Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, September 13, 2015

Utetezi wangu kwa Lowassa


JANUARI 2007 nilihamia Dar es Salaam, nikishughulika karibu na Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petrol (St. Peter). Februari 23, 2007 nilisali “njia ya msalaba” hapo “ St. Peter”.
Baada ya “njia ya msalaba”, niliona akina mama wanamsalimia mwenzao naye anatoka kanisani niliyeambiwa kwamba ni mke wa Waziri Mkuu, Regina Lowassa.
Baadaye katika “nia za misa” katika misa za katikati ya wiki pale “St. Peter”, nikawa nasikia jina “Regina Lowassa” likijirudia. Utasikia Jumatatu kamuombea marehemu fulani, kesho yake kaomba baraka kwa jambo fulani.
Kuhamia Dar es Salaam kuliniweka karibu na “Cathedral Bookshop” iliyoendeshwa na masista wanaoitwa “Paulines Daughters” ambao kufikia mwishoni mwa 2007 walikuwa wamekwishanizoea.
Mwaka 2008 ulipoanza, Askofu Methodius Kilaini alitoa kitabu kiitwacho “Kardinali Rugambwa-Tulivyomfahamu”. Ukurasa wa nane kina picha ya sita anaonekana Regina Lowassa akimpongeza Laurean Kardinali Rugambwa kutimiza miaka 25 ya ukardinali. Kardinali Rugambwa alitimiza miaka 25 mnamo Machi 28, 1985.Katika picha hiyo Edward Lowassa, japo hakutajwa, anaonekana kwa mbali, nywele zake zote zikiwa bado nyeusi.
Aprili 14, 2009, Polycarp Kardinali Pengo alizindua kitabu kilichotungwa na Regina Lowassa kinachoitwa “Walk the path with my “diary” in Israel-The Holy land”.
Sijui kama Regina Lowassa anatambua kwamba kitabu chake kinafundisha maisha ya mtu kuandika matukio ya kila siku kwenye “diary”. Wasiojua umuhimu wa “diary” wamsome Samuel Pepys ambaye “diary” yake ni sehemu muhimu katika historia ya Uingereza.
Siku moja rafiki yangu Restituta Issaka, alinishawishi nihudhurie sherehe ya kwaya ya “Don Bosco” ya Kigango cha Tabata-Kimanga. Lakini aliponifahamisha kwamba mgeni rasmi ni Regina Lowassa sikwenda, kwa sababu ndizo siku RICHMOND ilikuwa inaitwa “Rich-Monduli”.
Wale “Paulines Daughters” walijenga duka jipya likaitwa “Paulines Book and Media Centre”. Walipokaribia kulizindua walinialika nihudhurie uzinduzi huo.
Jioni Machi 27, 2010, Polycarp Kardinali Pengo aliongoza msafara wetu sisi waalikwa kuingia dukani kulizindua. Humo dukani ndipo nikamuona Regina Lowassa, amesimama mita tatu kutoka nilipo.
Ingawa hanijui (Regina) nikatumia ukaribu huo kumpongeza “hongera kwa kutoa kitabu kizuri”, akanijibu “Asante lakini nimekiandika nikiwa sina utaalamu wa kuandika”.
Wakatoliki ambao ni majirani zake Regina wanafahamu juhudi yake hudhuria “Jumuiya Ndogondogo” huku akiwa mke wa Waziri Mkuu.
Aprili 13, 2006 na Aprili 05, 2007 ni “Alhamisi Kuu” zilizomkuta Regina kama mke wa Waziri Mkuu. Licha ya wadhifa huo, Regina alizoea kukesha usiku wa “Alhamisi Kuu” pale “St. Peter” kuabudu Ekaristi.
Machi 19, 2012 ilikuwa siku ya kumsimika askofu Salutaris Melchior pale Ifakara. Huko nako, Regina Lowassa alialikwa kama mgeni kwa Jimbo Katoliki la Mahenge.
Kuonekana kwa Rais Mstaafu (Ali Hassan Mwinyi) na Waziri Mkuu Mstaafu kwenye sherehe ile, kulimfanya Mkuu wa Mkoa, Joel Bendera autambulishe pia uwepo wa Edward Lowassa, bila kujijua anatengeneza kosa.
Kosa lenyewe ni kwamba Lowassa hakutakiwa kutambulishwa kwani mgeni aliyealikwa ni mkatoliki kutoka Jimbo la Dar es Salaam yaani Regina Lowassa, lakini kaja na mumewe mlutheri, Edward Lowassa:{KIONGOZI: Machi 30, 2012, uk. 04}.
Ndivyo ninavyoweza kumsimulia Regina ambaye kwa jina lake juzi, (Septemba 07, 2015) kalenda ya Kanisa Katoliki duniani inamkumbuka jina lake, Mtakatifu Regina, msimamizi wa wafugaji hasa wa kondoo.
Ilifika mahala nikaanza kujiuliza, hivi hata mimi Jose, naichukia familia ya Lowassa sababu nina ushahidi upi? Kwa nini Edward Lowassa hapelekwi mahakamani?
Usidhani swali hili watu wameanza kujiuliza siku Lowassa alipojiunga na Chadema. Gazeti la KULIKONI la Februari 08, 2008, yaani siku moja tu baada ya kujiuzulu, kwenye ukurasa wa tatu liliandika hivi “Wataka Lowassa awajibishwe kisheria”.
Lowassa alipojiuzulu, Bunge liliendelea kutumia “sovereignty” yake kuijadili RICHMOND.
Gazeti la KULIKONI la Februari 16, 2008, ukurasa wa mbele lilisema hivi: “Serikali imeunda timu maalumu itakayopitia mapendekezo yote ya kamati teule ya bunge kuhusiana na sakata la RICHMOND ili kutoa mwelekeo na namna ya kufanyiwa kazi kulingana na matakwa yake”.
Sasa, ukitaka kuwa “mwanahistoria” mzuri, basi kamilisha “uanahistoria” wako kutukumbusha na historia inayoanzia siku Lowassa amejiuzulu hadi siku Bunge lilivyoridhishwa na utekelezaji wa maazimio yale ndipo likafunga mjadala wa “RICHMOND”.
Tumeona mwaka 1985 Regina na Edward Lowassa wameshiriki tafrija ya kumpongeza Laurean Kardinali Rugambwa. Je, siku hiyo napo Lowassa alikuwa anajipitisha makanisani kuanza kampeni mapema ili kumrithi Julius Nyerere urais miezi minane iliyofuata?
Wakati huo hata padri Polycarp Pengo ndiyo kwanza ametimiza mwaka akiwa askofu huko Nachingwea. Wewe msomaji ulikuwa wapi?
Mimi tu nimewahi kukataa mialiko kama ule wa “Don-Bosco”, kwa sababu tu Regina Lowassa alikuwa mgeni rasmi.
Rafiki yangu Marco Bisake alinisihi nijumuike sherehe ya kwaya yao (St. Kizito) ya Parokia ya “Beata Annuarite” ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam mnamo Juni 07, 2009. Nilimbishia kwa kumuuliza kwamba “kwa nini St. Kizito mnamkaribisha mama Salma Kikwete kama mgeni rasmi wakati si mkatoliki”? Sikwenda.
Hivyo, mialiko wanayoikataa akina Lowassa huenda ni mingi kuliko iliyoonwa na “mapaparazi” wanaonufaika kuifuatilia hiyo familia.
Binafsi sijali Lowassa kushindwa au kumshinda John Magufuli. Kikubwa ninachojali, ametoa mchango mkubwa kuifundisha jamii kujenga ujasiri wa kukabiliana na tuhuma ziitwazo “cheap popularity” na wakati mwingine zinaitwa “character assasination”.
Tuhuma za namna hii zimekuwa ni mazoea katika jamii na hufikia hadi kusambaratisha urafiki, ujirani, ukoo na ajira za kazini.
Sasa hivi hata watoto wanauliza, “hivi kwa nini huyu Lowassa hajapelekwa kortini kwa miaka minane sasa”? Hebu sikia majibu kwa swali hili.
Jibu la moja linasema “kesi ya jinai haina “limitation” anaweza kupelekwa hata kesho”. Wakati huo jibu jingine linasema “ukishapeleka ushahidi mahakamani kesi inakuwa ya Jamhuri, yaani wewe huna tena “locus stand”. Jibu la tatu linasema “nataka mdahalo”.
Waliomtuhumu Jacob Zuma hawakuishia kusema “tuna ushahidi mzito” au “tulijiridhisha bila shaka”. Rais Thabo Mbeki alipomuondoa Jacob Zuma serikalini Juni 14, 2005, msururu wa kesi ulimfuata Zuma pale pale bila kuwepo msururu wa sababu za kutomshitaki.
Kukosa uthibitisho ndiko kuliifanya Mahakama ya Kanisa Katoliki, iliyoitwa “Inquisition”, imuadhibu Galilei Galileo mwaka 1633 kwa kuhubiri mtaani kwamba dunia inalizunguka jua yaani “Heliocentrism”.
Uongo unaolichafua Kanisa kwamba lilimuonea Galileo, ni uongo ambao mabilioni wamekufa wakiuamini, kwa sababu tu ulisambazwa na maprofesa wa sayansi wa dunia hii!
Lakini maprofesa hao (astronomers) kamwe hawahubiri kwamba, ushahidi wa kisayansi alioutumia Galileo pale mahakamani Roma, ulijaa hoja finyu zilizopanguliwa kitaalamu na wanasayansi wenzake.
Galileo akashindwa kesi, akawekwa kizuizini maisha yote pale Vatican ili asiendelee kuropokea wananchi jambo lililomshinda kuthibitisha.
Hata dhana inayolinganisha ushabiki kwa Lowassa kama mkataba na “shetani” ni ya mtu asiyejua dini. Shetani aliupata ushetani kama adhabu baada ya kuthibitika bila shaka kwamba amemuasi Mungu.
Tumefundishwa hivyo kwenye Katekism ya Kanisa Katoliki, ibara ya 391 na 414. Asiye mkatoliki asome Ufunuo wa Yohana 12:7-9.
Edward Lowassa si kama shetani kwani hajathibitishwa ukosefu wowote kwa uamuzi wa mahakama yoyote duniani.
Nimeonyesha humu hata Laurean Kardinali Rugambwa, alivyokuwa karibu na familia ya Lowassa. Siku ya kukizindua kile kitabu cha Regina Lowassa, nyumbani kwa Lowassa kulikuwa na zaidi ya wafuatao: 1: Polycarp Kardinali Pengo (mkatoliki), 2: askofu Alex Malasusa (Mlutheri), 3: askofu Elinaza Sendoro (mlutheri), 4: Mchungaji Christopher Mwakasege (mpentekoste), 5: Monsignor Julian Kangalawe (mkatoliki), 6: Padri Benedict Shayo (mkatoliki).
Ndipo siku ambayo Polycarp Kardinali Pengo alipotamka palepale nyumbani kwa Lowassa “tangu sasa mimi ni mwenyeji wa nyumba hii”: {RAI: Aprili 16, 2009, uk. 01}.
Hivyo, maaskofu na wachungaji, hawahitaji kuelekezwa na vyombo vya habari, wala mahasimu wa Lowassa jinsi ya kuishi na familia ya Lowassa.
Neno fisadi lilipovuma sana tulisikia viongozi ambao magari yao yalipondwa mawe na wengine kuzomewa “fisadi huyoooo”. Lakini sikuwahi kusikia Edward Lowassa amepondwa mawe, iwe msafara wake, au yeye mwenyewe kuzomewa.
Mwaka 1981, Rais Julius Nyerere alituhumiwa kwa ufisadi wa kuficha fedha kwenye benki huko Switzerland. Tuhuma hizo, zilisemekana kwamba zimendikwa kwenye gazeti la “Time Magazine” au “Newsweek”.
Tony Avirgan, na mwenzake Martha Honey, ni mwandishi aliyeruhusiwa na Rais Nyerere kushiriki mstari wa mbele kwenye vita ya Idi Amini na hata kuchukua picha za sinema ya vita: {War in Uganda: The Legacy of Idi Amin, ISBN: 9789976100563, uk. x}.
Tony aliandika makala ikachapishwa Juni 15, 1981 kwenye “THE GUARDIAN” la London (Uingereza), kisha akairudia makala ile Juni 17, 1981 kwenye DAILY NEWS ya ya Tanzania.
Kwenye makala ile ya Tony, DAILY NEWS ilitangaza zawadi nono ya shs. 20,000/= kwa yeyote duniani atakayelipata gazeti lililodaiwa kufichua ufisadi ule wa Rais Nyerere. Tony akawa amewaumbua wababaishaji wote duniani walioeneza tuhuma zile.
Kumbe, Lowassa alipomjibu mwandishi kwa kujiamini kwamba “mwenye ushahidi kuhusu RICHMOND aupeleke mahakamani la sivyo shut-up and keep quiet”, alirudia mbinu ileile ya Tony Avirgan ya mwaka 1981 ya kuwanyamazisha (shut-up) wasambaza-tuhuma.
Wapo wanaodhani Mwembeyanga ndiyo “venue” ya kwanza kutangaza orodha ya mafisadi. Orodha ya kwanza kabisa baada ya vyama vingi ni ile iliyotajwa na Oscar Kambona, Novemba 21, 1992 pale Jangwani alipotangaza kwamba Mwl. Julius Nyerere, Rashid Kawawa na Amir Jamal wameficha fedha Ulaya: {DAILY NEWS: December 05, 1992, uk. 01}.
Lakini Oscar Kambona, kama walivyo “watuhumu” wengi, hakuwahi kuuwasilisha ushahidi wake kokote hadi anafariki, Juni 04, 1997.
Hivyo, waliomtuhumu Mwalimu Julius Nyerere kwa ufisadi, tena si mara moja, wasitulaumu kwa kuwapuuza. Tungekuwa wajinga kama tungeendelea kuamini tuhuma zao kwa ushahidi ambao hatujui kama hata ulikuwemo mifukoni mwao.
Hivyo, na hawa wanaotamani tuendelee kumtuhumu Lowassa, kama walivyofaulu mwanzoni kuninasa hadi nikamchukia Regina Lowassa kama, nao wasitulaumu. Sababu za kuachana nao au kuwapuuza sasa hivi ni zilezile zilizofanya tuwapuuze waliomtuhumu ufisadi Mwalimu Nyerere mwaka 1981 na 1992.
- See more at: http://raiamwema.co.tz/utetezi-wangu-kwa-lowassa#sthash.ilPG6nJa.dpuf

No comments :

Post a Comment