Ameihama CCM kwa kile alichodai kufanyiwa mizengwe ya mara kwa mara na viongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya.
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyeshindwa kura za maoni za ubunge katika Jimbo la Bunda, mkoani Mara, Maximillian Madoro, amejiondoa kwenye chama hicho na kuomba uanachama wa chama cha Democratic Party (DP) ili awanie ubunge jimbo hilo.
Awali Madoro alikuwa Diwani wa CCM kata ya Nyamuswa, wilayani Bunda.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Madoro alisema ameihama CCM kwa kile alichodai kufanyiwa mizengwe ya mara kwa mara na viongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya.
Alidai katika uchaguzi huo wa kura za maoni aliwekewa mizengwe ya kila aina na viongozi wa CCM ngazi ya wilaya, ikiwamo kumtangaza ameshika nafasi ya tatu kwa kupata kura 1,935 katika kinyang’anyiro hicho wakati alikuwa mshindi wa pili kwa madai ya kupata kura 2,276.
Akieleza kilichomsukuma kugombea ubunge katika jimbo hilo kupitia DP, Madoro alisema lengo ni kutaka kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo hilo katika sekta ya elimu, maji, afya na miundombinu.
Mwenyekiti wa CCM Wilayani Bunda, Chacha Gimanwa, alithibitisha kada huyo kukihama chama hicho na kukanusha kufanyiwa mizengwe, akisema amehama kwa utashi wake baada ya kukosa nafasi ya kuwania ubunge kupitia chama hicho.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment