Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, August 7, 2015

Mtikisiko: Ni baada ya Profesa Lipumba kujiengua uenyekiti CUF


Aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akiaga waandishi wa habari baada ya kuwatangazia kujivua wadhifa huo katika mkutano alioufanya Dar es Salaam jana.
By Nuzulack Dausen wa Mwananchi.
Dar es Salaam. Hakuna neno jingine linalofaa kuelezea hali ilivyo ndani ya Ukawa zaidi ya “mtikisiko” baada ya Profesa Ibrahim Lipumba kuamua kujivua uenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) wakati mkakati wa vyama vya upinzani kushirikiana kutaka kushika dola ukiwa umeshika kasi.
Uamuzi wa Profesa Lipumba, mmoja wa waasisi wanne wa Ukawa-Umoja wa Katiba ya Wananchi unaoundwa na vyama vinne vya Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD-,unamaanisha anapoteza wadhifa wake wa mwenyekiti mwenza wa umoja huo ambao umeamua kushirikiana kwenye Uchaguzi Mkuu kwa kusimamisha mgombea mmoja kuanzia ngazi ya urais hadi udiwani atakayeungwa mkono na vyama hivyo.
Wengine walioongoza harakati za kuasisi Ukawa ni Freeman Mbowe, ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi na Emmanuel Makaidi wa NLD.
Profesa Lipumba, mmoja wa wenyeviti wanne wa Ukawa walioeleza sababu za kumkaribisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwenye umoja huo takribani siku 10 zilizopita, jana alieleza kuwa ameamua kujivua wadhifa huo kutokana na vyama hivyo kukubali kupokea watu walioshiriki kukataa Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na wananchi, kitu ambacho kilikuwa msingi wa kuundwa kwa Ukawa.
“Nimejitahidi sana ndugu zangu kuvumilia, lakini dhamira inanisuta,” alisema Profesa Lipumba mbele ya waandishi wa habari jana kwenye Hoteli ya Peacock baada ya mkutano wa juzi aliopanga kufanyia ofisi za CUF kuzuiwa na wanachama.
“Sisi tumekaa tunaipigia kelele Rasimu ya Katiba ya (Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph) Warioba lakini iliyopitishwa ni Katiba Inayopendekezwa sasa tunawachukua waliopitisha ili waje kuisimamia. Hivi inaingia akilini?”
Lipumba aliwaomba radhi wanachama na wananchi waliomuamini wakati wote wa uongozi wake.
Tamko la maneno 900
Katika taarifa yake ya maneno 900 ambayo aliisoma mbele ya waandishi wa habari jana, Profesa Lipumba, ambaye amekuwa akibashiriwa kuchukua uamuzi huo tangu katikati ya wiki hii, alisema pamoja na kujivua uongozi hatahama CUF na kwamba ameshalipia kadi yake hadi mwaka 2020.
“Leo hii nimeikabidhi ofisi ya Katibu Mkuu barua yangu ya kung’atuka nafasi ya mwenyekiti wa taifa, lakini naendelea kuwa mwanachama wa CUF na kadi yangu imelipiwa mpaka mwaka 2020,” alisema Profesa Lipumba aliyekiongoza chama hicho kwa miaka 16.
Huku akionekana kuwa mtulivu, alisema hajashinikizwa wala kushawishiwa na mtu yeyote kujiuzulu na kwamba uamuzi huo ameufanya baada ya kutafakari sana na kushauriana na familia yake ambayo alisema imeridhia.
Mtaalamu huyo wa masuala ya uchumi alisema ameshiriki katika vikao vingi vya Ukawa vilivyowafikisha hapo walipo, lakini dhamira na nafsi vinamsuta kuwa wameshindwa kuenzi na kuzingatia tunu za Taifa za utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi na uwajibikaji.
Alipoulizwa sababu za kugeuka wakati yeye alikuwa ni miongoni mwa wenyeviti wa Ukawa waliomkaribisha Lowassa Ukawa, alikiri akisema kuwa suala la rushwa na ufisadi ni mfumo ambao lazima uondolewe lakini kwa sasa “dhamira yangu na nafsi yangu vinanisuta”.
Profesa Lipumba alipotakiwa kueleza iwapo kujiuzulu kwake kunahusiana na tuhuma za kuhongwa mamilioni na CCM ili kuusambaratisha Ukawa, alijibu:
“Yametengwa wapi? mimi sina taarifa hizo. Tulielezwa sisi tumemkaribisha kwa sababu tumepatiwa mamilioni na sasa unasema mamilioni yametengwa kusambaratisha Ukawa. Ila ninalosisitiza ni kwamba linalonipa tatizo ni dhamira na nafsi yangu, si vingine.”
Profesa Lipumba aliyekuwa ameongozana na mdogo wake Shaaban Miraji na rafiki yake Abdallah Shaaban, alisema kama mwanachama wa kawaida atashiriki kampeni za chama lakini ataendelea kuiunga mkono Rasimu ya Katiba ya Warioba.
Ukawa iliundwa mapema mwaka jana na wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka vyama hivyo vinne kupinga mwenendo wa chombo hicho cha kuandika Katiba, wakisema kilipuuza maoni yaliyokuwa kwenye Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Warioba na kuweka maoni yaliyotokana na maagizo ya CCM.
Miongoni mwa mambo yaliyozua mjadala mkubwa ni muundo wa Serikali ya Muungano baada ya Rasimu ya Katiba kupendekeza serikali tatu, na pia suala la Tunu za Taifa ambazo zilipendekezwa kuwa ni pamoja na utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya Taifa, lakini zikaondolewa.
Kikao cha dharura CUF Zanzibar
Baadaye jana jioni, uongozi wa CUF Zanzibar ulitoa taarifa ya kuitishwa kwa kikao cha dharura, huku ikiwahakikishia wanachama wake kuwa itavuka salama kwenye msukosuko huo kama ilivyofanikiwa dhoruba nyingine.
“Katika historia yake, CUF imepita katika dhoruba na misukosuko mingi lakini mara zote imeonyesha uwezo mkubwa wa kuhimili dhoruba na misukosuko hiyo na kukabiliana na athari zake. Hatuna chembe ya wasiwasi kwamba hata mtihani huu tutauvuka na tunaamini tutaibuka tukiwa chama imara zaidi,” inaeleza taarifa ya CUF Zanzibar.
“Katibu Mkuu ameagiza kuitishwa kwa vikao vya dharura vya Kamati ya Utendaji ya Taifa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa siku ya Jumapili, tarehe 9 Agosti, 2015 ili kujadili hatua hiyo na kufanya uamuzi juu ya hatua muafaka zinazopaswa kuchukuliwa katika kipindi hiki hadi hapo chama kitakapomchagua mwanachama mwingine kujaza nafasi hiyo ya mwenyekiti.”
Kuondoka kwa Lipumba kunaacha nafasi mbili za juu kuwa wazi baada ya aliyekuwa makamu mwenyekiti, Juma Duni Haji kuhamia Chadema na kupitishwa kuwa mgombea mwenza wa Ukawa kutokana na makubaliano ya kimkakati ya vyama vinavyounda umoja huo. Hali hiyo inafanya kiongozi mkuu kwa sasa kuwa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
CUF wajibu mapigo Dar
Nusu saa baada ya kutangaza kujivua uenyekiti, uongozi wa CUF jijini Dar es Salaam uliitisha mkutano wa ghafla na wanahabari kwenye ofisi za makao makuu yake zilizoko Buguruni na kueleza kuwa kama kiongozi, Profesa Lipumba ana uhuru na haki kikatiba kujiuzulu na CUF kama taasisi bado ipo imara.
“Tunakubaliana na uamuzi wake, lakini tuwaeleze wanachama wetu na Watanzania kwa ujumla kuwa uongozi wa CUF umebaki imara na unaendelea na shughuli zake kwa kufuata taratibu zote na vikao vyetu vitaendelea kama kawaida. Bado katibu mkuu yupo na viongozi wengine wapo,” alisema mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CUF, Mustafa Wandwi.
Aliwatoa hofu makada wanaogombea ubunge na udiwani akiwataka waendelee na mikakati yao ya uchaguzi kwa sababu uamuzi wa kugombea umebarikiwa na Baraza Kuu la Uongozi na hakuna mfarakano wowote ndani ya chama.
Alipoulizwa kuhusu kauli ya Profesa Lipumba kuwa Ukawa imevunja misingi na maadili wanayoiamini, alisema:
“Yeye alikuwa kiongozi wetu mkuu na aliridhia mengi kama kiongozi wa chama na yapo maandishi yanayoonyesha tulivyoridhia ndani ya Ukawa na tunaendelea vizuri bila tatizo lolote katika umoja huo.
“Kama amegundua udhaifu huo sasa, anaujua yeye kama kiongozi na mwanachama. Sisi hajatupatia taarifa rasmi katika kikao cha aina yoyote na siwezi kuyazungumzia kwa sababu kama chama hatujajadili hayo na tukijadili tutatoa maelezo.”
CUF bila Lipumba
Wakati uongozi ukieleza hayo, makada waliokuwa makao makuu ya CUF walikuwa katika makundi wakijadili kung’atuka kwa Profesa Lipumba huku wengi wakisema “CUF bila Lipumba inawezekana”.
Ili kuondoa simanzi na taharuki, walianza kushawishiana kuimba nyimbo za hamasa zikiwamo za “tuna imani na Ukawa, hoyaa, hoyaaa…tuna imani na Lowassa hoyaa, hoyaaa” na kuchagiza pia salamu ya maarufu ya CUF ya “CCM kwisha kwisha kwisha kabisa, mlalo wa chali, kifo cha mende, kwisha kabisa”.
“Taarifa za kujiuzulu imetushtua sana, mheshimiwa hakutumia hekima na busara,” alisema katibu wa vijana Kata ya Magomeni, Salim Mzee. Jana (juzi) wazee na viongozi wa dini walimwita kujadiliana lakini inaonekana alikuwa na chuki katika nafsi yake na kama kulikuwa na tatizo ndani ya Ukawa angetuita tukajadiliana lakini kama wana-CUF hatutatoka ndani ya Ukawa na tutajenga chama kuhakisha tunaing’oa CCM,” aliongeza.
Licha ya Profesa Lipumba kueleza kuondoka kwake hakuhusiani na kupatiwa mamilioni ya fedha kuvuruga Ukawa, kada Abdallah Mohamed alisema kuondoka kwa Lipumba siyo bure kuna mkono wa CCM.
“Juzi tu alikuwa akitoa kauli za wazi mbele ya vyombo vya habari kuhusu kuunganisha nguvu ya Lowassa na Ukawa CCM chali, chali, mlalo wa mende, sasa kwa hapa nani kawa mlalo wa mende?
Chadema walonga
Mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema hatua ya Profesa Lipumba kujiuzulu ni sawa na jenerali wa jeshi aliyeanguka katikati ya mapambano ya kuelekea Ikulu na harakati za mageuzi na mabadiliko alizoanza miaka 20 iliyopita.
Akizungumza nje ya Hoteli ya Ledger Bahari Beach kilipofanyika kikao cha Kamati Kuu ya Chadema jana, Lissu alisema katika mapambano kuna majenarali na askari wa kawaida, lakini Profesa Lipumba ni sawa na jenerali aliyeanguka katikati ya uwanja wa mapambano ya mabadiliko.
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), Halima Mdee alisema Profesa Lipumba alikuwa kikwazo katika maamuzi ya Ukawa.
“Sishangai kwa sababu tulikuwa tunajua kuwa yeye ndiyo kikwazo cha Ukawa tangu mwanzo wa vikao vyetu. Alikuwa na sababu nyingi, akimaliza hii anaibua nyingine,” alisema Mdee.
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alimfananisha Profesa Lipumba na abiria wa treni anayeamua kushukia njiani kabla hajafika anakokwenda.

No comments :

Post a Comment