dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, September 9, 2015

Je, ishara ya ukomavu wa demokrasia au dalili za kansa ya siasa uchwara?


TOFAUTI kubwa ya msimu huu wa uchaguzi na misimu mingine iliyopita ni kishindo kilichosababishwa na baadhi ya wanasiasa maarufu nchini kuvihama vyama vyao vilivyowajenga kisiasa kwa muda mrefu. 

Vyama vyote vikubwa, yaani CCM, CUF na Chadema vimehamwa na wanasiasa wao maarufu kitaifa. Sitaki kupoteza muda kutaja majina ya wanasiasa walioamua kutumia haki yao ya kikatiba kuhama. Lengo la makala haya siyo kujadili watu bali kujadili masuala ya msingi kwa manufaa ya taifa letu.

Watanzania wengi wanaendelea kujiuliza ikiwa wimbi hili ni ishara ya ukomavu wa demokrasia au ni dalili za kansa ya siasa uchwara. Napenda nitumie mtazamo wa kihistoria kushiriki katika mjadala huu muhimu.

Kihistoria, nchi zote za Afrika zimezalisha aina kuu mbili za wanasiasa. Aina ya kwanza inajumuisha wanasiasa walioongoza harakati za ukombozi. 

Wanasiasa hao walijitoa mhanga kujenga mshikamano wa kijamii na kisiasa dhidi ya mfumo wa kikoloni. Wanasiasa wa aina hii waliasisi na kuongoza vyama vya siasa vilivyosanifu na kufuata dira ya ukombozi. Vyama vya TANU, ASP, FRELIMO na ANC ni miongoni mwa vyama vilivyoasisiwa na wanasiasa wa aina hii ya kwanza.Katika kipindi chote cha mapambano ya ukombozi, wanasiasa hao walitumia vipaji na mali zao kwa mtindo wa kujitolea. Hawakuwa na uchu wa madaraka na wala hawakutumia mamlaka yao au umaarufu wao kama nyenzo ya kujilimbikizia mali na sifa. Mshikamano wa kijamii na kisiasa walioujenga na dira ya ukombozi waliyoisanifu na kuifuata vilikuwa kichocheo cha kupatikana kwa uhuru wa kisiasa katika nchi zao. Wote waliamini kuwa binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja. 

Walidhamiria kwa dhati kujenga jamii huru, yenye usawa, inayojitegemea na inayoheshimu utu. Hawa walikuwa wajamaa kifikra na kivitendo. Maisha ya kisiasa ya wapigania uhuru kama Mwalimu Nyerere, Mzee Abeid Karume, Kwame Nkrumah, Bibi Titi Mohammed, Mzee Ali Migeyo, Patrice Lumumba, Samora Machel na Mzee Nelson Mandela ni kielelezo cha sifa njema za wanasiasa walioongoza mapambano ya ukombozi. Bila shaka, maisha ya wanasiasa wa aina hii ni hazina ya maarifa kwa Waafrika wanaotambua umuhimu wa historia ya mapambano ya ukombozi wa nchi zao. Katika zama za sasa, wanasiasa wa aina hii ni wachache na adimu sana.

Katika miaka zaidi ya kumi ya utumishi wangu kwenye vyuo vikuu vya umma nchini (Mzumbe na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) nimeshuhudia kiwango cha chini sana cha uelewa wa baadhi ya wanafunzi wangu kuhusu historia tukufu ya vyama vya ukombozi na sifa nzuri za wanasiasa walioongoza vyama hivyo. 

Kuna wakati baadhi ya wanafunzi wangu wa mwaka wa tatu walishindwa kufafanua kirefu cha chama cha TANU. Wapo baadhi ya wanafunzi wangu wa mwaka wa pili ambao walishindwa kunieleza Samora Machel alikuwa nani. Siwalaumu wanafunzi wangu hata kidogo. Ujinga wa aina hii miongoni mwa vijana wa Afrika ni hatarishi na ni kielelezo cha ubutu wa mfumo wa elimu yetu. Hili ni bomu la maangamizi linaloweza kulipuka wakati wowote.

Ushupavu, utu, usikivu, unyenyekevu na uadilifu wa wanasiasa wa kizazi cha kwanza ndiyo chimbuko la uhuru wa kisiasa uliopatikana katika nchi zote za kiafrika. Miaka michache baada ya uhuru, mambo yalibadilika ghafla na kwa kasi. Nchi nyingi za kiafrika ziliingia katika awamu mpya ya utawala kandamizi wa mabeberu na vibaraka wao. Baadhi ya waasisi wa mapambano ya ukombozi walioshika hatamu za uongozi wa dola baada ya huru walipinduliwa, wengine walifungwa, wengine waliuwawa kikatili na wengine walilazimika kulegeza misimamo yao ya kimapinduzi ili wasishikishwe adabu na mabeberu.

Kutokana na hila na mbinu za mabeberu na vibaraka wao dira iliyoongoza mapambano ya ukombozi haikufuatwa tena. Ombwe la dira ya ukombozi likajazwa na siasa uchwara. Ikazuka aina ya pili ya wanasiasa wasio na ari wala uwezo wa kuendeleza mapambano ya ukombozi. Wanasiasa wa aina hii ndiyo wamekuwa wakiitawala Afrika kwa takriban miongo minne sasa. Mwongozo wa CCM wa 1981 umechambua kwa ufasaha namna mabeberu na vibaraka wao walivyofanikiwa kuiondoa Tanzania katika njia mwafaka ya kujenga taifa huru na linalojitegemea.

Hivi sasa tunashuhudia ubeberu ukiendelea kutamalaki barani Afrika na matumaini ya wavuja jasho yakizidi kuyoyoma. Afrika imesalimu amri kwa mabeberu na vibaraka wao. Tayari nchi mbili za kiafrika, Sudan na Libya zimesambaratika kabisa kutokana na hila na mbinu za mabeberu na vibaraka wao. Hivi sasa nchi hizo zimepasuka vipande na ni vigumu kutabiri kama zitatawalika tena.

Ingawa mfumo wa ubaguzi wa rangi katika nchi ya Afrika Kusini haupo tena kisheria mpasuko wa kijamii katika nchi hiyo uko pale pale hata baadaya ya ANC kushika hatamu za dola. Walioendesha, kufadhili na kukomaza mfumo wa ubaguzi wa rangi leo hii wanasifiwa na kutukuzwa kama wawekezaji na wabia wa maendeleo. Inasikitisha kushuhudia wanasiasa wa kizazi cha sasa wakikumbatia mifumo hii kandamizi. 

Kila mara, taasisi za kibeberu zinawakejeli mamilioni ya mafukara wa Afrika kwamba uchumi wa nchi zao unakuwa kwa kasi kutokana na ubora wa sera zinazowafukarisha. Ukubwa na utajiri wa nchi za Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (zamani Zaire) vimekuwa laana badala ya kuwa neema kwa wavujajasho. Maeneo mengi katika nchi hizi hayana usalama wa kutosha ingawa ajenda ya amani na usalama huhubiriwa na kila mwanasiasa anayesaka madaraka kila ufikapo msimu wa uchaguzi.

Kuanzia katikati ya miaka ya 1980 hadi sasa, na hasa baada ya ujio wa sera za ubinafsishaji na itikadi ya kuvunja misingi ya utaifa, mwelekeo wa siasa za kimapinduzi katika nchi zetu umepindishwa. Huu ndio wakati ambapo ardhi ya umma imekuwa ikiuzwa kama mbuzi. Hivi sasa, ardhi ya umma siyo tena chimbuko la uhai na uhuru wa Waafrika bali ni kichocheo cha migogoro hatarishi mijini na vijijini.

Huu ndiyo wakati ambapo huduma muhimu, hasa elimu na afya, zimegeuzwa kuwa bidhaa zinazouzwa sokoni.

Hata soko la kuuza na kununua kura limeanzishwa wakati huu. Vyama vipya vya siasa, na hata vile vikongwe, vyote vinaendeshwa na wanasiasa uchwara kama mitambo yao binafsi ya propanda chonganishi. Kura haziombwi tena bali zinanunuliwa.

Kila mpiga kura amepangiwa bei yake na baadhi ya wagombea wamejipa jukumu la kuwa mashine za ‘ATM’ za wapiga kura hasa wale waliokata tamaa. Vile vile, baadhi ya vyama vya siasa vinapata ufadhili fedheheshi kutoka katika makampuni na mataifa ya kibeberu. Vibaraka wa ubeberu, hasa wale wanaopigia debe sera za ‘uzawa’ nao wamejiingiza katika mchezo huu mchafu wa biashara ya kura kwa matarajio kwamba watakirimiwa na wanasiasa watakaoweza kununua kura nyingi.

Vyama vya wafanyakazi na vyama vya ushirika, ambavyo viliwahi kuwa chimbuko la mshikamano wa wavujajasho, vimekufa kifo cha mende. Wakulima na wafanyakazi siyo chimbuko la uhalali wa kisiasa tena. Badala yake, wanasiasa uchwara wamesambaa mitaani na vitongojini wakishindana kuwaghilibu na kuwachonganisha mamilioni ya vijana waliofukarishwa. Ufukarishaji umebatizwa jina jipya la ‘ujasiriamali’ na mafukara wamepachikwa majina ya kebehi kama vile: ‘mama na baba nitilie’, ‘wamachinga’, ‘wanavikoba’, ‘vijana wa bodaboda’na ‘wachimbaji wadogowadogo’.

Mabeberu na vibaraka wao wanaendelea kutumia mkanganyiko huu wa kisiasa na kiitikadi kuziponda kauli, sera na vitendo vya kimapinduzi vya wapigania uhuru. Kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano pamoja na taasisi za propaganda, wanasiasa uchwara wanawachochea vijana wa Afrika kuvunja nchi zao kwa mikono yao wenyewe. Miongoni mwa athari mbaya za siasa uchwara zilizotamalaki ni kupuuzwa kwa historia tukufu ya mapambano ya ukombozi na pia kumomonyoka kwa misingi ya utaifa.

Kwa kuwa hamasa za uchaguzi tunazozishuhudia hivi sasa hapa nchini hazijachochea mjadala mkali juu ya namna ya kuwaandaa na kuwapata wanasiasa wenye sifa kama walizokuwa nazo waasisi wa mataifa yetu, nachelea kusema kwamba wimbi la wanasiasa wanaohama vyama vyao ni ishara ya ukomavu wa demokrasia. Kwa tathmini yangu, hamasa hizi ni dalili za kansa ya siasa uchwara.

Katika muktadha huu wa siasa uchwara, ningependa kuwaasa watanzania wenzangu kwamba hatima ya uhuru na utu wetu iko mikononi mwetu. Jambo muhimu sana la kuzingatiwa na watanzania wanaothamini damu na jasho la wapigania uhuru ni kukataa katakata kuchonganishwa na wanasiasa uchwara ambao lengo lao mahsusi ni kuingia Ikulu kwa gharama yeyote.

Nihitimishe kwa kusisitiza kwamba uchaguzi wa Tanzania wa mwaka huu unatupa fursa adhimu na adimu ya kutafakari kwa undani chimbuko la hizi siasa uchwara tunazozishuhudia mwaka huu. Ukweli ni kwamba biashara ya kura haina tofauti na biashara ya utumwa. Utumwa ni udhalilishaji wa utu wa kiwango cha juu sana. Kwa hiyo, watanzania tusikubali kuuza utu wetu. 

Pia tusikubali kuchonganishwa na watawala watarajiwa na hatimaye kuvunja taifa letu kwa mikono yetu wenyewe. Kazi ya ukombozi wa Afrika siyo mradi wa kutekelezwa kwa mtindo wa fastafasta au ‘Matokeo Makubwa sasa (BRN)’ bali ni mapambano endelevu yatakayovihusisha vizazi vingi kwa miaka mingi ijayo. Mgombea yeyoye anayejitambisha au kutambulishwa kama mkombozi wetu tumuogope kama ukoma. Tujiandae kuitafuta tiba ya kansa ya siasa uchwara inayolitafuna taifa letu kwa kasi.

No comments :

Post a Comment