Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, August 17, 2015

Sasa Tanzania kuongozwa kidikteta au kijeshi?


MWEZI Agosti mwaka 1990, akiwa anastaafu uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwalimu Julius Nyerere, alizungumza maneno mazito sana na ya kutia uchungu kweli kutokana na jinsi ambavyo tuna viongozi wengi na wasomi vilevile ambao hawana habari kabisa na wapi nchi inatoka na matokeo yake nchi inajikuta inazidi kudidimia.
Nikinukuu yaliyotamkwa na Mwalimu: "Lakini ni vizuri nikasema pia kwamba kwa maoni yangu hatuwezi tukaamua kuacha mfumo wa Demokrasia ya Chama Kimoja, tukajaribu mfumo wa Demokrasia ya Vyama Vingi, kwa matumaini ya kwamba tukikuta kuwa mfumo huo hautufai, basi tutarudia tena Demokrasia ya Chama Kimoja.
“Tutajidanganya, haiwezekani na ni vigumu kabisa. Ukimwacha mkeo na ukaoa mwingine, na ukagundua kuwa huyu wa pili ni balaa, ni vigumu kumrudia mkeo wa kwanza. Demokrasia ya Vyama Vingi ikitushinda, mfumo ambao ni rahisi kufuatia utakuwa ni udikteta wa mtu mmoja au utawala wa kijeshi. Hiyo ni sababu nyingine muhimu ya kutofanya uamuzi kwa pupa. Inafaa tukajipa muda wa kutosha kuelewa athari zinazoweza kutokea kutokana na uamuzi wowote tutakaoufanya. Si vema kuruka bila kuwa na hakika utaangukia wapi!" .

Ni imani yangu kwamba mfumo wa Demokrasia ya Vyama Vingi nchini Tanzania sasa hivi unakabiliwa na mtihani mgumu ambao si wa kufanyiwa mzaha hata kidogo. Kwa kutambua uzito wa suala hili, nitarejea safari yetu ya nyuma ya vyama vingi. Imani yangu ni kwamba kwa ujumla miaka ishirini na mitatu ya mfumo wa Demokrasia ya Vyama Vingi imekuwa hasara kuliko faida kwa maendeleo ya nchi.
Na hapo kwa namna fulani namlaumu Hayati Mwalimu kwa kutuingiza kiaina ndani ya huo mfumo pamoja na angalizo zake kibao juu ya matatizo ya Demokrasia ya Vyama Vingi.
Hivi mpaka Mwalimu alikuja na mfumo wa chama kimoja kiitwacho 'Demokrasia ya Chama Kimoja', kuna sababu za msingi tu. Mwalimu kwa maneno mengine alipaswa kupigania kwa nguvu zake zote ile dhana ya 'Demokrasia ya Chama Kimoja' hadi kweli ionekane imeshindikana. Na tunafahamu alikuwa na ushawishi mkubwa MNO.
Matokeo ya kuingia kwa pupa ndio sababu haikuchukua muda mrefu kumsikia Mwalimu akianza kusema ohh 'upinzani wa kweli utatoka ndani ya CCM'. Lugha hiyo ilisababisha mpaka yeye mwenyewe kukasirika bure alipoulizwa mwaka 1995 kama Augustine Mrema ndiyo huyo mpinzani aliyebashiri.
Ni vyema nirudie kidogo maneno niliyoandika kipindi cha nyuma kidogo ili kupanua mawazo ya msomaji wa makala hii. Niliandika yafuatayo: "Mfano mzuri wa athari ya kuingia kwa pupa kwenye Demokrasia ya Vyama Vingi ni kurejea mwezi Oktoba mwaka 1990, kabla ya Tume ya Nyalali kuanzishwa. Iliteuliwa kamati ya CCM ya Kushauri Juu ya Mageuzi, chini ya Waziri wa zamani wa Sheria, Bakari Mwapachu, na ambayo kama ilivyo kawaida tu Tanzania, taarifa hiyo haijulikani na viongozi wengi wa nchi.
Katika sehemu ya mwisho ya taarifa hiyo, kamati ilitahadharisha kuhusu umuhimu wa mageuzi makubwa ya kiuchumi. Nikinukuu sehemu ya kwanza: "Kuwepo kwa uchumi mzuri pia kunafanya hata vyama vitakavyoanzishwa kuwa vya kweli na siyo miradi ya viongozi na wanachama wake kupata njia ya kuendeleza maisha".
Sehemu ya pili ya taarifa kuhusu umuhimu wa mageuzi makubwa ya kiuchumi ilisema: "Vyama vitakavyoanzishwa vitakuwa na nafasi nzuri ya kuwa na wanachama watakaoendesha chama chao wenyewe bila kutegemea wafadhili wachache au misaada ya chinichini na ya vificho kutoka nje".
Ni jambo lililo wazi kwamba hili la kwanza na la pili ni tatizo kubwa sana. Nikianza na la kwanza, ni nadra sana kusikia hata kuhusu mikutano mikuu ya wanachama wa vyama vingi tu ili kutimiza sharti la msingi la kuchaguana. Inawezekana hata ada za kila mwaka za chama hazilipwi. Na inaelekea kwamba viongozi wakuu wa nchi ndiyo wanaopendelea huu utitiri wa vyama ili kujigamba kwa wafadhili kwamba demokrasia imeshamiri Tanzania.
Ni imani yangu ya dhati kwamba ingekuwa jambo la kushangaza kutokana na kuingia kwenye mfumo mpya "kichwa kichwa" kama kweli tungepata vyama kwa maana halisi ya vyama kwa muda mrefu. Ni lazima kuwepo na msingi imara katika kitu chochote kikubwa kama vile kujenga nyumba!
Nimepata kusoma mara kadhaa makala na hotuba zake za miaka ya nyuma, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akiwatupia mpira Watanzania kwamba ni kama vile watu wa kutaka 'mabadiliko' bila kujitazama kwanza na kuviunga vyama vilivyopo kwa hali na mali. Kwa lugha nyingine, ni "armchair critics".
Nadiriki kusema Watanzania wengi si watu wa kuunga mkono kitu mara nyingi kwa kubahatisha. Mfano wa wazi kwa hili ni mwaka 1995 wakati Augustine Mrema alipogombea urais na kupata kura nyingi. Watanzania wengi walimwona Mrema kama kiongozi wa watu. Ni bahati mbaya tu kwamba ilikuwa si rahisi kwa wengi kupata picha sahihi kilichokuwa kinamsukuma Mrema.
Kulionyesha hili, katika kitabu cha maisha cha Mwenyekiti mwanzilishi wa Chadema, Mzee Edwin Mtei, anaeleza kwamba Chadema kilituma ujumbe kuzungumza na Mrema kuhusu uwezekano wa kujiunga na chama hicho. Masharti waliyopewa na Mrema ni kwamba Chadema kimteue kuwa mgombea urais na vile vile Mwenyekiti wa Taifa wa chama.
Chadema kilikuwa tayari kumteua Mrema kuwa mgombea urais ila si Mwenyekiti kutokana na ulazima wa kikatiba wa kuitisha Mkutano Mkuu. Matokeo yake, Mrema alijiunga na NCCR Mageuzi na kupitishwa kuwa Mwenyekiti na Mgombea Urais.
Sasa kweli yeye Mrema kutaka kukabidhiwa nafasi zote mbili haikuwa uchu wa madaraka? Kwa upande wa Chadema, pamoja na kutofanikiwa kumpata Mrema kuwa mwanachama halafu mgombea, kilimuunga mkono kwenye harakati za urais kwa uelewa kwamba vyama hivyo vingeunda serikali ya mseto endapo wangeshinda.
Kwa maneno yake Mzee Mtei, mtu mmoja mkubwa ndani ya CCM alimwambia miaka michache baadaye kwamba tangu siku yeye Mtei alipotangaza kwamba Chadema kingemuunga mkono Mrema, alipoteza imani kwake. Na Mtei anasema akitazama nyuma, anakiri hilo lilikuwa kosa moja kubwa katika maisha.
Anaendelea kusema kwamba yalikuwa ni maoni ya wengi ndani ya chama chake ambayo alikuwa anajaribu kuheshimu lakini anasema alipaswa kuwa na nguvu kuupinga. Hiki kitendo kilinipa picha jinsi ambavyo Chadema kilikuwa ni chama cha kubahatisha bahatisha.
Hili suala la kubahatishabahatisha limejitokeza tena majuzi kwa kitendo cha Chadema pamoja na jumuiko la Umoja wa Katiba ya Wananchi kumkaribisha Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, kuwa mgombea Urais. Tofauti iliyopo sasa ni kwamba inaelekea kutishia mpaka usalama wa taifa letu. Sina budi nitofautishe kidogo suala la Mrema na Lowassa.
Mrema hakusubiri mpaka jina lake likatwe halafu ahame. Aliamua kwa sababu alizozijua mapema kuondoka kwa kishindo baada ya kuilipua serikali bungeni na kujikuta anatimuliwa kama Waziri. Yeye Lowassa amepambana mpaka mwisho na kutishia kuwa hakuna mwenye ubavu wa kumkata.
Na kufuatia kukatwa kwake, katika kilichoonekana kwangu kama kumsafishia njia Lowassa kuingia Chadema, Mwenyekiti wa chama hicho alitamka maneno ya kuchefua mno tarehe 21 Julai 2015: "Chadema haimzuii mtu kujiunga kwani Chadema kuna kila aina ya wanachama - kuna vibaka, majambazi, wezi, wachawi, wala rushwa, mafisadi na wengineo, hiki ni chama cha siasa, kina jumuisha watu wengi, siwezi kusimama na kusema wanachama wa Chadema wote ni wasafi, itakuwa si kweli, hivyo anayetaka kujiunga na chama chetu anakaribishwa ila lazima kuzingatia kanuni na maadili ya chama".
Sina budi niseme nimejikuta natafakari zaidi na zaidi hii ndoto ya Lowassa kuwa Rais kwa gharama yote. Kilicho dhahiri ni kwamba Lowassa kwa maneno ya mitaani aliamua 'piga ua' lazima picha yake iwe kwenye karatasi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi tarehe 25 Oktoba na sio tu kusubiria vikao vya juu vya CCM.
Kwa hili naweza kusema ni haki yake kabisa. Ila ninajikuta na hofu kwamba kile kinachoitwa kwa kiingereza 'political astuteness' au tuseme utashi wa kisiasa kwake kama hamna kabisa.
Maana yangu ni kwamba kwenye siasa, kuna suala la wakati au 'timing'. Katika kulifafanua hili, ni vyema kunukuu sehemu ndogo ya makala niliyoiandika huko nyuma: "Jambo la nne lililodhihirisha hitilafu nyingine ya msingi ya Lowassa ni kwenye ndoa yake ya kisiasa na Kikwete mwaka 1995. Katika ufuatiliaji wote wa siasa duniani, sijapata kuona uhusiano kama huu wa Lowassa na Kikwete.
Nikimnukuu Lowassa: "Tunasindikizana. Tuko pamoja. Sisi ni vijana, ni wadogo, tunafikiri ni vizuri sisi wawili tushirikiane, two in one, tushikamane tu na baadaye tutakavyoona mbele atakayefanikiwa amefanikiwa mwenzake atamsaidia, atakayekuwa ameshinda na mwenzake ataendelea kuangalia".
Niliendelea kuandika: "Kwenye siasa hakuna kitu kama kusindikizana, pengine kwenye vyuo vikuu. Ikibidi wote wanagombea kwa nguvu zao zote na katika hatua za mwisho basi wanaweza kukubaliana kuhusu nafasi za uongozi. Vilevile hata kama ni muungano wa vyama au serikali ya mseto, ni lazima kuwa na kiongozi.
Sasa taarifa zinaonyesha kwamba Lowassa alikuwa juu kabisa ya Kikwete kiasi cha jina lake kuwa miongoni mwa majina manne yaliopendekezwa na UVCCM kugombea Urais. Sasa tena alijishusha kwa mtu ambaye siku nyingi sana alikuwa na sifa ya kutokuaminika sawasawa. Ni kama alivuna alichopanda kwa kuingia kwenye ndoa isiyo takatifu".
Nadiriki kusema kwamba ndoa hiyo ya Kikwete na Lowassa imesababisha mateso ya aina yake kwa Watanzania. Mpaka leo hatuelewi vizuri suala la Richmond kama mfano. Ilikuwa jambo la dhihaka kumsikia Kikwete akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano mwezi uliopita kabla tu ya kuanza kwa vikao vya kuwachuja wagombea wa CCM na kumwagia sifa Lowassa.

Kwa kifupi kilichokuwa kinatakiwa na Lowassa kwa upande wa 'political timing' ni kujitoa CCM mwaka 2010 na kuingia ulingo na mbaya wake Kikwete ili amtambue vilivyo. Nadhani nafsi yake Lowassa ingekuwa nyeupe hii leo na pengine Kikwete angekiona cha moto uchaguzi huo kiasi cha kufanya kazi ya Lowassa mwaka 2015 kuwa wa 'kupungia tu mkono' wananchi kama alivyotaka kutuaminisha ingekuwa asingeondolewa kwenye Uwaziri Mkuu.
Na kama isingewezekana kabisa yeye kujitoa CCM mwaka 2010, basi angefanya juu chini miaka mingi kupitia kwa wale wabunge waliokuwa wanamuunga mkono kuhakikisha Katiba inaruhusu mgombea binafsi mapema ili ikibidi atumie hiyo njia.
Haishangazi hata mchambuzi mmoja kutoka nchi jirani alidhania Lowassa angetumia hiyo njia huku hajui Katiba hairuhusu hilo. Kwa hili suala la mgombea binafsi naweza kusema wanasiasa wengi wa Tanzania ni wa 'kawaida sana' kama alivyosema Mwalimu na ndio maana hawawezi kufikiria mbele sana.
Naamini hata hii leo Dk. Wilbrod Slaa angekuwa salama kabisa kisiasa kama Katiba ingeruhusu hilo. Lakini naye na wenzake hawakuweka msukumo wa kutosha kutokana na maslahi ya vyama vyao.
Vilevile Lowassa angekuwa ni mtu makini kwenye siasa, angepingana na adhabu ambayo yeye na watu wengine watano walipewa kwa kuanza kampeni kinyume cha utaratibu. Isitoshe waliongezewa kipindi cha adhabu, jambo ambalo lingemfanya hapo aone imetosha na kuhamia kwingine.
Halafu kwa mambo mengi Lowassa alijitengenezea mazingira magumu bila sababu yoyote. Mfano tu ni mchakato wa kutafuta wadhamini ndani ya CCM. Ilikuwa vituko tupu! Hivi kweli mtu unaambiwa unatakiwa tu kuleta wadhamini takribani mia nne tu na badala yake wewe unakaribia milioni moja, maana yake nini kama si kuwatisha viongozi wa CCM? Alijidai kusema angepeleka majina yao nyumbani kwake kama kumbukumbu!

Kwa hili tu, pengine alikuwa anawapa viongozi wa CCM sababu nzito kufutilia mbali jina lake kwa sababu zoezi la kuhakiki majina ya wadhamini wote mkoani si kazi ya kupuuzia hata kidogo. Mdhamini ni mtu muhimu sana. Hasa kwa idadi ya kihistoria ya wagombea 38.
Na kufuatia kujiunga tu na Chadema, aliendelea na vituko vya kusaka wadhamini. Eti milioni moja na nusu ndani ya siku mbili !
Ukiondoa hayo machache niliyoandika juu ya safari ya kisiasa ya Lowassa, kwenye suala nyeti kabisa la Katiba Mpya, mtazamo wake ni wa viongozi wengi ndani ya CCM. Japokuwa alikuwa kama bubu ndani ya Bunge Maalum la Katiba, ni aibu ya karne kuungana kwake na Ukawa. Jamani ili tupige hatua tunahitaji siasa safi inayofuata kanuni!
Nikimgeukia mgombea urais wa CCM, John Joseph Pombe Magufuli, sina mengi ya kusema ila ni shida tupu! Kabla ya kuchukua fomu ya urais wale watu wengi hawakumzungumzia kama mtu anayefaa kuongoza nchi. Na haiwezekani kwa mtu kuwa sehemu ya Baraza la Mawaziri ya awamu mbili ambazo zimeonekana kushindwa kabisa kupambana na rushwa na ujipambanue kuwa msafi.
Haipo popote duniani. Halafu niongeze udhaifu wa Magufuli ni kama ambavyo mtu mmoja mwenye jina Padri Mapunda, alivyosimulia kwenye gazeti alipokutana naye na ambayo hata mimi nimeshuhudia nyumbani kwake. Mapunda anasema yafuatayo: "Ni kweli kuwa huyu ni kati ya mawaziri wachapakazi na wenye kuonyesha uwajibikaji katika serikali iliyopo sasa. Hili halina ubishi, hata hivyo si sifa pekee za kumwezesha kukubaliwa na Watanzania ili awe Rais kupitia CCM ambayo nadiriki kusema imechokwa na Watanzania.
“Nikiwa mkweli naweza kusema kwamba simjui Magufuli isipokuwa siku moja nilipokutana naye. Nilikuwa na shida ofisini kwake nilitaka kumwona na baada ya kusubiri alitoka nje ya ofisi na watu zaidi ya wanne. Nilipofanya jitihada za kujitambulisha na kujaribu kumweleza kilichonipeleka, hakunisikiliza na hata hakupenda kujua ni nani anayetaka kumweleza shida hiyo. Tangu siku niliendelea kujiuliza maswali mengi kuwa huyu ni kiongozi wa namna gani na akiwa Rais atawasikiliza watu wangapi?".
Hili ni jambo la bahati mbaya sana kwa nchi kujikuta na kiongozi ambaye hana uvumilivu na pengine haishangazi kwamba hata kwenye jimbo lake wananchi walielekea kumpumzisha mwaka huu.
Kuhitimisha, Tanzania inakabiliwa na uchaguzi mkuu mgumu kuliko wakati wowote baada ya miaka 50 ya TANU/CCM. Kiu ya mabadiliko ni kubwa mno kutokana na ombwe la muda mrefu sana. Kama tunavyoambiwa "siasa huchukia ombwe", isipokuwa sasa wananchi watajikuta na uchaguzi uliojaa joto kuliko mwanga.
Mfumo wetu wa demokrasia uko kwenye mtihani mzito. Kutokana na historia ya Lowassa ndani ya CCM, si rahisi kuachiwa madaraka kama kweli ataelekea kushinda na hapo sasa sijui nini kitafuata. Najikuta nakumbuka kilichotokea nchini Algeria mwaka 1992 na chama cha FIS.
Katika hali ya sasa hivi ya Demokrasia ya Vyama Vingi kuwa katika hali ya umahututi, ni rai yangu kwa vyama vya kiraia na vyombo vya habari (civil society) kujipanga upya kwa mapambano ya kudai Katiba Mpya nje ya vyama vya siasa.
Imeshaonekana vyama vya siasa ni tatizo kubwa katika nchi mbalimbali za Afrika na ndiyo sababu Rais Barack Obama katika ziara yake nchini Kenya hivi karibuni, alielekeza nguvu kwa vyama vya kiraia na vyombo vya habari kuwa mstari wa mbele kwenye maendeleo ya nchi.


No comments :

Post a Comment