Ushindani halisi utakuwa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambavyo vimeweka utaratibu wa kumsimamisha mgombea mmoja katika nafasi hizo ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imetangaza idadi ya majimbo ya uchaguzi kuwa ni 265.
Hata hivyo sehemu ya ushindani mkubwa katika nafasi za ubunge kwa upande wa Tanzania Bara unatarajiwa kwenye majimbo yafuatayo:
UBUNGO
Jimbo hili lilikuwa likishikiliwa na Chadema kwa kipindi cha miaka mitano tangu uchaguzi wa mwaka 2010. Awali, Mbunge wake alikuwa Charles Keenja wa CCM. Tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, mbali na John Mnyika wa Chadema Ubungo imewahi kuwakilishwa na Masumbuko Lamwai (NCCR-Mageuzi).
Wagombea katika uchaguzi wa mwaka huu ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi (CCM) na Mhariri wa Mwanahalisi, Saed Kubenea (Chadema). Wote wanagombea kwa mara ya kwanza.
ILALA
Jimbo hili ni kitovu cha jiji la Dar es Salaam kutokana na ofisi nyingi za serikali ikiwamo Ikulu kuwa katika jimbo hili. Kwa sasa linashikiliwa na Mussa Azzan Zungu (CCM) ambaye anawania kwa mara nyingine baada ya kuongoza kwa vipindi viwili tangu mwaka 2005.Zungu atashindana kwa karibu na mgombea aliyesimamishwa kupitia Ukawa, Muslim Haiderally Hassanali (Chadema) ambaye ni mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema. Hassanali anatajwa kuwa na wafuasi wengi maeneo mengi ya jimbo hilo.
KINONDONI
Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi 1992, jimbo hili limekuwa ngome ya CCM. Kwa sasa linawakilishwa na Idd Azzan. Mpaka sasa Ukawa inaendelea kutafakari mtu wa kumsimamisha kupambana na Azzan.
KAWE
Jimbo hili limeongozwa na Halima Mdee (Chadema) tangu 2010 baada ya kushikiliwa na CCM tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza. Uchaguzi huu CCM imemsimamisha Kippi Warioba.
UKONGA
Unaweza kuiita ngome ya CCM kutokana na wagombea wake kushinda kwa kipindi kirefu. Ni jimbo lililokuwa linaongozwa na marehemu Eugene Mwaiposa.
Ugumu wa jimbo hili unafuatia pale aliyekuwa Meya wa Ilala, Jerry Slaa kuwania nafasi ya kuliongoza kupitia CCM, huku Ukawa wakimsimamisha Mwita Waitara (Chadema).
KIBAMBA
Ni jimbo jipya ‘lililomegwa’ kutoka Ubungo ambapo kila chama kikiwania kuliongoza.
Ukawa imemsimamisha John Mnyika (Chadema) wakati CCM imemsimamisha Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenela Mkangala. Chama cha ACT-Wazalendo, kimemsimamisha Mwandishi wa habari, Dickson Amos Ng’illy.
SEGEREA
Lilikuwa likiwakilishwa na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga (CCM) ambaye kwa sasa amehamia Chadema baada ya ‘kukatwa’ katika kura za maoni.
Hivyo ni jimbo linalotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kati ya Bonna Kaluwa (CCM) na Julius Mtatiro wa CUF anayeungwa mkono na Ukawa.
IRINGA MJINI
Ushindani mwingine upo katika jimbo hili, baina ya Fredrick Mwakalebela (CCM) na Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).
Wagombea wote wana mvuto kwa wananchi wa Iringa Mjini hasa vijana. Mchuano katika jimbo hilo unatarajiwa kuwa mkali hasa ikizingatiwa kwamba Mwakalebela alishinda kura za maoni mwaka 2010 lakini vikao vya juu vya CCM ‘vikamkata’.
Mbunge wa sasa, Mchungaji Msigwa ameliwakilisha jimbo hilo kwa miaka mitano.
ARUSHA MJINI
Ushindani mkubwa unatarajiwa kuwapo jimboni humo kutokana na wagombea wawili wenye ushindani mkubwa, Mbunge anayemaliza muda wake Godbless Lema (Chadema) na Phillemon Mollel (CCM).
BUNDA MJINI
Mpambano katika jimbo hilo ulianza ndani ya CCM baada aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia Vijana, Esther Bulaya kulitaka na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira ambaye anamaliza muda wake.
Hivi sasa Bulaya, anagombea jimbo hilo kwa kusimamishwa na Ukawa kupitia Chadema baada ya kujiunga na chama hicho hivi karibuni.
MOSHI MJINI
Ni ngome ya Chadema iliyokuwa inaongozwa na Philemon Ndesamburo maarufu kama `Ndesa Pesa’, lakini kwa sasa amestaafu na kumwachia Meya wa Manispaa hiyo, Jaffar Michael.
CCM kimeamua kulikomboa jimbo hilo kwa kumsimamisha mfanyabiashara maarufu, Davis Mosha.
BARIADI MASHARIKI
Aliyekuwa anashikilia jimbo hilo, Andrew Chenge (CCM), aliyepachikwa majina lukuki ya utani yakiwamo ‘Mzee wa rada’ ‘Mzee wa vijisenti’ ‘Nyoka wa makengeza’ atapambana na Godwin Simba ( Chadema).
NYAMAGANA
Ni jimbo lenye ushindani mkubwa kutokana na historia yake ya kutoongozwa na mbunge kwa vipindi viwili tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
KilaMbunge anayeshinda jimbo hilo huongoza kwa kipindi cha miaka mitano na kisha kuondoka. Hivi sasa linaongozwa na Ezekiel Wenje (Chadema). Uchaguzi huu atakuwa na wakati mgumu wa kupamba na mgombea wa CCM, Stanslaus Mabula
ILEMELA
Jimbo hilo kwa sasa linaongozwa na Highness Kiwia (Chadema) ni mojawapo ya ngome ya Chadema kwa muda mrefu, CCM kimejipanga kulichukua jimbo hili kwa kumsimamisha Angelina Lubala.
SIMANJIRO
Ni mchuano kati ya mgombea wa CCM, Christopher Ole Sendeka na James Millya (Chadema).
Wagombea wote hawa wanapendwa na wananchi wa Simanjiro pia wana uwiano sawa wa umaarufu, kwa kuwa wote ni wazoefu katika siasa.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment