NA MHARIRI
6th September 2015
Fedha zinazopatikana hutumika kama zilivyoainishwa kwenye mchanganuo uliowashawishi wafadhili wenyewe, na serikali haiingilii matumizi ya fedha hizo zinazotolewa na wahisani kwa taasisi na sekta hizo binafsi.
Walengwa wanahitaji kujua asasi hizo zinafanya nini, na kwamba fedha wanazozipata zinatumikaje, na serikali pia inaweza kuhitaji taarifa hizo kwa sababu za kiusalama, hivyo taasisi hizo zisione kama ni usumbufu zinapotakiwa kutoa taarifa za matumizi ya misaada ya wafadhili wao.
Mwishoni mwa wiki hii, Rais Jakaya Kikwete alizitaka asasi za kiraia kuweka wazi fedha wanazozipata kutoka kwa wafadhili na namna wanavyozitumia, alitoa wito huo jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akifungua mkutano wa Takwimu Huria Kanda ya Afrika (Africa Open Data) uliojumuisha wajumbe kutoka zaidi ya nchi 30 za Afrika.
Rais Kikwete alisema asasi hizi zinapoulizwa taarifa zao zinatakiwa ziwe wazi, kinyume chake wakiulizwa wanaona kama wanaonewa au kuingiliwa masuala yao binafsi, alifafanua kuwa hata serikali hupokea fedha kutoa kwa wahisani na taarifa zake ziko wazi kwa kila anayehitaji kufahamu.
Rais alibainisha kuwa serikali kwa kiasi kikubwa inajitahidi kutoa taarifa zinazohusu takwimu katika mambo ambayo ni wazi kwa umma, akatoa rai hata katika asasi za kiraia kuweka matumizi yote wazi ili kuwe na uwajibikaji.
Katika hatua ya serikali kutekeleza dhamira ya uwazi wa matumizi ya fedha kwenye halmashauri mbalimbali nchini, Rais Kikwete alikumbusha kuwa aliamua kuanza kujadiliwa kwa uwazi taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bungeni na hatua zikachukuliwa kwa taasisi ambazo hesabu zao hazikuwa sawa.
Tunaamini kuwa kuweka wazi takwimu za matumizi ya fedha zitokazo kwa wafadhili ni hatua moja kubwa katika uwajibikaji katika sekta mbalimbali ambao pia ni kichocheo cha maendeleo.
Thamani ya mfumo wa kuweka uwazi wa matumizi ya fedha za wafadhili huharakisha maendeleo ya asasi binafsi na pia hutoa nafasi kwa wanachama wa asasi husika kushuhudia maendeleo yao na inapolazimika kuwa na fursa ya kuhoji masuala mbalimbali yanayofanywa na sekta binafsi.
Tunaamini kuwa ipo miradi mikubwa ya asasi binafsi inayopokea fedha kutoka kwa wafadhili, miradi ya kusaidia wanawake na watoto, kilimo, madini, uvuvi na wafadhili wanawasiliana moja kwa moja na asasi hizo bila kupitia taasisi nyingine.
Kama taarifa za namna fedha zinazofadhili miradi hiyo zinatolewa kwa uwazi, hakuna dosari wala utata utakaoweza kujitokeza.
Ni imani yetu kuwa asasi za kiraia zitazingatia maelekezo hayo ili kuboresha uwajibikaji ndani ya sekta binafsi na pia kuwapa imani wafadhili ili waendelee kutoa fedha kwa maendeleo ya wananchi na taifa.
Tunaamini kuwa wafadhili huridhika kutoa misaada kwa miradi ya maendeleo yenye kupunguza umaskini kwa walengwa wao, pia wafadhili hawawezi kutoa fedha kwa ajili ya kudhamini vikundi vya uhalifu nchini.
Tunakubaliana na maelekezo ya Rais Kikwete aliyoyatoa kwa wajumbe wa mkutano huo wa Takwimu Huria Kanda ya Afrika kuwa hata asasi za kiraia zitaona umuhimu wa kuweka wazi matumizi ya fedha zinazotolewa na wafadhili.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment