dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, September 7, 2015

Lowassa atikisa kuiteka Dar leo.

Mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.
Zikiwa zimebakia siku 47 Watanzania kupiga kura kuchagua viongozi wanaowataka, mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, ameendelea kuungwa mkono na umati huku akiwataka wasiwe waoga katika suala la kuamua hatima ya taifa lao.
 
Lowassa alisema hayo jana wakati akihutubia wananchi wa Nzega mjini kwenye uwanja wa Uhuru.
 
“Bado siku chache utaamua hatima ya nchi yako, maji safi, elimu ya aina gani, huduma gani, ulale vipi hospitali, utaamua ule mlo mmoja ama mitatu angalieni miaka 50 nyuma, jipime uamue utaendelea hivi mpaka lini, fanya maamuzi sahihi, tupeni kura zenu,” alisema.
 
“Piga kura, linda kura tuiondoe madarakani serikali ya CCM, jinsi mlivyojaa hapa uwanjani mkienda kupiga kura walahi nimeshakuwa rais,” alisema huku akishangiliwa na wananchi.
 
Lowassa alirejea kutoa ahadi ya kuboresha elimu ambayo itakuwa bure na kufuta ushuru wa mazao kwa wakulima ikiwa wananchi watampa ridhaa ya kuwa rais wa awamu ya tano.
 
Alisema akichaguliwa atahakikisha anaunda serikali makini yenye kujali maslahi ya wananchi.Alisema inashangaza mahasimu wao, Chama Cha Mapinduzi  (CCM) wanaeleza kuwa watu wanaofurika katika mikutano ya kampeni ya Ukawa wanapelekwa na malori wakati siyo kweli.
 
Wakati akihutubia wananchi hao, Lowassa alipewa nafasi na kuwasalimia wananchi kwa kusema CCM oyeee, hali iliyozua kelele za kabla ya kuwaeleza kuwa alikuwa anawatania.
 
“Nawatania na nyie mnaitikia,” alihoji Lowassa.
 
BAADA YA KUWASILI UWANJANI
Sekunde chache kabla ya umati uliokuwa umefurika ulilipuka kwa shangwe huku wakiimba nyimbo za kusema Lowassa rais…Lowassa rais…Lowassa rais.
 
Shangwe hizo zilidumu kwa takriban dakika 10 huku Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, akijaribu kuwatuliza wananchi ili Lowassa  apande jukwaani kuzungumza nao, lakini ilichukua muda mrefu wananchi hao kunyamaza.
 
“Jamani najua mna mapenzi makubwa na mheshimiwa rais Lowassa, lakini mngenyamaza kidogo ili nimkaribishe hapa jukwaani azungumze nanyi kwa kuwa muda umeisha na tunataka kurudi Dar es Salaam kwa sababu usiku wa leo (jana) tuna kikao muhimu cha kupanga mikakati,” alisema.
 
FREDERICK SUMAYE 
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, alisema Tanzania ipo katika mfumo wa vyama vingi, lakini CCM imeteka nyara dhana hiyo na kufanya kama chama kimoja na ndiyo maana mtu akitoka CCM anasakamwa na kusemwa vibaya.
 
“Hata mimi pamoja na kutoka sitaogopa nitakuwa na Watanzania wanaotaka mabadiliko,” alisema.
 
Alisema CCM wamekuwa wakitumia mbinu kwamba wananchi wakichagua upinzani nchi itaingia katika vita.
 
 “Libya vurugu zilitokea kwa sababu chama tawala cha nchi hiyo hakikutaka chama kingine kitawale na CCM nao wanafanya hivyo,” alisema.
 
Alisema hali ya maisha imekuwa ngumu na umaskini umezama zaidi kwa wananchi licha ya ahadi ya Rais Jakaya Kikwete kwamba ataleta maisha bora kwa Watanzania, lakini ahadi hiyo imekuwa kinyume.
 
Alisema mgombea urais CCM Dk. Magufuli anasema akiingia madarakani rushwa ataikomesha, lakini serikali ilishindwa kukomesha suala hilo.
 
Alisema Dk. Magufuli anaahidi kuwa akiingia Ikulu atanyang’anya mashamba ya watu kwanza na kwamba Ukawa wakiingia Ikulu watawabana  walificha fedha nje wazirudishe.
 
Alisema kuna kashfa ya kusafirisha twiga hai kwenda nje, lakini serikali ya CCM hadi sasa haijaweka wazi ni akina nani waliohusika.
 
Sumaye alisema deni la taifa limefikia zaidi ya Sh. trilioni 35 ambazo zimefanya kila Mtanzania kudaiwa Sh. 800,000 na kama wananchi wataichagua tena CCM kuna hatari vitu vyao vya ndani vikauzwa ili kufidia deni hilo.
 
Kuhusu kashfa ya Richmond, alisema Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, ilieleza kuwa Lowassa hana hatia.
 
“Leo wanawatafuta akina Dk. Slaa ili wasema Lowassa, ahusike hivi dude hilo la Richmond rais alikuwa hajui, lakini leo kwa sababu ametoka CCM, Lowassa ndiye mtuhumiwa namba moja.
 
Alisema Sitta akiwa Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, aliapa kuwa fedha za kulipa Dowans hazitalipwa na kwamba zikilipwa atachia madaraka, lakini hadi sasa hajafanya hivyo na fedha hizo zimelipwa.
 
Alisema Dk. Slaa aliwatuhumu mafisadi 11 ambao wote wapo CCM, lakini leo Lowassa hayupo huko na katika kipindi ambacho hayupo kumefanyika ufisadi mwingi.
 
Katika hatua nyingine, Sumaye alimuweka katika wakati mgumu mgombea ubunge jimbo la Nzega kupitia CCM, Hussein Bashe, baada ya kueleza kuwa anampenda Lowassa na atampigia kura ya ndiyo.
 
 “Huyu mgombea ubunge CCM hapa Nzega si mnamjua alikuwa anampenda Lowassa na mpaka sasa, atampa kura Lowassa ila sasa amebaki katika gari bovu, lakini hatuna shida naye ila amebaki katika gari ambalo halifai,” alisema na kuongeza kuwa anatakiwa kujiunga na Ukawa.
 
LAWRENCE MASHA
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Laurence Masha, amesema yeye na viongozi wengine wamehama CCM kwa sababu chama hicho kimekosa mwelekeo kutokana na kutozingatia miiko.
 
Masha alisema  hivi sasa CCM kimebaki kuwa ni chama chenye nembo ya nyundo na jembe tu, lakini misingi yake yote imekufa na kuwataka wananchi kuichagua Ukawa ili kuleta mabadiliko.
 
UTATA UBUNGE NZEGA WAMALIZWA
Wakati huo huo, Sumaye alipata taabu kuwanadi wagombea ubunge na udiwani kutokana na jimbo la Nzega Mjini  kutokana na kuwapo makada wawili  wa Ukawa.
 
Sumaye baada ya kuwakaribisha wagombea hao jukwaani kuwanadi kwa wananchi, walijitokeza wote  wawili ambao ni Meza Leonard wa CUF na Charles Mabula wa Chadema.
 
Kabla ya kuwapa nafasi wagombea hao, Sumaye alisema kwa kuwa jimbo hili lina wagombea wawili, viongozi wa Ukawa watashughulikia suala hilo kumpata mmoja.
 
Hali hiyo ilimlazimisha Mwenyekiti Mbowe aliingilie kati na kuwaita wenyeviti wa CUF na Chadema wa wilaya hiyo waeleze kwanini jimbo hilo lina wagombea wawili.
 
Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Nzega, Jeremia Mwanamitumba, alisema  hakuna tatizo isipokuwa kilichotokea kila mmoja alikwenda kuchukua fomu katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
 
Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Nzega, Shehe Omary, alisema kilichojitokeza ni kila chama kutomwamini mwenzake, hali iliyosabaisha kila chama kwenda kuchukua fomu ya mgombea wake.
 
Baada ya maelezo hayo, Mbowe aliwapandisha jukwaani wagombea wote kujieleza na wa kwanza kuzungumza ni mgombea wa CUF ambaye alipata wakati mgumu kutoka kwa wananchi kupiga kelele wakati akijieleza.
Mgombea wa Chadema alipopanda  jukwaani, wananchi walimshangilia kwa muda wote.
 
Baadaye Mbowe aliwataka wananchi kupiga kura ya nani wanataka awe mgombea ubunge jimbo la Nzega Mjini na mgombea. Mgombea wa CUF alipigiwa kura na watu wasiozidi watano na wa Chadema alipigia kura na kundi kubwa, hivyo kutangazwa kuwa mgombea.
 
Mgombea wa CUF, Leonard alikubaliana na matokeo hayo na kumshika mkono mgombea wa Chadema, Mabula ikiwa ni ishara ya kukubaliana na maamuzi ya wananchi.
 
KUITEKA DAR LEO
Wakati huo huo, Lowassa leo anatarajiwa kuliteka Jiji la Dar es Salaam wakati atakapohamishia kampeni zake katika majimbo ya Kibamba na Kawe.
 
Kwa mujibu wa ratiba ya mgombea huyo, kesho Lowassa ataelekea Morogoro ambako alitoka mshindani wake, Dk. John Magufuli wa CCM.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment