dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, September 9, 2015

AFUNGUKA!

  Gwajima asema tatizo la Dk. Slaa ni mkewe siyo Lowassa.

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.
Sakata la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, kumuita mshenga Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, limechukua sura mpya baada ya askofu huyo kuibuka na kile alichodai kuwa ni ushahidi wa maandishi na sauti kuthibitisha kuwa kinachomsumbua Slaa ni mkewe Josephine Mushumbuzi na wala siyo kitu kingine.
 
Wiki iliyopita, Slaa aliwaambia waandishi wa habari kuwa alilazimika kujiweka kando Chadema na pia kujing'atua katika shughuli za siasa baada ya kutoridhishwa na mchakato uliomuwezesha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuhamia chama hicho akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kisha kuteuliwa kuwa mgombea urais, akiwakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (Cuf).
 
Katika baadhi ya madai yake wakati akizungumza na waandishi wa habari, Dk. Slaa alidai vilevile kuwa Gwajima ndiye 'mshenga' aliyemuwezesha Lowassa kutua Chadema na mwishowe kuteuliwa kuwa mgombea urais.   
 
Hata hivyo, akizungumza jana katika mkutano uliojumusha waandishi wa habari, waumini wa kanisa lake na watu wa makundi mengine, Gwajima alikiri kuwa ni kweli yeye anastahili kuitwa 'mshenga' wa Lowassa kwani ndiye aliyewakutanisha viongozi wa chama hicho hadi kuingia kwenye kikao cha kamati kuu ya Chadema.Gwajima ambaye katika maelezo yake alithibitisha urafiki wake wa karibu na Dk. Slaa na Lowassa, na alisema amejitokeza kuweka wazi baada ya kusikia kauli ya kiongozi huyo kuwa maaskofu 30 wa makanisa mbalimbali wamepewa rushwa ili wamsaidie Lowassa katika kampeni zake.
 
Alisema yeye (Gwajima) aliombwa na Dk. Slaa huyo kumpa walinzi ambao ni watu salama wa kumsaidia kwa kuwa hakuamini mtu yeyote kutokana na kuwapo kwa tishio la kuuwawa na kwamba, alikuwa na woga wa kulindwa na polisi na watu wengine kwa hofu ya kusalitiwa na ndiyo maana aliomba walinzi kutoka kanisani.
 
“Nilimpa walinzi ambao ni Edwin Mwandimo, Sixtus Nyimbo na Cornel Mwakatabu...ni watu ambao walikuwa wanaaminika kwangu. Kwa miaka minne hadi mitano analindwa na watu niliompa mimi, mpishi wa nyumbani kwake alikuwa mama mtu mzima aitwaye Macelina Mushi (50)... alifanya usafi hadi chumbani kwake. Naye alitoka kwangu, nilimpa kama rafiki wa ukombozi,” alisema na kuongeza.
 
“Walikuwepo nyumbani kwake usiku, mchana na jioni… nani mjanja kati yangu mimi na yeye. Mimi niliyekuwa najua umeingia saa ngapi, umetoka saa ngapi, najua unachopikiwa na unakolala, nani ana uwezo wa kumjua mwenzake. Ninamjua toka jikoni, chumbani, sebuleni hadi kwenye gari,” alisema Gwajima.
 
SHINIKIZO LA MKEWE
Gwajima alimtuhumu Dk. Slaa kuwa hasemi kweli kwa kuwa hakuhama Chadema kwa sababu ya ujio wa Lowassa kama alivyowaambia waandishi wa habari bali shinikizo la mkewe.
 
Gwajima ambaye alitamba kuwa ndiye 'Baba wa Kiroho' wa Dk. Slaa na mchumba wake, alisema kiongozi huyo (Dk. Slaa) ndiye aliyemfuata nyumbani kwake na kumuomba atumie ushawishi wake kumvuta Lowassa Chadema, akiamini kwamba waziri mkuu huyo wa zamani ana nguvu kubwa ndani ya chama chake na jamii; na kwamba kumpata kwake kungeiimarisha Chadema na mwishowe kuipa ushindi katika uchaguzi.
 
Alisema kisa cha Slaa kumtaka yeye amfuate Lowassa na kumshawishi ajiunge Chadema ni ukweli kwamba yeye (Gwajima) na Lowassa wana urafiki wa siku nyingi.
 
“Kwa kuwa namfahamu Dk. Slaa kuanzia jikoni hadi nje, nilifanya kila linalowezekana ili Lowassa atue Chadema, kwenye aliloniita mshenga...alipatia kwa kuwa mshenga anajua vitu vyote vya mposaji na vyote nitaviongea. 
 
Alichokosea ni kutosema kuwa ujio wa Lowassa Chadema ilikuwa ni mpango wa Mungu. Bibilia inasema heri wapatanishi mana hao watauona ufalme wa Mungu, kwa desturi wanasiasa hawapatani... lakini mimi nilisimama kama mpatanishi,” alisema.
 
Gwajima alisema baada ya hapo, Dk. Slaa alimkutanisha na Mwenyekiti wa Chadema,  wakafanya mazungumzo ya kutosha na kukubaliana hadi Julai 26, mwaka huu walipokutana hoteli ya Bahari Beach katika kikao cha Kamati Kuu na hapo Lowassa alipokelewa Chadema baada ya majadiliano marefu.
 
“Nilikuwapo ili nione Lowassa ameingia Chadema kwa usahihi na kupokelewa. Niliwaomba watu wa Kamati Kuu niingie kwenye kikao ili nione Lowassa amefika salama. Alipokelewa na alihutubia,” alisema.
 
“Siku zote wagombea urais, vyeo... huanzia kwa waganga wa jadi, wanachanjwa chale, wanazindikwa...  ni jambo zuri kama wameanzia kwenye nyumba ya ibada,” alisema Gwajima.
 
Alisema Lowassa alipokelewa nje ya ukumbi na Dk. Slaa, Mwenyekiti wa Chadema (Freeman Mbowe), Prof. Mwesiga Baregu na viongozi wengine; na kwamba kikao kilimalizika majira ya saa 6:00 usiku na baada ya hapo wote walitawanyika.
 
“Ilipofikla saa 7:19, nilipokea ujumbe kutoka kwa mmoja wa walinzi wangu kuwa baada ya Dk. Slaa kufika nyumbani lilitokea jambo la ajabu.
 
MLINZI ASIMULIA
Alipofikia hapo, Gwajima alimuita mmoja wa walinzi ili kuelezea kilichotokea baada ya Dk. Slaa kufika nyumbani kwake usiku, akitokea kwenye kikao cha kamati kuu kilichompokea Lowassa.
 
Aklianza kusimulia, Cornel Mwakatabu alisema majira ya saa 6:20 alipigiwa simu na mlinzi wa Dk. Slaa kuwa anakuja akiendesha mwenyewe kwakuwa amemuacha eneo la Boko ili asipate shida ya usafiri baada ya kumfikisha (Slaa) nyumbani na kwamba alitaka kujua kama amefika salama.
 
“Alifika, nilimfungulia geti akaingia. Nikampa pole na baadaye nilibeba briefcase yake hadi ndani, nilimuamsha mama (Josephine Mushumbuzi) kupitia dirishani. Tulikuwa tunaishi kama familia. Tukiwa tunasubiri mlangoni, alifungua mlango wa kwanza kabla hajafungua mlango wa pili wa grill... alisema Dokta rudi ulikotoka,” mlinzi huyo alisema.
 
“Alipofungua geti, alitoka na sanduku la nguo na kulirusha... Dk. Slaa alishikilia mlango, lakini alimtaka aachie (mlango) na kurudi alikotoka huku akimuonyesha begi lake...kitendo kile kiliniuma sana,” alisema.
 
Alisema walikaa kwa sekunde kadhaa na kumuuliza nini cha kufanya, ndipo Dk. Slaa aliposema atakwenda kulala kwenye gari na hapo ndipo yeye (mlinzi) alipomjulisha Gwajima juu ya kile kilichomtokea Slaa kwa mkewe.
 
“Nilimsindikiza hadi kwenye gari, begi tukaliacha mlangoni. Alilala kwenye gari hadi asubuhi, nikamuomba mama tena na kumsihi amuache baba ili aingie ndani," alisema.
 
Mwakatabu alisema walipoingia nyumbani asubuhi, walikaa pamoja na alieleza masharti aliyompa Dk. Slaa kwamba ili arejee ndani ya nyumba hiyo ni lazima afuate masharti atakayompa.
 
“Kama atarudi Chadema, nyumbani kwangu simtaki. La pili, kama Lowassa atajiunga na Chadema, nimemwambia aandike barua ya kuacha uanachama ndani ya Chadema...baada ya maneno hayo nilisema tumempoteza mzee.. ndani ya muda mfupi, Dk. Slaa alimuelekeza dereva wake kumpeleka (Josephine) Mushumbuzi katika mizunguko yake kwa kutumia gari la chama,” alisema.
 
SABABU KUJIUZULU
Askofu Gwajima anasema alifika nyumbani kwa Dk. Slaa mapema asubuhi na alimweleza kuwa amelala ndani ya gari. Alionyesha ujumbe aliotumiwa na Slaa majira ya saa 7:19 usiku.
 
Alionyesha ujumbe huo kwa waandishi wa habari ambao ulisema:“Baba familia yangu inavunjika, nimeamua kujiuzulu. Kuanzia leo nimejitoa kwenye siasa”.
 
Aidha, alisema kauli ya Dk. Slaa kuwa amejitoa Chadema kwa sababu ya ufisadi wa Lowassa si sahihi bali mchumba ndiye amemkamata.
 
“Dk. Slaa alikuwa Padri, hana uzoefu wa ndoa. Afadhali sisi wengine ambao ni wachungaji tunaoa, tuna uzoefu wa kutuliza lolote linapotokea,” alisema.
 
Alisema alikutana na Josephine (Mushumbuzi) eneo la Shekaina Garden, na alirekodi mazungumzo yote, huku akimbembeleza na alieleza jinsi alivyojiandaa kuwa mke wa rais (First Lady), alijiandaa kibiashara na alishaeleza watu hilo na kwamba hatakubali.
 
“Julai 28 mwaka huu, nilimuita tena (Mushumbuzi) eneo la Tegeta Kibo Complex, nikiwa na mtu mwingine...  tulikaa ndani ya gari yake, tulimuomba kuanzia saa sita hadi nane… ikumbukwe hiyo ndiyo siku Lowassa aliyopewa kadi ya Chadema,” alisema na kuongeza:
 
“Mama alitueleza alipaswa kuniomba mimi kwanza, alikubali kwa sharti moja la Lowassa kutopokelewa Chadema na mkutano wa saa 9:00 siku hiyo ufutwe. Tulimueleza jambo hilo halipo leo, jana, harakati za ukombozi zimeanza muda mrefu, mtu mmoja hawezi kuturudisha nyuma.”
 
Gwajima ambaye muda mwingi alijigamba kumfahamu kwa undani Dk. Slaa, alisema aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro, Philemon Ndesamburo, alitumwa kuzungumza na Mushumbuzi lakini alishindwa kumpata.
 
MCHUNGAJI ANENA
Mchungaji aliyezungumza na mchumba wa Dk. Slaa baada ya kuombwa kufanya hivyo na Ndesamburo, Maxmillian Machumu, alisema ni kweli aliongea na mchumba wa Dk. Slaa ambaye aliendelea na msimamo wake wa kutaka awe mke wa rais na alishafanya maandalizi makubwa.
 
“Dk. Slaa ametekwa, mwenye nguvu ametekwa, hadi juzi nimeongea naye kwenye simu, msimamo wake ni kuwa mke wa rais na amemnyima kurudi Chadema,” alisema.
 
ASKOFU KAKOBE 
Alisema Agosti 4 mwaka huu, Askofu Zakaria Kakobe alijaribu kumshawishi akubali kumruhusu mumewe aendelee na shughuli za kisiasa Chadema, lakini alikataa na kuendelea na msimamo wa kutaka kuwa ‘First Lady’. Gwajima alidai kuwa mazungumzo hayo pia yalirekodiwa.
 
AMUONYA SLAA
Gwajima alisema iwapo Dk. Slaa atajitokeza tena hadharani na kuendelea kuwashambulia viongozi wa dini wakiwamo maaskofu, wachungaji, masheikh na maimamu ataanika mambo yake mengine zaidi ikiwamo jinsi alivyokuwa akiishi ndani ya nyumba yake, alivyotelekeza familia yake ya watoto wawili na mke wa ndoa.
 
Alisema kudai kuwa maaskofu wa Kanisa Katoliki wamepewa rushwa ni kulidhihaki kanisa hilo kwa kuwa ni kubwa na kanisa mama, na pia ni kuwachafua ili wasiaminike kwa waumini wao na kusahau kuwa alisomeshwa nao (Katoliki); alikuwa Padri na Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (Tec).
 
Aidha, Gwajima aliwataka viongozi wa dini watakoshambuliwa tena kukaa kimya kwa shutuma zozote zitakazotolewa na Dk. Slaa na kwamba wamuachie yeye, atazijibu kila wakati itakapobidi na kwamba, wakumbuke viongozi hao wana wafuasi na ni wapiga kura wa mwaka huu.
 
USALAMA WA TAIFA
Gwajima bila kumumunya maneno amewarushia kombora Usalama wa Taifa kutumika na kuwa nyuma ya kiongozi huyo kwa malengo ya kukisaidia Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi huu.
 
“ Dk. Slaa wa leo siyo wa miaka iliyopita tunaongea na mtu tofauti kabisa… tulisikia akihojiwa na Televisheni moja na kukiri kwa sasa analindwa na Usalama wa Taifa…kuna mtu nyuma yake anamtuma kufanya haya anayofanya ndiyo maana anatukana maaskofu, nawaambia ‘strategic’(mkakati) ’ hii imeshindwa watafute nyingine, hii ndiyo silaha ya mwisho katika Bunduki yao na imewarudia inawaangamiza,” alisema.
 
Alisema usalama wa taifa ni usalama wa nchi na siyo wa kulinda watu wachache wala CCM, na kwamba ni aibu kwa Usalama kuhusika kutukana maaskofu na kwa kufanya hivyo ni kujivunjia heshima.
 
“Nawaonya sana mnajivunjia heshima, mnamharibia mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli, waachane wapigane masumbwi kwenye majukwa ya siasa na siyo kumuitwa Gwajima Mshenga na kumrundikia kesi nyingi,” alisema.
 
Aidha, alisema kwa sasa ameweka kiporo safari ya Dk. Slaa nchini Afrika Kusini, aliambatana na watu wanne na mizigo aliyokuwa amebeba.
 
Alisema kinachomsimbua Dk. Slaa ni wakati na majira kwani huwezi kushindana navyo, kwa kuwa wakati wa baridi unatakiwa kuvaa koti kukabilia baridi na hauvai koti kutoa baridi na kwamba wakati huu siyo wa kushindana na majira bali kuangalia anayestahili katika majira husika.
 
Akizungumza na Nipashe, Mlinzi Mwakitabu alisema ameacha kazi kwa Dk. Slaa Septemba mosi mwaka huu, na kwamba Emmanuel Njile bado anaendelea na kazi.
 
Alisema walipelekwa na Gwajima lakini walikuwa wanalipwa na Chadema na kuwataja wenzake ambao walianza kazi tangu mwaka 2001 hadi 2014 kuwa ni Sixmund na Edwin.
 
Nipashe ilimtafuta Mushumbuzi na Dk. Slaa, lakini simu zao hazikupatikana na hata walivyotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi haukujibiwa, na kwa mujibu wa taarifa ambazo hazijathibitishwa zinaeleza kuwa wamesafiri kwenda nchini Marekani.
 
Imeandikwa na Salome Kitomari, Moshi Lusonzo, Frank Monyo na Beatrice Shayo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment