STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
21.07.2015
WAZIRI Mkuu Mstaafu wa Kenya Mhe. Raila Amolo Odinga amepongeza hatua za uimarishwaji wa uchumi na maendeleo uliofikiwa hapa Zanzibar hali ambayo imeendelea kuijengea hadhi na sifa kubwa Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo katika nchi za ukanda wa Afrika ya Mashariki.
Waziri Odinga alisema kuwa hatua hiyo sio ngeni kwa Zanzibar kwani imekuwa ikitambulikana kwa muda mrefu kutokana na hisrtoria yake kubwa ya kuimarisha sekta zake za maendeleo ikiwemo biashara na nyenginezo kutokana na juhudi nzuri za viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Waziri Mkuu huyo Mstaafu aliyasema hayo leo huko Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo naWaziri wa Nchi Afisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora, Mhe. Dk. Mwinyihaji Makame.
Mhe. Odinga ambaye yuko Zanzibar akihudhuria Mkutano wa Kuimarisha Masuala ya Ushirikiano Katika amani, usalama na maendeleo kwa nchi za Afrika Mashariki, unaofanyika hapa Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Rais Mstaafu wa Zanzibar Mhe. Amani Abeid Karume.Alisema kuwa Kenya inathamini uhusiano wa kihistoria uliopo kati yake na Zanzibar tokea wakati wa ukoloni na kusisitiza kuwa wakati huo Zanzibar iliweza kutajika kutokana na shughuli zake mbali mbali za kimaendeleo ikiwemo biashara katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki jambo ambalo imeijengea sifa hadi hii leo.
Waziri Mkuu Odinga alieleza kuwa kutokana na uhusiano sambamba na mafanikio yaliopatikana kwa Zanzibar pamoja na nchi ya Kenya kuna kila sababu ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano wake huo wa kihistoria kwa manufaa ya pande zote mbili.
Alieleza kuwa anatambua umuhimu wa kuwepo uhusiano kati ya Kenya na Zanzibar na kusisitiza kuwa ipo haja kwa kuimarishwa zaidi mahusiano kwa nchi za Afrika ya Mashariki ili uchumi wa nchi hizo uzidi kuimarika zaidi.
Sambamba na hayo, Waziri Mkuu huyo alipongeza mafanikio makubwa yaliopatikana katika kuendeleza, kuutunza na kuuthamini Muungano uliopo kati ya Tanganyika na Zanzibar.
Aidha, Waziri Odinga alisisitiza haja ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kibiashara na hata masuala ya ujasiriamali kati ya Kenya na Zanzibar kwa lengo la kuimarisha zaidi mashirikiano kati ya pande mbili hizo.
Nae Waziri Dk. Mwinyihaji Makame alimpongeza Waziri Mkuu huyo wa Kenya kwa kuendelea kuthamini uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Kenya na Zanzibar na sambamba na kuendeleza utamaduni wake wa kuja kusalimiana na viongozi wa Zanzibar kwa kila anapopata nafasi ya kufika Zanzibar.
Dk. Mwinyihaji alimueleza Waziri Odinga kuwa uhusiano na ushirikiano wa Kenya na Zanzibar una historia kubwa na kuna kila sababu ya kuendeleza na kudumishwa kwa manufaa ya pande zote mbili.
Katika maelezo yake, Dk. Mwinyihaji alitumia fursa hiyo kumueleza Kiongozi huyo mstaafu wa Kenya mafanikio makubwa yaliofikiwa hapa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa uchumi wake kutoka asilimia 4.3 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 7.0 mwaka 2014 sawa na ongezeko la asilimai 2.7.
Dk. Mwinyihaji alimueleza Waziri Mkuu huyo Mstaafu kuwa Pato la Taifa kwa mwananchi mmoja mmoja limekuwa kutoka Tsh. 856,000 ($613) kwa mwaka 2010 hadi kufikia Tsh. 1,552,000 ($939) kw mwaka 2014, hali ambayo imeonesha mafanikio makubwa.
Aidha, Dk. Mwinyihaji alitumia fursa hiyo kumueleza Waziri Mkuu Odinga kuwa kwa upande wa mfumko wa bei katika mwaka 2010, mfumko wa bei ulikuwa wa wastani wa asilimia 6.1 na kushuka hadi kufikia wastani wa asilimia 5.6 katika mwaka 2014.
Alieleza kuwa Sekta Binafsi imekuwa na mchango mkubwa kwa kuimarisha uchumi hapa Zanzibar hivyo mashirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta hiyo yamekuwa mazuri hali ambayo imepelekea kuimarika kwa uchumi wa Zanzibar kila kukicha.
Sambamba na hayo, Dk. Mwinyi alieleza kuwa amani, umoja na utulivu ndio misingi mikubwa ya maendeleo hapa Zanzibar hali ambayo imepelekea kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo chini ya muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Akizungumzia suala la ajira, Dk. Mwinyihaji alimueleza Mhe. Odinga kuwa suala hilo ni suala mtambuka duniani kote lakini hata hivyo, kwa upande wa Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein imeanzisha Mfuko wa Uwezeshaji kwa lengo la kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana na wanawake sambamba na kuwajengea uwezo wa kipato wananchi.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments :
Post a Comment