Serikali yatambua juhudi zinazofanywa na sekta binafsi ndio maana ikatoa mwongozo huo.
Akizungumza katika warsha ya kupitia na kutoa maoni kuhusu Rasimu ya Sera ya Maendeleo ya Sekta Binafsi nchini jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TPSF, Dk. Reginald Mengi, alisema kunapaswa kuwapo na viongozi ambao watasimama kidete na kusema rushwa haikubaliki.
Alisema rushwa imeendelea kuwapo kutokana na viongozi kutokuonyesha vitendo kwa matamko wanayoyatoa, hivyo kuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya uchumi katika sekta hiyo nchini.
“Tunataka tufike mahali, Mtanzania aogope kupokea na kutoa rushwa.
Tunataka kiongozi atakayesema rushwa basi na kila Mtanzania ajue hivyo na siyo kuonekana tunazungumza maneno yale yale bila vitendo,” alisisitiza Dk. Mengi. Kuhusu sera hiyo, alisema kipaumbele cha msingi ni elimu na ujuzi kwani hakuna taifa ambalo limepiga hatua ya maendeleo huku watu wake wakiwa hawana vitu hivyo.
Dk. Mengi alisema haiwezekani kuwa na sera yoyote kama vile ya elimu ambayo ni vipande vipande kutokana na kila Waziri kuwa nayo ya kwake.
Dk. Mengi alisema haiwezekani kuwa na sera yoyote kama vile ya elimu ambayo ni vipande vipande kutokana na kila Waziri kuwa nayo ya kwake.
Alitoa wito kuwapo kwa viongozi watakaotengeneza sera kama hiyo ambayo itaweza kutumiwa kwa zaidi ya miaka 20 au 25 mbele.
Mshauri wa sekta binafsi na huduma za maendeleo ya biashara wa PPP Solutions Ltd, Bede Lyimo, alisema lengo la sera hiyo ni kubainisha masuala muhimu kama vile elimu ili iende sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025.
Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo Sekta Binafsi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ezamo Maponde, alisema serikali inatambua juhudi zinazofanywa na sekta binafsi ndiyo maana ikatoa mwongozo huo unaogusa pande zote na kumwezesha kila mwananchi kuinua pato lake la halali.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Sembeye, alisema warsha hiyo ilikuwa na lengo la kukutana na wadau wa sekta binafsi, serikali na wabia wa maendeleo ili kuangalia rasimu ya sera hiyo kwani kwa muda mrefu hakukuwa na utaratibu wa kuandaa sera ya maendeleo ya sekta binafsi nchini.
“Leo serikali imekuja na rasimu kuwa hii ndiyo sera ya maendeleo ya sekta binafsi , ikatuletea sisi TPSF. Tukatoa mawazo mara ya kwanza na mara ya pili.
Tupo na wadau tuone namna ya kuirekebisha na kuiwasilisha kwa serikali ili iweze kuwa ndiyo sera kamili ya maendeleo ya sekta binafsi,” alisema Sembeye.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment