Mgombea huyo, Abdi Seif Hamad, alidai kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 17, mwaka huu majira ya asubuhi katika maeneo ya jimbo hilo. Alidai kuwa akiwa maeneo hayo wakati akitafuta wadhamini, ghafla kikatokea kikundi cha watu wapatao wanane wakiwa wamejifunika nyuso na kumteka, kumtisha kisha kumnyang’anya fomu ambazo alikuwa ametoka kuzichukua kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
“Namshukuru Mungu hawakunijeruhi wala kunipiga, waliniambia wanachokihitaji ni fomu ambazo nilizokuwa nimebeba mfukoni,” alidai Abdi.
Alidai kuwa baada ya kumnyang’anya fomu hizo walimuachia na kwenda kuripoti kituo cha polisi cha Ng’ambu na kupewa namba RB/6085/2015 kisha kuripoti Nec na jana alipewa fomu nyingine.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, alisema hajapata taarifa za kuripotiwa kwa tukio hilo.
“Watu wangu waliopo katika doria siku ya mkutano wa Chadema uliongozwa na mgombea wa urais kupitia chama hicho, Edward Lowassa, ndio walipata taarifa hiyo kutoka kwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alitoa taarifa ya tukio hilo akiwa juu ya jukwaa akiwahutubia wananchi,” alisema Mkadam.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment