STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 16.07.2015
MGOMBEA nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli leo amewasili Zanzibar na kupata mapokezi makubwa akiongozana na Mgombea wake Mwenza Samia Suluhu Hassan na kuwaahidi Wazanzibari kuwa hatowaangusha.
Viongozi hao ambao wamewasili Zanzibar kwa ajili ya kutambulishwa sambamba na kutoa shukurani kwa kuungwa mkono na WanaCCM kwa kuteuliwa katika vikao vilivyofanyika hivi karibuni huko mjini Dodoma.
Mwenyeji wao Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia, ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliwatambulisha rasmin viongozi hao kwa wanaCCM na wananchi waliohudhuria katika viwanja vya Ofisi ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar.
Dk. Magufuli aliwahutubia wanaCCM na wananchi waliohudhuria katika mapokezi hayo makubwa yalioanzia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume na kuishia Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui ambapo kabla ya utambulisho huo alizuru kaburi la Muwasisi wa Mapinduzi Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na kumuombea dua.
Katika hotuba yake alitoa ahadi kwa WanaCCM na wananchi wa Zanzibar kuwa hatowaangusha na kuwahakikishia kuwa atashirikiana nao ili Tanzania izidi kupata maendeleo ya kutosha.
Alisema kuwa katika mchakato wa kutafuta mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kulikuwa na makundi 42 ndani ya CCM lakini hivi sasa limebaki kundi moja tu la CCM na kuwataka WanaCCM kushikamana kwani umoja ndio ushindi.
Alisema kuwa katika mchakato wa kutafuta mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kulikuwa na makundi 42 ndani ya CCM lakini hivi sasa limebaki kundi moja tu la CCM na kuwataka WanaCCM kushikamana kwani umoja ndio ushindi.
Dk. Magufuli (56) ambaye pia, ni Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Chato, Mkoa wa Geita amepata nafasi hiyo kwa kupata kura 2,104 kati ya kura halali 2,416 zilizopigwa na wajumbe 2,422 wa mkutano huo ambapo alisema kuwa lengo lake ni kuwatumikia wananchi wote bila ya kujadi itikadi zao za kisiasa huku akiahidi kuwa ana deni kubwa sana lakini atajitahidi kwa uwezo wake wote kulilipa.
Mgombea huyo wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano aliendelea kuahidi kutoa ushirikiano wake kwa wananchi ili Tanzania iweze kusonga mbele kwa kasi kubwa.
Aidha, alieleza umuhimu wa kulinda umoja na mshikamano na kusisitiza kuwa bila ya umoja maendeleo hayatopatikana na kutoa mfano kwa nchi nyingi zilizosambaratika duniani ambazo zilifikia hatua hiyo kutokana na kutokuwepo umoja miongoni mwao.
Dk. Magufuli pia, alitumia fursa hiyo kwa kuahidi kutekeleza Ilani ya CCM wakati utakapofika hasa kwa kuzingatia mambo mbali mbali yameelezewa katika Ilani hiyo yakiwemo, biashara, kilimo, uvuvi, ujnezi, barabara gesi na mengineyo.
Alisema kuwa yeye, Rais Dk. Shein pamoja na Mgombea wake mwenza Samia Suluhu Hassan wataendelea kuitetea CCM, wataendelea kuutetea Mungano sambamba na maendeleo ya Watanzania wote.
Sambamba na hayo, Dk. Magufuli alitumia fursa hiyo kumpongeza na kumsifu Dk. Shein kuwa ni kiongozi mwenye huruma, anayependa wananchi wake wote asiye na majivuno na anaependa maendeleoa na kuahdi kushirikiana nae ili kuipa ushindi CCM.
Nae Mgombea Mwenza Samia Suluhu Hassan alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa mapokezi hayo makubwa pamoja na kutoa shukurani kwa viongozi kwa kujali nafasi za wanawake huku akiwataka wanawake wote wa vyama vyote kuipigia kura CCM wakati utakapofika kutokana na kuwajali wanawake.
Mapema Dk. Shein aliendelea kutoa shukurani kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa kusimamia vizuri demokrasia na kuweka historia ndani ya chama hicho sambamba na uchaguzi na vikao vyote vya CCM vilivyomalizika hivi karibuni huko Dodoma na hatimae kuwapata viongozi watakaopeperusha bendera ya CCM wakati utakapofika.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Magufuli, Mgombea wake mwenza, viongozi wote wa CCM kwa kuendesha mchakato wa kuwapata wagombea wa chama hicho huku akielezea sifa kedekede za Dk. Magufuli ikiwa ni pamoja na uchapa kazi wake, uadilifu, mkweli kutokana na kumtambua vilivyo kwani walishafanya kazi pamoja.
Alisema kuwa Dk. Magufuli ana uwezo mkubwa unaujua Muungano na anayajua Mapinduzi na kupata nafasi hiyo ni stahiki yake na wala hakupendelewa.
Nao wanaCCM wa Mikoa sita ya Kichama hapa Zanzibar walitoa pongezi zao huku wakiahidi kuendelea kuwaunga mkono wagombea hao sambamba na kukiimarisha chama chao cha CCM.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments :
Post a Comment