Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, August 21, 2015

TUNATAKA “mabadiliko” au MABADILIKO?


UPEPO wa mabadiliko nchini unaendelea kuvuma. Ni mwendelezo wa upepo ule ule ulioanza mwanzoni mwa miaka ya 1990, baada ya kurudi kwa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa. 

Ni upepo ule ule ambao ulivuma na kutuletea kina Augustino Mrema, James Mapalala, Seif Sharrif Hamad, Masumbuko Lamwai na wanasiasa wengine mahiri waliovuma katika upinzani wakati ule ule. 

Ni mwendelezo ule ule uliowaibua wanasiasa wengine na kuwainua katika jamii yetu wakipiga mbiu ya kutaka mabadiliko. Kuanzia kina Kabouru hadi Slaa, Mbowe hadi Zitto, Mnyika hadi Lissu. 

Upepo huu umeendelea kuvuma na sasa hivi umeleta wanasiasa wengine ambao nao wanatudokeza kuwa ipo haja ya mabadiliko. Kuanzia Lowassa hadi Mgeja, Said Nkumba hadi Lawrence Masha. Upepo huu unatuletea wote –wazuri na wabaya, wenye kutupa matumaini na wenye kutukata maini; upepo huu unavuma na sauti yake inasikika “mabadiliko, mabadiliko!” Tangu kuanza kwa muhula wa uchaguzi miezi michache iliyopita kauli za “mabadiliko” zimezidi kuvuma.
Kwa watu waliokuwa ndani ya chama tawala hadi ya wale walio nje ya chama tawala. Na hili la kutaka mabadiliko wengine wanalihusisha hata na kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kuwa CCM isipowapa Watanzania mabadiliko basi Watanzania watayatafuta mabadiliko hayo nje ya CCM. Na wapo wanaoamini kuwa labda safari hii neno hili ni kweli zaidi kuliko wakati mwingine wowote tangu upepo huu wa mabadiliko uanze kuvuma. 

Leo hii Watanzania wanashuhudia jinsi maelfu ya wananchi wakijitokeza kumpokea na kumshangilia aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Edward Lowassa ambaye wiki chache tu nyuma alikuwa anang’ara ndani ya CCM akionekana kuwathubutisha CCM walikate jina lake waone kama hatahama chama na kujaribu ndoto yake ya kutaka kuwa Rais hatoitafutia mahali pengine nje ya CCM. Licha ya kuwa kwa muda mrefu upinzani Tanzania ulimtaja na kumhusisha Lowassa na kashfa mbalimbali za ufisadi leo hii tuhuma hizi zimefutika – labda sababu ya upepo huo huo – na sasa Lowassa anabeba ujumbe wa mabadiliko nje ya CCM. 

Watanzania wenye kiu ya mabadiliko wanajikuta wanalazimika kudandia treni hili la Lowassa ambalo hatujui hasa linataka kwenda wapi lakini linaimba wimbo wa mabadiliko na watu kwa imani na kwa maelfu yao wanalidandia wakiamini kuwa linaelekea kuwatimizia ndoto na matarajio yao – mabadiliko. 

Hili linapaswa kutufanya tuulize kama nilivyodokeza kwenye makala za huko nyuma mabadiliko haya bila kutaka kuyajua vizuri tunaweza kujikuta tunashabikia kisichokuwepo na tukashindwa kutazamana huko mbeleni kwa sababu tulichobadilisha sicho hasa tulichotaka kibadilike. 

Nimewahi kuandika huko nyuma kuwa mabadiliko ambayo Tanzania inahitaji siyo mabadiliko ya sura bali ya sera. Ni kweli tofauti ya maneno hayo mawili kiuandishi ni herufi moja tu lakini kimaana maneno haya yana mbili tofauti kubwa sana. Ni rahisi zaidi kubadilisha sura kuliko kubadilisha sera. 

Hofu yangu kubwa leo hii ni kuwa tusipoangalia katika kushabikia mwamko huu ambao wengine wanautaja kuwa ni gharika, mafuriko au kimbunga tunaweza kabisa tusiangalie maana hasa ya maneno haya kwani ndani yake yameficha kitu kikubwa hasi; mafuriko, gharika na vimbunga vyote haviji na mazuri! Kimbunga cha Katrina kule Marekani na mafuriko ya mapema mwaka huu jijini Dar na sehemu nyingine duniani yanatufundisha tu kuwa mafuriko hayashangiliwi. 

Hata gharika siyo kitu cha kushabikia kwa sababu gharika ile moja ya kibiblia tunajua matokeo yake; ni kweli ilileta maisha mapya kabisa lakini ilisababisha kuangamia kwa dunia ile ya kwanza kwa wale wenye imani. Hivyo, tunapotumia maneno kama gharika, mafuriko, kimbunga ni lazima tujue kuwa ndani yake tunaweza kujitabiria mabaya zaidi kuliko tunavyoweza kufikiria. 

Ni kweli, mafuriko, kimbunga au ngarika vinaweza kuondoa vitu vilivyokaa muda mrefu kwa haraka zaidi kuliko njia nyingine lakini kinachotokea baada ya hapo ni vigumu sana kubashiri. Lakini kama wanafunzi wazuri wa historia ni lazima tujikumbushe pia kuwa maelfu ya watu kujitokeza kusema wanataka mabadiliko haina maana kweli mabadiliko hayo yakitokea yatawanufaisha wao au yatafanya nchi zao kuwa salama zaidi kuliko hapo nyuma. 

Tunakumbuka vizuri tu mwamko wa mabadiliko ya nchi za Kiarabu (Arab Spring) ulivyoanza na kuonekana kuleta matumaini mapya kabisa kwa wananchi wa nchi hizi. Kuanzia Tunisia hadi Syria, Misri hadi Oman kulikuwa na matumaini kuwa kubadilisha sura za watawala kutasababisha mabadiliko ya sera. 

Tumeona yaliyotokea Libya na Iraq na hata kwenye kama Ukraine na Georgia ambako kote huko mamilioni ya watu walijitokeza katika maandamano makubwa kudai mabadiliko na hata kuweza kuangusha serikali zilizokuwa madarakani. Hapa ndipo swali langu linabidi kusimama kama shahidi wa historia; ni mabadiliko gani tunayoyataka kweli; ni kubadilisha sura za watawala au sera za utawala? Je tunaweza kubadilisha sera bila kubadilisha sura tukawa na mafanikio? Je tunaweza kubadilisha sura na tukajikuta tumebadilisha sera vile vile? 

Kama hatujui wanaotuongoza kuimba mabadiliko mabadiliko wanasimamia sera gani hasa je tuendelee kushabikia tu kwa sababu wanasema wanataka kubadilisha? Tukiwauliza wanataka kubadilisha nini wanasema “watawala wabadilike kwanza mengine baadaye”. Je, hili linatosha kushawishi watu wenye akili kudandia treni la safari ya mabadiliko? 

Ni kweli kabisa chini ya utawala wa watawala wa sasa walioshindwa taifa letu limepigika; lakini tuna uhakika gani kuwa watawala wajao hawatatupiga zaidi? Au tunaamini tu kwa sababu wanasema hivyo hata kama hatujui hasa wanataka kufanya nini kutuondoshea mzigo tuliobebeshwa na utawala wa CCM? Lakini itakuwaje kama wale wanaotaka kutuongoza kwenye mabadiliko leo hii ndio wale wale waliotutwisha mzigo ambao wanasema wanataka wautue wakati tunajua kabisa kuwa muda wote ambao walikuwa kule kwingine hawakuwahi kunyosha hata kidole kutua mzigo huu? Hapa ndipo mababu walisema “akili mukichwa”. 

Kama nilivyosema makala yangu ya mwisho kuwa tunahitaji kudai zaidi kutoka kwa wale wanaotaka kuwaondoa watawala wa sasa. Tunaweza kweli kabisa tukajisifia tumeruka mkojo na kujikuta tumekanyaga kinyesi ambacho tulikiona lakini tulidhania dhahabu. Upande mwingine hata hivyo ni kuwa vipi kama kweli mabadiliko makubwa hayatatokea sasa isipokuwa hii ni hatua tu muhimu kuipitia kama taifa? 

Kwamba, hata kimbunga na mafuriko na gharika vinaweza kuharibu vitu vingine lakini vikatoa nafasi ya kuanza upya hata kama kuanza huko labda hakutaletwa na hawa wa sasa? Hapa napo inahitaji imani; tusuke au tunyoe vyovyote vile itakavyokuwa upepo huu wa mabadiliko inaonekana hauondoki sasa hivi. Kwani hata watawala wa sasa walioshindwa nao wameshaanza kuimba wimbo wa mabadiliko; wao wanasema sura zile zile sera tofauti! Hapa napo akili mukichwa.

No comments :

Post a Comment