naye tukamwambia kweli hayo maneno anayoyasema Oscar inaonyesha ni bora usirudi kwa sasa. Akasema hapa kuna mambo mawili. Moja, kuna kutosikilizana baina ya Oscar Kambona na Mheshimiwa Nyerere, Raisi Nyerere. Sasa huyu bwana akisema mimi nisirudi anazungumzia kule kutosikilizana baina yake yeye na Raisi Nyerere. Sasa anahisi mie nikirudi labda kwa sababu mimi nimefikia kwake au ni rafki yake Nyerere anaweza akachukuwa hatuwa. Mimi nimeshafanya kazi na Nyerere na namjuwa uzuri mzee Nyerere, mimi na yeye hatuna ugomvi wowote. Abdalla Kassim Hanga anasema kuwa yeye na Nyerere hawana ugomvi. Na yeye ikiwa anarudi harejei kwa Zanzibar. Atarudi anakwenda zake akakae nyumbani Dar es Salaam. La pili alisema, kuna ukweli wa kuwa mimi na Mzee Abedi Amani Karume kuwa hatuskizani na kusema kweli si makosa yangu. Akasema Abdalla, jambo dogo sana limemfanya Mzee Abedi anichukie mimi hata ikawa mimi nikienda Zanzibar sasa siwezi kukaa nikalala Zanzibar. Lazima siku ileile nirudi Dar es Salaam.
Na hili jambo anasema, mimi nilivokuwa niko Tanzania Bara na Dar es Salaam ni mmoja katika Mawaziri, nilikuwa nnakwenda Zanzibar mara kwa mara. Na nikenda nikifia katika nyumba ilioko Migombani ambayo niliwahi kukaa nilivokuwa Makamo wa Raisi. Wakati mmoja nafikiri baada ya mapinduzi, President wa Zanzibar alikuwa ni Karume na Makamo alikuwa Hanga. Sasa ile nyumba ya Migombani ikawa yeye bado Hanga hajairejesha serikalini kila akienda Zanzibar anafikia pale. Siku katika siku alizokuweko pale anasema yeye kaja kafikia nyumbani pale Migombani na kila akenda watu wakipata habari kuwa Abdalla kaja, watu, jamaa, ndugu na marafiki, walikuwa wanakwenda kumuona na kuzungumza naye, na wengineo wanakuwa nayo mahitajio yao wanakwenda kumuomba awasaidie. Sasa sku moja hiyo Mzee Karume anatokea njia ya uwanja wa ndege kwenda zake mjini akapita pale Migombani akaona magari, akauliza. Kuna nini hapa, mbona magari mengi? Akaambiwa basi lazim Mzee Abdalla Kassim Hanga kaja. “Ala, sasa yeye kila akija lazma iwe namna hii?” Akaambiwa, yeye akija watu wanakuja hapa kumuamkia na kuonana naye. Basi jambo hilo anavosema Abdalla Kassim Hanga ndilo liloanzisha ugomvi baina yake na Mzee Karume. Karume akawa hataki tena na ikawa na yeye Abdalla akenda Zanzibar hafikii tena katika nyumba ile. Akakataa kabisa.
Lakini inaskitisha kuwa tangu wakati ule yeye yupo pale London habari zishafika Cairo. Walioko Cairo maambassador wa pale wameshapeleka habari Tanzania kwa Mzee Nyerere. Ikawa serikali ninavosikia wamekaa wakimngojea arejee tu. Yeye Hanga hajajuwa, wala sisi hatujajuwa.''
Ukimsoma Dk. Ghassany anavyoeleza jinsi Hanga alivyoonywa asirejee Tanzania na yeye akakaidi unaweza kusema kuwa kifo kilikuwa kinamwita. Hebu sikiliza na kisa hiki kilichotokea uwanja wa ndege wa Dar es Salaam siku Hanga alipotua kutoka London kwa Egypt Air. Mpashaji habari wangu anasema:
''Wakati ule mimi nilikuwa meneja wa shirika moja la ndege. Nilikuwa uwanjani nikamuona Bi. Mkubwa. Huyu alikuwa mkewe Hanga, mwanamke wa Kingazija. Nikamuuliza mbona yuko pale akanambia kuwa alikuwa amekuja kumpokea Hanga. Nilishtuka sana. Mimi ni Mzanzibari na nikijuana na Hanga kwa miaka mingi na nilikuwa nasikia mengi. Hanga alipofika nilikwenda kumlaki na tukatoka sote nje ya uwanja na hapo nikamualika yeye na mkewe chakula cha mchana hapo hapo uwanja wa ndege. Wakati tunatoka nje ya uwanja nilimuuliza Hanga iweje karejea nchini wakati kama ule. Hanga akanijibu kuwa hapana kitu. Mimi sikuridhika. Tulipomaliza kula na tukawa tanazungumza nilitaka kwa mara nyingine niufungue moyo wangu kwa Hanga. Sikumbuki nilifanya nini lakini niliweza kumtoa mkewe pale mezani tukabaki sie wawili, mimi na Hanga. Hapo nikamwambia Hanga kuwa ni vyema kama akirejea London na ndege ile ile aliyokujanayo. Hanga hakuniskiliza. Jioni mimi nikamtafuta Ali Nabwa wakati ule anafanyakazi Tanganyika Standard. Nikampa habari kuwa Hanga yuko mjini. Tulimtafuta mji mzima mwisho tukampata Oyster Bay kumbe kafikia kwenye nyumba ya Kambona. Tukaja hadi Magomeni kwa Maalim Matar tukafanya dua. Ali Nabwa kumbe alikuwa amewaambia Tanganyika Standard wasubiri habari muhimu wachelewe kidogo kuchapa gazeti. Siku ya pili Tanganyika Standard ikachapa habari ukurasa wa mbele kuwa Hanga amerejea nchini. Haikuchukua siku Hanga akakamatwa.''
Ali Nabwa
Maalim Mohamed Matar
Kutoka kushoto kwenda kulia ni Abdulaziz Twala (Msaidizi Waziri katika Ofisi ya Rais), Aboud Jumbe (Waziri wa Siha na Majumba), Hasnu Makame (Waziri wa Fedha na Maendeleo), Othman Shariff (Waziri waElimu na Mila), Abdulrahman Babu (Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara), Abeid Karume (Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar), Abdallah Kassim Hanga (Makamu wa Rais), Saleh Saadalla (Waziri wa Kilimo), Idris Abdul Wakil (Waziri wa Kazi, Njia na Nguvu za Umeme) na Hassan Nassor Moyo (Msaidizi Waziri wa Kazi, Njia na Nguvu za Umeme).Abdalla Kassim Hanga.
http://www.mohammedsaid.com/2014/05/abdallah-kassim-hanga.html
No comments :
Post a Comment