UMOJA wa mashirikisho ya sanaa Tanzania umepinga uwepo wa Umoja wa Wasanii ulioandaa sherehe ya kumuaga Rais Jakaya Kikwete katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya umoja huo, Kimella Billa, alitangaza kutotambua umoja huo na kudai kwamba, kilichofanyika ni kinyume cha taratibu.
“Umoja huo haujasajiliwa, pia uwezo wa wasanii tunaufahamu, ni vigumu kufanya shughuli kubwa ile ambayo haikuwa na mdhamini, tunaamini kulikuwa na nguvu ya mtu mwingine anayewatumia wasanii hao, sisi na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) tulishaanza mchakato wa sherehe maalumu ya kumuaga Rais na maandalizi yanaendelea ili mapema Oktoba tufanye kwa ushirikiano na wasanii wote nchini.’’
Kwa upande wa Nickson Simon ‘Niki wa Pili’ aliyekuwa msemaji wa wasanii hao, alikiri kwamba umoja huo haupo kihalali kwa kuwa haujasajiliwa, lakini sherehe hiyo ilifanyika kwa lengo la kufikisha mrejesho kwa Rais uliotokana na maadhimisho ya sherehe yao ya awali iliyofanya mkoani Dodoma.
“Tulimuahidi Rais kumpa mrejesho wa tuliyokubaliana Dodoma na ndiyo maana tukaandaa sherehe iliyokuwa wazi na hao viongozi wanaopinga leo tuliwapa taarifa, wengine walitoa udhuru. Na katika hotuba yangu nilieleza kwa ujumla kuhusu maombi yetu kwa Serikali, hivyo hakukuwa na ubaguzi wowote,” alisema.
/Mtanzania
No comments :
Post a Comment