Asema siyo baba wala mama yake, achukua kadi Chadema, Afichua mamlaka za juu zilimzuia kuvunja mkataba Richmond.
Lowassa, aliyekuwa kada mkongwe ndani ya chama hicho tawala, alitangaza kuihama rasmi CCM jijini Dar es Salaam jana.
"CCM siyo mama yangu; kuanzia leo naondoka CCM...vitendo vya mizengwe, chuki, upendeleo na ubakaji wa demokrasia ndani ya CCM vimenifanya mimi kama Mtanzania mwenye nia njema na nchi yangu, nitafute mabadiliko nje ya chama hicho," alisema Lowassa katika hotuba yake aliyotumia takriban dakika 18 kwenye mkutano na waandishi wa habari, viongozi wa juu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), baadhi ya wabunge wa vinavyounda umoja huo na wanachama mbalimbali.
Lowassa alisema amechukua uamuzi wa kuitikia wito wa Ukawa baada ya kutafakari kwa kina na kukubali kujiunga na Chadema kwa lengo la kuungana na upinzani katika kuleta mabadiliko ya kweli nchini.Alisema tangu jina lake lilipoenguliwa na Kamati ya Maadili ya CCM mkoani Dodoma; watu wengi wanaomuunga mkono wamekuwa na shauku ya kutaka kujua hatma yake katika medani za siasa nchini na kumshauri afanye maamuzi magumu.
“Nilipokuwa natangaza nia ya kuwania urais kule Arusha, nilieleza nia yangu na kuanza mchakamchaka wa pamoja wa maendeleo nchini kuondoa umaskini nchini; pamoja na mambo yaliyotokea Dodoma, nia yangu bado iko pale pale," alisema.
Alifafanua kuwa mchakato wa kuteua wagombea ndani ya CCM uligubikwa na mizengwe, ukiukwaji wa maadili, uvunjaji wa Katiba ya chama hicho, utaratibu wa uchaguzi kuvurugwa na kwamba uchaguzi ulifanywa kwa upendeleo wa dhahiri na chuki iliyokithiri dhidi yake. Alisema Kikatiba, Kamati ya Maadili siyo chombo rasmi chenye mamlaka ya kuengua majina ya watu wanaoomba nafasi za kuwania uongozi wa CCM na kwamba kilichofanywa na kamati hiyo ni kupora madaraka ya Kamati Kuu kwa kukiuka Katiba akieleza kuwa kwa lugha ya sasa ni sawa na ‘ni ubakaji wa demokrasia.’
Aidha, alisema pamoja na mizengwe iliyotokea wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea urais kwa tiketi ya CCM; nia yake bado iko pale pale na hajafanya maamuzi ya pupa kujiunga na Chadema.
Alisema ameamua kutafuta mabadiliko nje ya CCM huku akinukuu kauli ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliyewahi kusema kwamba Watanzania wanataka mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya chama hicho.
Alisema kwa wiki mbili zilizopita tangu kuhitimishwa kwa mchakato wa uteuzi wa mgombea urais ndani ya CCM, ametumia muda mwingi kutafakari kilichotokea Dodoma na hatma yake kwenye siasa nchini.
Lowassa alisema wakati akitafakari, marafiki na wananchi wengi wanaomuunga mkono wamekuwa wakisubiri kusikia kauli yake; hivyo alichokifanya siyo cha kukurupuka bali maamuzi yenye tafakuri ya kina.
“Kama ilivyokwishaelezwa, mchakato wa kuteua wagombea uligubikwa na mizengwe, ukiukwaji wa maadili, uvunjifu wa katiba na taratibu za uchaguzi za CCM. Zaidi ya hayo, uchaguzi ulisimamiwa kwa upendeleo dhahiri na chuki iliyokithiri dhidi yangu,” alisema.
Aliongeza: "Kilichotokea Dodoma, ni kupora madaraka ya Kamati Kuu na kukiuka katiba ya CCM.”
Alisema hata vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu viliitishwa na kuburuzwa ili vitekeleze azma ya watu binafsi ndani ya CCM bila kujali demokrasia, katiba, kanuni na taratibu za uchaguzi za chama hicho.
“Niliwekewa mizengwe na kuzushiwa majungu na uongo mwingi kuhakikisha jina langu halifikishwi Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kujadiliwa licha ya ukweli usiopingika kuwa nilikuwa mgombea ninayeungwa mkono na wananchi na wanachama wengi wa CCM kuliko wenzangu wote,” alisema.
“Kibaya zaidi, ni kile kitendo cha kuwanyima wagombea wote 38 haki ya kujieleza mbele ya Kamati Kuu…cha msingi kuzingatia ni kuwa ili kuhitimisha njama za kunipora mimi na wagombea wengine haki zetu za msingi za kusikilizwa, viongozi wachache walikuwa tayari kupanda mbegu ya chuki na mfarakano ambao ni mfano mbaya kwa CCM na hata Taifa letu.”
Alisema: “Kwa kifupi ninaamini sikutendewa haki katika mchakato mzima wa kupendekeza majina na kuteua mgombea wa urais kupitia CCM.”
“Kwa mantiki hii nitakuwa mnafiki kama nitaendelea kujidanganya mimi mwenyewe na umma wa Watanzania kwa kusema kuwa bado nina imani na CCM au kuwa CCM ni chama kitakachowaletea ukombozi wa kweli wa kiuchumi, kisiasa na kijamii…ni dhahiri kwamba CCM imepotoka na kupoteza mwelekeo na sifa ya kuendelea kuiongoza Tanzania yetu. Mimi kama Mtanzania aliye na uchungu na nchi yake nasema imetosha na sasa basi,” alisema.
Alisema safari yake ya matumaini inaendelea kupitia Ukawa.
SHUKRANI
Aliwashukuru watu mbalimbali waliomsaidia kwenye harakati zake za siasa ndani ya CCM akianza na mke wake, Regina, watoto na wanafamilia.
Pia makundi mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini zote, marafiki wa Lowassa, For your movement, Team Lowassa, umoja wa bodaboda, maelfu ya wanachama wa CCM waliomdhamini na mamilioni zaidi waliomuunga mkono.
KASHFA YA RICHMOND
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Lowassa alizungumzia kashfa ya mkataba tata wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond akieleza kuwa hausiki kwa namna yoyote na chochote na kwamba alijiuzulu wadhifa wa Uwaziri Mkuu kwa maslahi ya serikali.
Alisema mwaka 2007 wakati nchi ikikaribia kuingia gizani, serikali ililazimika kuchukua hatua za dharura kujinusuru, lakini baadaye alipobaini kuwa Richmond ni kampuni isiyo na uwezo wa kutimiza azma hiyo, alishauri mkataba uvunjwe.
Hata hivyo, alisema aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha, aliomba apewe muda wa kuzungumza na mamlaka ya juu na baada ya saa moja alimjulisha kuwa mamlaka hiyo imezuia kuvunjwa kwa mkataba huo.
Aidha, kuhusu mikataba mibovu na sheria mbovu, Mwenyekiti wa Cuf, Prof. Ibrahim Lipumba, alisema serikali ya Ukawa itaipitia na kuirekebisha ili Watanzania wote wanufaike na rasilimali za nchi.
VISASI
Kuhusu kulipa visasi kwa wapinzani wake wa kisiasa, Lowassa alisema yeye ni Mkristo ambaye ameaswa kusamehe saba mara sabini.
"Waulizeni hao wanaosema nitalipiza kisasi wamefanya nini hadi wawe na hofu? Lakini niseme hayo yote namwachia Mwenyezi Mungu, yeye ndiye atakayewahukumu."
HALI ILIVYOKUWA UKUMBINI
Saa 9:20 jioni, waandishi kuingia ukumbini. Katika mkutano wa jana, waandishi wa habari zaidi ya 120 wakiwamo wahariri walianza kuingia ukumbini kwa kuitwa majina. Tukio hili, ni miongoni mwa matukio machache ambayo yaliwahi kuhudhuriwa na waandishi wengi waandamizi nchini.
Saa 10:12 familia ya Lowassa ambao ni watoto wake na ndugu wa karibu. Wanafamilia hao waliwasili na kuingia kwenye ukumbi …kupitia lango la Magharibi, mlango ambao ulikuwa na ulinzi mkali wa Red Brigade.
Saa 10:19 viongozi waandamizi waandamizi wa Ukawa na Lowassa, waliingia ukumbini.
Lowassa aliwasili ukumbini akiambatana na viongozi hao pamoja na mkewe, Mama Regina.
Wengine ni James Mbatia wa NCCR-Mageuzi, Prof. Ibrahim Lipumba (Cuf) na Freeman Mbowe (Chadema), aliyekuwa kiongozi wa msafara huo.
Kuwasili kwa Lowassa kuliibua hamasa ya watu mbalimbali wakiwamo waliotaka kupiga picha kwa njia ya simu na waandishi wa habari waliotaka kupata picha ya tofauti. Saa 10:51 Mbowe alimkabidhi Lowassa na mkewe kadi ya uanachama wa Chadema.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment