zanglassworks

AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, July 25, 2015

Maslahi ya CUF yapo ndani ya UKAWA

Image result for cuf of tanzania

Na Njonjo Mfaume
NANI anamuhitaji mwenzake zaidi katika UKAWA, CUF au Chadema? Changamoto gani zinaukabili UKAWA zinazoweza kutishia uhai wake?
UKAWA ukitengemaa nani atafaidika, na ukitetereka nani atapoteza zaidi? Natamani ningejua majibu ya maswali haya. Ukweli ni kuwa sijui ila huu nitakaoandika hapa ni mtazamo wangu tu.
Chadema ni chama kikubwa cha Upinzani kwa sasa. CUF kinafuata kwa ukubwa. Hata hivyo, kati ya vyama hivi viwili, kila kimoja kimekubalika upande mmoja zaidi wa Muungano. Chadema kimestawi Bara, CUF Zanzibar.
Kimsingi vyama hivi vinakubalika maeneo tofauti. Ilipo Chadema kwa wingi, CUF ni dhaifu. Ilipo CUF Chadema dhaifu. Inajulikana kuwa CUF ina nguvu sana Zanzibar, kadhalika pia katika Mikoa ya Tanga na Mikoa ya Pwani ya Kusini. Chadema ina nguvu sana Mikoa ya Kaskazini na Nyanda za Juu Kusini (huenda si wilaya zote za mikoa hiyo).
Maeneo mengine ya nchi, kama Dar es Salaam na Kanda ya Ziwa, vyama vyote viwili vina nguvu kutegemeana na asili na hali ya wilaya hadi wilaya.
Vyama hivi viwili vina nguvu maeneo tofauti kwa sababu vinavutia makundi tofauti ya kijamii. CUF, chama cha watu wa hali ya chini hususan, Waswahili. Iangalie Dar es Salaam, chunguza maeneo ambayo CUF imetaga mayai: Tandale, Buguruni, Tandika.. ni maeneo ya watu wa kipato cha chini (si wote) lakini pia Waswahili fulani.Chadema ni chama pia kinachowavutia watu wa daraja la chini, lakini si wale unaoweza kuwalezea kama ‘Waswahili’. Lakini nguvu hasa ya Chadema inatokana na watu wa kipato cha kati, wasomi.
Ingawa tunakwepa kujadili dini inavyoathiri siasa Tanzania, ukweli utabaki kuwa jamii inavihusianisha vyama hivi viwili Ukristo na Uislamu. Nani atapinga ukweli kuwa kuna uhusiano kati ya ufuasi wa vyama hivi na imani za dini?
Nisiingie sana katika udini ambao kimsingi nimeutaja kusisitiza hoja yangu kuwa Chadema na CUF vinatimilizana na kwamba wafuasi wa vyama hivyo wanatoka katika makundi tofauti ya kijamii.
Hivyo basi, iwapo vyama hivi viwili vina malengo makubwa ya kuiondoa CCM madarakani, tija na ufanisi wa haraka inaweza kupatikana kwa kushirikiana. Hata vikikosa urais, ili kuiwajibisha serikali bungeni, upinzani utahitaji idadi kubwa ya wabunge. Wingi wa idadi ya wabunge utapatikana kwa kufanya kazi pamoja katika uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Kwa kuachiana majimbo na labda kata, vyama vya UKAWA vitafanikiha mambo mawili. Kwanza, vitaweka wagombea katika majimbo machache ambayo wanaamini wana nguvu na hivyo kutumia rasilimali zao chache katika eneo dogo litakalowapa mafanikio.
Pili, ushirikiano unapunguza maadui. Uzoefu wa miaka iliyopita unaonyesha jumla ya kura za wapinzani katika baadhi ya majimbo ilikuwa ni kubwa kuliko kura za CCM.
Baada ya uchaguzi, ushirikiano huu utasaidia vyama hivi kutumia idadi yao kubwa kuweza kuibana Serikali. Kwa hiyo ushirikiano wa vyama vya UKAWA hususan CUF na Chadema, ni muhimu kwa maslahi ya Taifa, lakini pia utasaidia vyama hivi kukua kwa kupata matokeo mazuri.
Uzuri ulioje kuwa vyama vikuu katika muungano huu, CUF na Chadema, vina nguvu katika maeneo tofauti na kuvutia makundi tofauti ya kijamii, jambo linalofanya vitimilizane kuliko kushindana. Ni kama mwanamke na mwanamume.
Lakini ni huu utofauti ndio unaoweka ushirikiano wa vyama vya UKAWA katika shaka, hususan, unapokuja mjadala wa suala la nani apeperushe bendera ya UKAWA katika nafasi ya urais.
Tofauti za makundi ya kijamii yanayounga mkono vyama hivi ni kubwa mno kiasi kwamba mfuasi wa kindakindaki wa Chadema akihama chama chake ataingia CCM kuliko kujiunga na CUF, na wa CUF vile vile.
Wiki iliyopita mwana CUF mmoja alisifia kampeni za wana CUF za kumsaidia Rais Kikwete mwaka 2010 ambapo wafuasi wa chama hicho waliagizwa wamchague Kikwete ili tu Dk. Willibroad Slaa asishinde.
Kutokana na tofauti za makundi ya kijamii yaliyo nyuma ya vyama vya UKAWA, sikushangaa kuibuka minon’gono kuwa UKAWA wanakaribia kusambaratika, baada ya muda mrefu wa mradi wa ujenzi wa UKAWA na kunyanyua matarajio ya Watanzania.
Mara tukasikia CUF hawapo katika kikao cha mashauriano ya vyama viliyounda umoja huo na kisha viongozi wa chama hicho wakatangaza kuwa wenye chama chao wamewavuta shati na kutaka washauriwe kwanza.
Kiufupi, kuna hali ya kutoaminiana. Kuna suala la ruzuku na kuna hofu ya suala la kutumiana, kama mshumaa unavyoangazia wengine huku wenyewe ukiisha.
Lakini kwa ujumla, ushirikiano huu ni muhimu kwa maslahi ya Taifa na hata kwa maslahi ya vyama husika hususan, CUF ambao ndio wanaotajwa kutaka kujitoa.
Ningekuwa mshauri wa chama cha CUF ningewashauri kuwa maslahi ya chama chao yapo ndani ya UKAWA kuliko nje ya UKAWA, kwa hiyo wasifanye kosa la kujitoa, walau kwa sasa.
Huu ni wakati ambao CCM wana nguvu mpya inayotokana na mgombea John Pombe Magufuli ambaye anatoa matumaini makubwa kwa Watanzania.
Huku CUF wakikabiliana na CCM, si busara kuongeza washindani wengine wakubwa kama Chadema, chama ambacho dalili zinaonyesha kimejipanga kufanya vema mwaka huu.
Kuimarika kwa Chadema kutokana na faida ambayo chama hicho kinaelekea kupata kufuatia kukatwa kwa jina la waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa katika kinyang’anyiro cha urais, hasa kwa kuwa Lowassa anatoka Kaskazini ambako ni ngome ya Chadema.
Dalili za Chadema za kujizolea wafuasi waliokuwa wakimuunga mkono Lowassa zimeanza kujionyesha. Ni ukweli mtupu pia kuwa Chadema ni imara zaidi katika ufanisi wa uendeshaji wa shughuli zake, kikijivunia hazina ya viongozi ambao tayari wana mvuto, umaarufu na uzoefu wa kutosha. Na kwa hali ilivyo, Chadema inaweza kuisumbua CUF katika ngome zake kuliko CUF kuisumbua Chadema katika ngome zake.
Shida ya wana CUF ni hisia kuwa Profesa Ibrahim Lipumba ni mtaalamu wa ajabu sana ambaye akiwa rais, yeye peke yake anaweza kuitoa nchi katika umasikini.
Wapenzi wa CUF wanatamani Lipumba awe rais kuliko wanavyotamani chama chao kupata wabunge wa kutosha na kuweka misingi ya ujenzi wa chama, mtazamo ambao si mzuri katika ujenzi wa chama.
Baada ya miaka mingi ya CUF kuvuma mno Bara bila mafanikio makubwa, hususan, upande wa ubunge, ni wakati muafaka sasa kwa CUF kuweka malengo yanayofikika kutokana na rasilimali walizonazo.
Ni muhimu vilevile CUF watumie mwamvuli wa UKAWA kupiga hatua mbele katika kukijenga chama kwa kupigania na kushinda viti vya ubunge vingi iwekanavyo.
Ushindi wa viti vya kutosha vya ubunge kutoka bara utawapa CUF uwiano mzuri wa pande mbili za Muungano. Ni jambo la aibu kwa CUF, chini ya uongozi wa Profesa Lipumba, katika miaka zaidi ya 20 ya kuwapo kwake, kuwa na wabunge wawili tu wa majimbo kutoka Bara na kila siku kiendelee kutegemea Wazanzibari kukipa viti bungeni. Na tatizo la CUf ni vipaumbele, urais kabla ya ubunge!
Binafsi itanisikitisha iwapo CUF najitoa ndani ya UKAWA eti kwa sababu Profesa Lipumba hajapewa nafasi ya kugombea urais – urais ambao hata akigombea hataupata; na pia mantiki inaonyesha hawezi kupeperusha vema bendera ya UKAWA kuliko Dk. Slaa.
Profesa Lipumba amegombea mara nyingi mno na kwa sasa hana mvuto tena ila kwa wafuasi wake wa kindakindaki, wanaoamini uprofesa wake wa ajabu unaweza kutibu matatizo yote ya nchi hii.
Rekodi za Profesa Lipumba zinaonyesha kuwa alishapita kilele cha umaarufu wake wa kisiasa na kwa sasa hana mvuto tena.
Mwaka 1995 aligombea kwa mara ya kwanza akapata asilimia 6.43%, mwaka 2000 alipokuwa katika kilele cha umaarufu wake alipata asilimia 16.26% na baada ya hapo asilimia ya kura zake imekuwa zikishuka ambapo mwaka 2005 alipata asilimia 11.68% na mwaka 2010 alipata asilimia 8.28%.

- See more at: http://raiamwema.co.tz/maslahi-ya-cuf-yapo-ndani-ya-ukawa#sthash.7VdvKse5.dpuf

No comments :

Post a Comment