zanglassworks

AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, July 22, 2015

Jina “Lowassa” na hatima ya CCM


Na Ahmed Rajab
KWA sasa hakuna asiyejua nani aliyeibuka mshindi wa mchuano wa ndani ya CCM wa kumtafuta mshika bendera wake katika uchaguzi wa Urais unaotazamiwa kufanywa Oktoba.
Tumeambiwa kuwa aliyeshinda ni Dk. John Magufuli. Lakini tukiutathmini mchakato mzima wa mchuano huo, tangu ulipoanza hadi ulipomalizika, ni taabu kutoamini kwamba Magufuli siye aliyeshinda.
Mshindi halisi hakuwa binadamu bali ulikuwa usanii wa kisiasa. Huu ni usanii ambao nchini Tanzania ni CCM peke yake, hadi sasa, iliyoonyesha miujiza ya kuweza kuufanya huku ikiwaziba macho wanachama wake na wananchi kwa jumla.
Wapo wenye kutabiri kwamba ushindi huo wa kulazimishwa unaweza ukakifanya chama cha CCM kisambaratike na hata pengine kipasuke. Ishara tumekwishakuanza kuziona tangu sasa ingawa ni mapema mno kuagua kiwango cha mpasuko huo kitakuwaje.
Ikiwa patatokea nyufa nyufa tu CCM itaweza kuziziba kwa haraka na kusonga mbele. Lakini iwapo mpasuko huo utaikata CCM kwa mapande, hali itakuwa nyingine.
Yakitokea hayo, CCM itakwenda na maji kama kilivyokwenda chama cha Kenya African National Union(KANU), kilichotawala Kenya kwa takriban miaka 40 tangu nchi hiyo ipate uhuru 1963, au chama cha United National Independence Party (UNIP) kilichotawala Zambia tangu 1964 hadi 1991, au kile cha Malawi Congress Party (MCP), kilichotawala Malawi kwa mkono wa chuma chini ya dikteta Dk. Hastings Kamuzu Banda, tangu 1964 hadi 1994.

Hiyo ni mifano mitatu tu ya nchi zilizo jirani ya Tanzania. Kuna mifano mingine pia barani Afrika na nje ya mipaka ya Afrika.
Kwa mfano, nchi kadhaa za Ulaya ya Mashariki, ikiwamo Urusi, zilikuwa na vyama vilivyokuwa madhubuti zaidi ya KANU, UNIP, MCP na hata CCM, na ambavyo havikuwa na mwisho mwema. Baadhi vilisalimika visizame na kutoweka kabisa lakini ni kama vilivyokufa.
Wanaoamini kwamba tunaanza kuushuhudia mwanzo wa mwisho wa CCM kama chama tawala wanasema kwamba ingawa CCM iliyopata pigo ina uzoefu mkubwa wa kuweza kujizoazoa wakati wa uchaguzi mkuu na kuwa kitu pamoja, safari hii hali ni mbaya na inahatarisha uhai wa chama hicho kilicho kikongwe katika ukanda mzima wa Afrika ya Mashariki.
Ukweli wa mambo ni kwamba mpaka sasa hatujui nini itakuwa hatima ya CCM kutokana na matokeo ya uchaguzi wa ndani ya chama hicho uliomchagua Magufuli.
Ni wazi kwamba uchaguzi huo umewavuruga baadhi ya vigogo wa chama hicho, pamoja na wenye kuhisi kwamba wao ndio wenye kukimiliki chama.
Miongoni mwao ni Edward Lowassa aliyeamini kwa dhati kwamba hakuna lililoweza kumzuia asichaguliwe kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM.
Lowassa alikuwa na sababu nzito za kumfanya aamini hivyo. Alikuwa na mtandao madhubuti wa kumpigia debe, alikuwa na fedha nyingi mno, pengine zaidi ya za mahasimu wake wote zikijumlishwa pamoja.
Aidha, akitegemea umaarufu wa jina lake kwamba utazidi kumnyanyua ndani ya CCM.
Sababu zote hizo zilimfanya aamini kwamba ushindi utakuwa wake. Yeye pamoja na wapambe wake wakaanza kujinata kwamba akiungwa mkono na wanachama wengi zaidi wa CCM pamoja na hata Watanzania wengine wasio katika CCM.
Hata hivyo, licha ya nguvu zake zote hizo, za kweli na za kujidhania, Lowassa hakuwa na ubavu wa kuweza kupambana na lile dubwasha ambalo wenye kulijua wanaliita “the system”.
Ni taabu kulielezea dubwasha hilo sawasawa, jinsi lilivyo na linavyofanya kazi. Labda, kwa mkato, niliite “dola kivuli”. Hili ndilo lililomkataa Lowassa asiiongoze Tanzania. Linaamini, kama tunavyoamini wengi wetu, kwamba jina “Lowassa” linanuka ufisadi na kwamba itakuwa aibu tupu kwa taifa la Tanzania iwapo litaongozwa naye.
Waliomo kwenye dubwasha hilo lisilo rasmi ni watu wenye vyeo rasmi katika serikali, hususan, katika Usalama wa Taifa na taasisi nyingine za ulinzi, na pia katika ngazi za juu za chama cha CCM.
Nao wanawatumilia watu wa nyendo mbalimbali za maisha wenye ushawishi katika jamii, wakiwa pamoja na waandishi habari. Kwa jumla, wanaamini kwamba Tanzania daima iwe mikononi mwa CCM, ili waweze kuihodhi na kuidhibiti nchi.
Mitandao aina hii humea katika nchi zenye mifumo tofauti ya kisiasa. Lakini aghalabu huwa na nguvu zaidi katika nchi zenye mfumo wa chama kimoja tu cha kisiasa au zile ambazo, kama Tanzania, zamani zilikuwa na mfumo aina hiyo.
Viongozi wengi wanaliogopa dubwasha hilo kwa sababu wanajuwa kwamba linaweza likawameza wazimawazima. Ndiyo maana viongozi wa CCM wa Zanzibar mara kwa mara huonekana wakibadili misimamo yao, hasa kuhusu suala la Muungano.Huwa wanaliogopa hilo dubwasha.
Pengine ndilo pia lililomvunja nguvu Rais Jakaya Kikwete asimuunge mkono Lowassa, ikiwa huko nyuma alikuwa akimuunga mkono.
Kikwete akijua wazi kwamba waliomo kwenye dubwasha hilo hawakumtaka Lowassa. Ndiyo maana jina lake likafutwa na mapema miongoni mwa wana CCM waliozingatiwa na Kamati ya Maadili ya chama hicho pamoja na Kamati Kuu.
Jina la Lowassa lilipoondolewa ilidhihirika kwamba kwa kweli alikuwa dhaifu na hakuweza kuhimili vishindo vya kumzuia asisogezwe mbele zaidi kuwa mgombea wa CCM ili baadaye, akishinda, awe Rais wa Tanzania.
Udhaifu wake ulipodhihirika akabadili mbinu. Badala ya kutaka awe yeye Rais, akaridhika awe muamuzi wa nani achaguliwe na chama chake afikie lengo hilo.
Alitambua kwamba alikwishadhoofishwa asichaguliwe, lakini alihisi kwamba alikuwa na nguvu za kutosha za kuweza kumbeba mwingine kwa vile alikwishatambua kuwa yeye mwenyewe alikuwa habebeki.
Ndipo jicho lake lilipomuangukia Balozi Amina Salum Ali, aliyekwishasema zaidi ya mara moja, tena hadharani, kwamba hatomtupa Lowassa. Duru za ndani ya CCM zinadokeza kwamba kura za waliokuwa wakimuunga mkono Lowassa zilimbeba Amina na kwamba yeye ndiye aliyeshinda.
Dokezo hilo linawajibu wenye kuuliza: kwanini kura za mwisho zisihesabiwe na kutangazwa usiku, zikawekwa uporo hadi siku ya pili?
Jina la Lowassa liligeuka kuwa mkosi na, wakati huohuo, kitendawili kwa CCM. Hamna shaka yoyote kwamba chama hicho kingeliathirika vibaya lau kingelimkubali Lowassa awe mgombea wao wa Urais;lakini na kwa kumkataa, nako pia kumekiathiri chama.
Haya si matokeo ya kushangaza kwa chama kilichopoteza dira. Chama hiki kimejipatia sifa mbovu ya kufuga mafisadi na viongozi wasiofaa, kifikra, kiutendaji na kwa kukosa maadili ya uongozi bora. Baadhi yao wamo chamani ili kujineemesha wao binafsi na walio wao.
Ndani ya chama mafisadi wamepiga mahema yao katika ngazi tofauti; chama chenyewe kinaendeshwa kwa njia za kifisadi, tangu mashinani hadi juu. Ikiwa katika ngazi za chini, kwenye matawi, watu wanachaguana kwa kuhongana hali ya mambo si salama hata kidogo katika ngazi za juu ambako wenye kutakiwa kutoa mfano mwema wenyewe hawashikiki kwa ufisadi.
Mporomoko wa maadili ndani ya CCM haukutokea kwa ghafla, kwa mkupuo mmoja. Maadili ya chama hicho yamekuwa yakipuputika kidogokidogo kwa miaka sasa.
Wenye kuona mbele ndani ya chama, akina Joseph Butiku, Salim Ahmed Salim na Jaji Joseph Warioba, wote wa Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere, wamekuwa wakiwaonya viongozi wenzao kwamba wanaelekea kubaya. Lakini hawakusikilizwa na wangali hawasikilizwi. Imefika hadi kwamba hii leo chama hicho kinapojiangalia katika kioo hakijitambui.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, amekuwa akionyesha moyo wa kutaka kuleta mageuzi ndani ya chama hicho. Sijui kama jitihada zake zilikuwa za kweli au la, lakini hakufanikiwa. Ikiwa jitihada hizo zilikuwa za kweli inashangaza kwamba hakujiuzulu.
Vyama vingine huenda vikawa na yao pia lakini tunakiangaza CCM kwa sababu licha ya kuwa chama kikongwe, tena chenye hatamu za uendeshaji wa taifa, kinatuchezea akili. Ubaya wa mambo ni kwamba kinafanya hivyo kikiwa hakina nidhamu.
Yote haya yanatokea kwa sababu ya ukosefu wa uongozi ulio imara, ulio na uadilifu na wenye kufuata msimamo na itikadi inayofahamika. Siasa za ndani ya chama zinazidi kuwa siasa za kupikiana majungu.
Ndiyo maana tunaziona njama za kutosana zikipikwa katika mahema fulani ya ndani ya chama. Kila mmoja wa viongozi wake anavutia upande wake na katikati mpini wenye kukihimili chama ushaanza kurega. Na sasa jina la Lowassa limeanza kuwa kitisho kwa uhai wa chama.
Inavyoelekea ni kwamba Lowassa atafanya kila aliwezalo, ndani ama nje ya chama, kuwatia adabu viongozi wenzake wa CCM waliomkosesha nafasi ya kuwa mgombea wa urais wa chama chao. Kisasi chake hakitokuwa na mpaka. 


- See more at: http://raiamwema.co.tz/jina-%E2%80%9Clowassa%E2%80%9D-na-hatima-ya-ccm#sthash.R6sLoAQz.dpuf


No comments :

Post a Comment