zanglassworks

AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, July 22, 2015

CCM imeingiwa hofu, Magufuli kuwa shughuli


KUNA hofu imetanda ndani ya CCM; hofu ambayo inajaribu kufichwa mapema kwani kama mambo hayatobadilika ndani ya miezi hii mitatu hivi iliyobakia kabla ya Uchaguzi Mkuu basi chama hiki kikongwe zaidi nchini kinaweza kujikuta kikipumzishwa kutoka madarakani kwa nguvu. Dalili ya hofu hii imeonekana baada ya kutangazwa kwa mgombea wao wa kiti cha Urais Dk. John Pombe Magufuli. Ilitarajiwa katika mazingira ya kawaida kuwa John Magufuli angeweza kusaidia kuponya majeraha ya kutangaza nia na kukiunganisha chama kwa kusaidia kuvunjika kwa makundi mbalimbali. Ukweli ni kuwa majeraha ya watangaza nia hayajaponyeka na tukichukulia yale ya 2005 kama mfano basi haya ya 2015 yanaweza kuwa ni makubwa, yaliyopenya zaidi na makovu yake bado mapya zaidi. Yanatonesheka kiurahisi. Magufuli, ilitarajiwa kuwa angekuja na umaarufu fulani hivi ndani ya chama kiasi kwamba hata watu ambao walikuwa wameumizwa vibaya sana wangejikuta hawana jinsi bali kumuunga mkono. Tumeona baadhi yao wakitoa kauli za kumuunga mkono. Kutoa kauli ni jambo rahisi zaidi kuliko kuonesha vitendo vya kumuunga mkono. Hili halina shaka. Wengine waliobadili kambi kutoka kambi za wagombea wengine kwenda ile ya Magufuli wamefanya hivyo kama namna ya kuyaokoa maisha yao ya kisiasa (political self-preservation). Lakini majina yao yatakapokatwa na wao watajikuta wametoneshwa tena. Na hakuna mtu ambaye kuunga mkono anahitajika sana ndani ya CCM kama majeruhi mkuu wa mchakato wa kutangaza nia Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa. CCM inamhitaji Lowassa sasa kuliko Lowassa anavyoihitaji CCM. Kama ni kulipa madeni Lowassa amelipa madeni zaidi ya alivyodaiwa; kuanzia Richmond na sasa kuwa alama ya ufisadi ndani ya CCM. Na adhabu yake imekuwa kubwa – kama inaendana na uzito wa tuhuma dhidi yake au la hilo jingine. Pamoja na kuadhibiwa huku kwa fedheha Lowassa alitarajiwa kumuunga mkono Magufuli. Magufuli alifanya kazi chini ya Lowassa na kiutendaji labda ndiye mtu pekee anayeweza kushindana naye mbele ya mwonekano wa jamii. Lowassa alijikuta amedhalilika sana kwenye kashfa ya Richmond na alijiona ameonewa sana wakati ule. Lakini huwezi kulinganisha hisia ile ya kudhalilika au kuonewa kama hii ya kukatwa jina kiasi kwamba hata ndani ya tano bora hayumo. Siyo tu ndani ya tano bora hayumo alijikuta anapitwa hata na watu ambao majina yao au utendaji wao haukaribiani na mtaka nia mwingine yeyote. Hii ilikuwa ni zaidi ya kudhalilika na kuonewa. CCM lakini bado ilimhitaji; inajikuta inamhitaji. Uhitaji huu sasa umegeuka kuwa hofu; hofu inayotokana na swali la “itakuwaje kama?” Lowassa ataamua kujitoa CCM? Au itakuwaje kama Lowassa atakataa kumfanyia kampeni Magufuli hasa maeneo ya Arusha ambayo ni miongoni mwa maeneo CCM imekuwa ikiyagombania? Na cha kutisha kwa CCM ni kuwa tayari mashabiki na wapenzi wa Lowassa wameanza kuiambia CCM “Bye Bye”. Vijana na wazee kutoka mikoa mbalimbali wamechoma na wengine kurudisha kadi zao kama ishara ya kukataa kwao na kubeza kitendo cha Kamati Kuu ya CCM iliyoongozwa na “rafiki” wa Lowassa kulitupilia jina lake pembeni. Wananchi hawa wanajisikia kuumizwa na kusalitiwa na wanaunganisha hasira, huzuni, machungu, kisasi na hisia nyingine zote hasi na zile za Lowassa. Wengi wamejitokeza kujiunga na Chama Kikuu cha upinzani nchini Chadema, wakisubiri au kutarajia kuwa Lowassa atawafuata. Hili linatia CCM hofu. Itakuwaje kama kweli Lowassa ataenda upinzani na makundi ya wana CCM wenye kumpenda wakaamua kumfuata? Lakini pia unaweza kuiona hofu hii kwa namna nyingine. Mojawapo ya mambo ambayo yametokea baada ya Magufuli kutangazwa ni kauli za kuwe yeye “anakubalika na anachagulika”. CCM imetaka kuliaminisha taifa kuwa Magufuli siyo tu anajulikana kwa utendaji kazi wake kwa kweli wananchi wengi wanampenda na wanaweza kumchagua. Kiasi kwamba wametaka watu waamini kuwa Magufuli ni Rais anayesubiria (President in waiting). Kwamba, upinzani hauna nafasi hata kidogo ya kumnyang’anya uwezekano huo. Ukweli ni kuwa matendo ya CCM hayaoneshi kujiamini huku. Kama kweli CCM inaamini Magufuli anajulikana na kazi zake zinakubalika nchi nzima kwa nini juhudi kubwa sana inajaribu kufanywa ya “kumtambulisha”? Unamtambulisha vipi mtu ambaye tayari unaamini anajulikana, kufahamika na kukubalika? Ukiangalia utaona kuwa CCM inataka kumtumia Magufuli kukibeba chama; tatizo ni kuwa Magufuli mwenyewe – ukiondoa kukariri kwake takwimu mbalimbali – utendaji kazi wake una shaka. Tayari wizara ambayo amekalia imeshagubikwa na kashfa lukuki na hili peke yake lingetosha hata kumchafua. Akija mgombea mzuri kutoka upinzani na akajizibu hizi takwimu za Magufuli, basi Magufuli na CCM iko matatani. Yote haya yanatosha kufanya watu wajiulize mara mbili kama kweli Magufuli hatokuwa shughuli kweli kweli. CCM imepasuka, rekodi yake mbovu, na upinzani ukimsimamisha mgombea makini, Magufuli ataweza vipi kushinda? Njia pekee ya kushinda katika mazingira ya namna hiyo ni matumizi makubwa ya nguvu, vyombo vya dola na hata kuliingiza jeshi katika siasa kama walivyofanya chini ya Jenerali Shimbo mwaka 2010. Vyovyote vile ilivyo hata hivyo kuna hofu imetanda kwa CCM; hofu kama vile wingu zito la mvua lenye dalili ya radi na ngurumo. CCM hawajui sasa wafanye nini zaidi ya kuombea Magufuli aweze kuwaokoa. Akishindwa je? Hili ndilo swali la kuogopesha zaidi kwa kila mwana CCM.
- See more at: http://raiamwema.co.tz/ccm-imeingiwa-hofu-magufuli-kuwa-shughuli#sthash.LPuM859G.dpuf

No comments :

Post a Comment