zanglassworks

AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, July 22, 2015

Haki haikutendeka Dodoma, sawa, lakini ni wapi, lini, ilitendeka?


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimekamilisha mchakato wake wa kumtafuta mwanachama atakayekiwakilisha katika Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mwishoni. Shughuli nzima ya kumpata mgombea huyo ilianza miaka kadhaa iliyopita, makada kadhaa wa chama walipoanza kutajwatajwa kama wagombea watarajiwa.
Ingawaje maelekezo rasmi ya chama hicho yalitaka makada wasianze kufanya kampeni “kabla ya muda” kuwadia, ni siri ya wazi kwamba wahusika wengi walifanya kampeni, baadhi zikiwa za wazi kabisa na nyingine zikiwa za chini chini zaidi.
Baadhi ya makada hao walionywa, na hata kudaiwa kufungiwa shughuli za kisiasa, kifungo hata hivyo ambacho hakikuwa na maana yoyote kihalisia. Mwisho wa siku ilipatikana sura ya kushangaza ya kuwa na wanachama takriban 40 wa CCM waliotangaza nia yao ya kuomba ridhaa ya chama chao wakiwakilishe katika uchaguzi huo. Hatimaye ilionekana waziwazi kwamba mmoja wa wale waliofanya kile kilichoitwa “kutia nia” ndiye aliyeonekana kuwa na nguvu kuliko wengine wote: Edward Ngoyai Lowassa.

“Mtia-nia’ huyu ndiye alikuwa amezoa saini 800,000 za wadhamini wakati idadi iliyohitajika ilikuwa 450 tu. Kila kona ya nchi ilionekana kuwa na umati mkubwa wa watu waliomuunga mkono, nao walijitokeza hadharani kudhihirisha waziwazi msimamo wao huo.
Hata hivyo, kwa baadhi ya wakuu wa chama, hali hiyo haikuridhisha. Zilikuwapo sababu kadhaa kwa nini wakuu hao hawakupendezwa na hali hiyo ilipojitokeza. Ni wazi kwamba wengi walimuona mgombea huyo, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu kabla ya kujiuzulu katikati ya kashfa iliyoitwa “Richmond,” kama mtu aliyetumia fedha nyingi mno katika kampeni yake.
Minong’ono ya matumizi ya fedha, tena fedha za ufisadi katika mchakato huo ilizagaa kila kona. Minong’ono ilizidi kukua na kusambaa pale makundi mbalimbali ya Watanzania kutoka sehemu mbalimbali yalipoonekana yakienda kwake “kumshawishi” atie nia. Makundi hayo yalikuwa ni ama ya wanafunzi, vijana, madereva wa bodaboda, viongozi wa dini na kadhalika.
Katika mkusanyiko mkubwa uliofanyika jijini Arusha mwezi uliopita, ambapo watu wengi maarufu walijitokeza kumuunga mkono Lowassa, ilikuwa wazi kwamba iwapo atapitishwa katika hatua za mwanzo za mchujo, Lowassa asingepata tatizo lolote la kuchaguliwa kama mgombea wa CCM.
Hii ilikuwa na maana moja tu, nayo ni kwamba yeyote aliyetaka kumzuia asiwe mgombea wa CCM alihitaji kumzuia kabla jina lake halijaingia mbele ya Halmashauri Kuu ya CCM. Na hilo ndilo lililofanyika. Jina la Lowassa liliondolewa kutoka katika orodha, kabla ya kikao cha halmashauri kuu.
Hii ndiyo hatua iliyozua mjadala mkubwa nchini, baina ya wale waliomuunga mkono Lowassa, ambao walichukizwa na kitendo cha jina lake kukatwa, na wale waliompinga, ambao walifurahishwa na kukatwa kwa jina lake. Hatimaye, tunajua, katika mvurugano uliofuatia hatua hiyo, ilionekana wazi wazi kwamba chama hicho kikongwe kilikuwa kimeendelea kugawanyika zaidi.
Ishara kuu ya mgawanyiko huo ilijitokeza pale wajumbe wa halmashauri walipompokea mwenyekiti wao kwa wimbo wa kumsifia Lowassa, ambayo ni dalili ya wazi kabisa ya uasi ndani ya uongozi wa chama hicho. Imejulikana kwamba kikao hicho kiliweza kuendelea tu pale marais wastaafu walipokemea kitendo hicho na kuwataka wale waliokuwa hawataki kuendelea na kikao watoke nje.
Hiyo ni dalili ya uasi ambao hauwezi kutoweka tu kwa sababu wakuu wa zamani wamekemea; huo ni uasi ambao utaitafuna CCM ndani kwa ndani na matokeo yake yanaweza kuwa na athari kubwa na za muda mrefu kwa chama hicho. Tutakuja kuyashuhudia, lakini tunaweza kuelewa ni wapi yalikotokea na sababu zake ni nini.
Chama Cha Mapinduzi ni asasi ambayo imekuwa ikienda kinyume cha nasaba yake kwa muda mrefu. CCM ilikwisha kuachana na siasa yake ya utumishi wa wananchi wa hali duni na kugeuka kuwa asasi ya kutafuta madaraka ya kiserikali. CCM ilikwisha kutupilia mbali siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na kuwa kampuni ya wabia ambao sifa yao kubwa ni kwamba wana utajiri mkubwa na wanaweza kununua nafasi yoyote wanayohitaji au mtu yeyote wanayemtaka, kwa maslahi yao.
CCM ilikwisha kujipambanua na misimamo ya kimsingi kabisa ya muasisi wake, Julius Kambarage Burito Nyerere, na kuizika misingi ya falsafa yake ya usawa wa binadamu na umoja wa Waafrika.
CCM ilikwisha kuacha utamaduni wa kujadili masuala mazito, ikabakia ni chama cha kusengenyana, kung’ong’ana na kupikiana majungu. Mmoja wao akionekana kakosea hawamuiti na kumwambia amekosea, bali watamsema wakati hayupo. Lakini hata hilo kosa lenyewe ambalo watakuwa wanamlaumu kwalo linaweza kuwa si kosa ila ni kwamba kawaambia wamewasaliti wananchi na wanachama.
CCM ni chama ambacho, ukiwa ndani yake, usalama wako ni kukaa kimya na kukubaliana na kila ujinga utakaousikia. Ukitaka kuzungumza na ubaki salama, basi huna budi kusifu na kushangilia mawazo hafifu na maono finyu ya kila anayeonekana kuwa na nguvu kwa wakati huo. Na nguvu hizo zinaweza kutokana na ukweli tu kwamba huyo mtu ndiye anawalisha na kuwanywesha wakuu.
Chama kilichojipachika nembo ya Jembe na Nyundo, hivi sasa hakimtetei mkulima wala mfanyakazi, bali kinasimamia moja kwa moja maslahi ya makabaila, mabepari, matapeli na wote ambao shughuli yao kuu ni udalali wa rasilimali za nchi, au kama alivyoandika Profesa Chachage Sethy Chachage, “Makuwadi wa Soko Huria.”
Katika kampuni kama hiyo, nani anaweza kuinua mkono na kudai haki? Dhana yenyewe ya haki ilikwisha kufa na kuzikwa. Nani anayeweza kuifufua leo kwa ajili ya kuendesha mchakato wa kumpata mgombea wa chama? Hakuna. Hakuna kwa sababu huwezi ukaua kitu katika kila unalofanya, halafu ukakifufua ili kikufanyie kazi moja tu halafu kirudie ufu.
Ndilo kosa analolifanya kaka yangu Ngombale pale anaposema kwamba haki haikutendeka, ni kosa ambalo nitaendelea kulijadili. Tuwe pamoja, lakini si kwa maana ya wana-CCM wanapodanganyana kwa msemo wa “Tuko pamoja,” wakati moyoni wanajua wako mbalimbali kama mbingu na ardhi.

- See more at: http://raiamwema.co.tz/haki-haikutendeka-dodoma-sawa-lakini-ni-wapi-lini-ilitendeka#sthash.8NDnrXvS.dpuf

No comments :

Post a Comment