zanglassworks

AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, July 22, 2015

Kingunge: Mkomunisti msaliti au mfukuzia dinari chafu?

Image result for kingunge ngombale mwiru
Kingunge Ngombale Mwiru!
KAMA kuna mwanasiasa machachari aliyewahi kuteka siasa za nchi hii na katika kutetea siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kuelekea Ukomunisti kuliko hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwanasiasa huyo si mwingine bali ni Kingunge Ngombale Mwiru.
Umaarufu wa Kingunge katika medani za siasa nchini ulivuma Afrika Mashariki nzima kiasi kwamba, wenzetu wa Kenya walidhani jina “Kingunge” lilikuwa ni cheo cha madaraka kisiasa na kuwaita wanasiasa wote wazito nchini “Vingunge”, kwa maana ya wenye madaraka makubwa na wazito kisiasa. Neno na sifa hii imedumu hadi leo.
Enzi hizo, kufuatia kutangazwa kwa Azimio la Arusha, Februari 1967, zilikuwa za Kingunge Ngombale Mwiru kujitangaza dhamiri na dhamira yake kwa Tanzania iliyotakiwa, katikati ya migongano ya kitabaka iliyowakilishwa na kambi mbili kinzani; yaani Kambi ya Ubepari (Capitalist Roaders all the Rightists), ambayo ilitakiwa kupigwa vita na kung’olewa; na Kambi ya Kijamaa (Socialist Roaders all the Leftists) iliyopaswa kusimikwa, kulindwa na kuimarishwa.
Kwa kambi ya Ujamaa ambayo Kingunge alikuwa mtetezi wake mkuu, Azimio la Arusha lilikuwa ndio njia na msingi mkuu kwa safari ya kujenga usawa na uchumi wa taifa unaojitegemea ili kuondokana na adha ya ubepari na ubeberu wa kimataifa.

Kwa kambi ya Ubepari, wazo la Kujitegemea lilikuwa aina fulani ya mzaha na kichekesho chenye hatari kubwa.
Jambo moja la kutambua hapa ni kwamba, “Ujamaa” au “Udugu” unahusu usawa wa binadamu na ujenzi wa mazingira ya kisosholojia ambamo watu wote ni sawa kibinadamu wenye fursa sawa katika kujipatia mahitaji na nyenzo za kuendesha maisha bora.
Aidha, Ujamaa si adui wa umiliki wa mali au utajiri binafsi, ila tu pale utajiri huo unapotumikia vibaya kuzuia utekelezaji wa madhumuni ya Ujamaa.
Kingunge Ngombale Mwiru pamoja na Mwasisi wa Azimio la Arusha, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, waliishi maisha yasiyo yao. Walifanya kazi siku saba kwa juma, kutoka alfajiri hadi machweo. Kwa Mwalimu Nyerere, watumishi wa Ikulu na mawaziri walikuwa tayari kwa wito saa 24 kwa siku, siku saba kwa juma.
Mtu aliyekubali kuwa mfuasi wa Mwalimu kikazi, alipaswa kuwa muumini wa alichoamini yeye (Mwalimu) katika uongozi wa nchi; alitakiwa kuwa mvumilivu mwenye kujitoa na kujitolea, huku akiamini njia ya kupita atakayoambiwa. Kwa maneno mengine, alitakiwa kuacha vyote na kumfuata katika ujenzi wa jamii yenye usawa.
Lakini majaribu njiani yalikuwa mengi na makubwa kiasi cha wengi kudondoka. Kubwa kati ya hayo ni pale ilipotangazwa “Miiko” ya Viongozi (Leadership Code) iliyotaka, pamoja na mambo mengine, viongozi kutokuwa na mishahara miwili, wasiwe waajiri wala kuwa na nyumba ya kupangisha.
Hatua hiyo iliua matumaini ya viongozi wenye uchu wa kujilimbikizia mali kama sehemu ya “kula na kufurahia matunda ya uhuru” kwa gharama ya umma masikini.
Mwalimu alifariki Oktoba 14, 1999 mjini London, alikokwenda kutibiwa ugonjwa wa kansa ya damu, akiwa ameng’atuka madarakani miaka 14 iliyopita wakati huo.
Kuanzia mwaka 1985, Mwalimu alipong’atuka, kambi ya Usoshalisti ilianza kuyumba na watetezi wake kugeuka kuwa viumbe vilivyokuwa hatarini kutoweka, akiwamo Kingunge mwenyewe, aliyeanza kulegea, hasa kufuatia kupigwa mweleka kwa Azimio la Arusha na Azimio na Zanzibar mnamo mwaka 1992.
Itakumbukwa kuwa, Kingunge ametumikia awamu zote nne za serikali, akibakizwa mahususi si kwa umahiri wa kuongoza, bali kwa sababu moja tu: “Kulinda na kusimamia sera za Ujamaa kwa kila awamu aliyoteuliwa kutumikia kama Waziri”.
Ndiyo kusema kwamba, bila machachari ya “kuhubiri” na kusimamia Ujamaa nchini, Kingunge asingeweza kuukwaa Uwaziri.
Lakini Mzee Kingunge Ngombale Mwiru anafahamika kwa “usaliti” wa chinichini kwa mamlaka za juu na kwa chama, si juzi, jana wala leo pekee, bali hata kesho kwa maana ya kuwa mtu asiyetabirika wala kutegemewa kwa yale anayohubiri.
Mwaka 1983, wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere, ilikuwa aukwae U-Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kama mfumo wa Usalama waTaifa usingemtonya Mwalimu na kumtaka aondoe mikono juu ya bega la “kada” huyo wa chama aliyedhani alifaa kuitwa “mwana mpendwa”, wakati ilikuwa kinyume chake.
Kabla ya hapo, enzi za chama cha “Tanganyika African National Union” – TANU, alifanywa kuwa Mkuu wa Mkoa na hivyo Mjumbe wa Bunge kwa mfumo wa enzi hizo. Alikuwa jasiri vya kutosha kiasi cha kukataa na kuchanachana Muswada wa Serikali Bungeni kwa mshangao wa wengi, chini ya utawala wa chama kimoja, na kwa kufanya hivyo akachokoza hasira ya watawala.
TANU, kama chama tawala kilikuwa kikali ilipohusu suala la maadili ya chama na nidhamu kwa watendaji wake; hatua zikachukuliwa haraka kwa Kingunge kufukuzwa uongozi kwa kuzomewa; akiitwa majina mbali mbali ya ovyoovyo, kama vile, “Mtafuta Umaarufu”, ikatangaza Redio Tanzania; “Mnafiki Mkubwa”, likaandika gazeti la serikali – The Daily News.
Wakati mmoja, kabla ya hapo, alichokoza ghadhabu ya Mwalimu, pale alipomtuhumu (Mwalimu) hadharani, kwamba alikuwa anaipeleka nchi kwenye “Ujamaa” polepole mno na kimzaha. Mwalimu alimsamehe kwa hilo, akimwona kama mfuasi mchanga wa siasa za Ki-Marx (Marxism) asiye na weledi wala uchambuzi wa kutosha juu ya sera hizo.
Kingunge Ngombale Mwiru wa leo, japo ya kuwa na rekodi ya kutotabirika kiuongozi huko nyuma, si Kingunge yule wa enzi za TANU na Azimio la Arusha, aliyetema cheche katika kutetea “usawa” wa kijamii.
Mwaka 2007, aliishangaza dunia ya wapenda haki na wanyonge wa nchi hii, pale alipotetea viongozi mafisadi waliotajwa na mbunge mmoja katika orodha ya watu wachafu wenye kulitia aibu Taifa – “List of Shame”, yeye (Kingunge) alidai kwamba, viongozi wote wa serikali ni safi, wakati akijua fika kwamba ilikuwa ni kinyume chake.
Leo, ana lipi la kutuambia, baada ya kuibuka kwa kashfa za IPTL, EPA, Meremeta, Tegeta Escrow Account, na ufisadi mwingine mwingi wa kipindi hicho?.
Miaka michache iliyopita, Mzee wetu, Kingunge Ngombale Mwiru, alipandisha mori ya vijana wasaliti wa chama dhidi ya uongozi wa kitaifa wa chama na serikali; na kuunda kamati iliyopendekeza kwamba, Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kuonekana kuwa ameshindwa kudhibiti madaraka ya urais na uenyekiti kwa pamoja, achague moja kati ya vyeo hivyo viwili na kuachia ngazi kwa kingine.
Kwa nini jambo hilo halikupelekwa kwenye vikao sahihi vya chama lijadiliwe? Kwa nini Mzee wetu aliridhia jambo hilo kama si usaliti na uasi ndani ya chama na serikali?.
Kwa yote hayo, hatukushangaa pia kumsikia Mzee Ngombale hivi karibuni, wakati wa mchujo wa watia nia wa nafasi ya urais wa chama cha CCM, akilalamika na kukandia kwa nguvu zote na kwa hasira ya mkizi, kuenguliwa kwa jina la Lowassa ambaye sifa yake ya uongozi si ya kutamani sana kutokana na kashfa zinazomwandama, na zenye kufahamika na kila Mtanzania mwenye kuitakia mema nchi hii.
Inamshangaza kila mwanasiasa makini wa nchi hii, kuona mwanasiasa mwenzao kama Kingunge Ngombale Mwiru, kada wa chama aliyewahi kuwa Mkuu wa Chuo cha Chama, Kivukoni; Katibu Mkuu wa TANU Youth League (TYL) na Ofisa Elimu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), akigeuka “Yuda Iskariote” dhidi ya wanyonge wa nchi hii.
Inashangaza kumwona mtu aliyefikiriwa kuwa “Kamusi” ya Ujamaa wa Tanzania na mwandishi wa Mwongozo wa TANU 1971, akiisaliti dhamiri yake bila hofu kwamba dhambi hiyo inaweza kumpeleka “motoni”.
Nimalize kwa kunukuu ujumbe mfupi wa simu (sms) kutoka kwa mmoja wa wasomaji wangu hivi karibuni juu ya “usaliti” huu, akisema: “Ama kweli, “Pecunia non olet” (sarafu haina harufu); Kingunge Ngombale Mwiru, aliyemvuruga Lowasa mwaka ule 1995 mbele ya Mwalimu Nyerere, kuwa hana chembe ya sifa ya kuwa Kiongozi Mkuu wa nchi yetu, ndiye huyuhuyu anayesimama tena sasa kumtangaza Lowassa kuwa anafaa na (eti) hakuna zaidi yake?”.

- See more at: http://raiamwema.co.tz/kingunge-mkomunisti-msaliti-au-mfukuzia-dinari-chafu#sthash.OfveGLT6.dpuf

No comments :

Post a Comment