dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, September 7, 2015

Kura zitapigwa hivi Oktoba 25




Dar es Salaam. Kampeni za Uchaguzi Mkuu zinaendelea mpaka Oktoba 24 zitakapohitimishwa. Kila mgombea anajaribu kuwashawishi wapigakura juu ya ilani ya chama chake, pia vipaumbele atakavyovitekeleza kwa miaka mitano ijayo ikiwa atachaguliwa kuliongoza taifa.
Pamoja na wawakilishi hao wa vyama vya siasa kuendelea kujinadi, kumekuwapo pia na kauli juu ya ulinzi wa kura kwa lengo la kujihakikishia kuwa hakutokei ulaghai wakati wa kuhesabu kura. Vyama vya upinzani vimekuwa vikiweka mikakati kwa kuandaa vijana watakaotekeleza jukumu hilo.
Mapema mwaka huu baada ya kuchaguliwa kukiongoza tena Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alizindua kikosi cha ulinzi maarufu kama Red Brigade kilichokuwa na askari 500 ‘watakaolinda’ kura kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC), Kailima Ramadhan anasema kuwa hakutakuwa na haja wala fursa ya kufanya hivyo kwa chama chochote kwenye uchaguzi wa mwaka huu, baada ya taratibu za uhesabuji kubadilika tofauti na ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita.
“Matokeo yote ambayo yameridhiwa na mawakala wa vyama husika yatabandikwa nje ya kila kituo na nakala kupelekwa kwa msimamizi wa uchaguzi wilayani kwa nafasi ya udiwani na ubunge wakati yale ya urais yatakuja makao makuu. Hakuna atakayeondoka na boksi la kura kabla kila alichopata mgombea kubandikwa kwenye ubao wa matangazo wa kituo husika,” anasema Ramadhan.
Mkurugenzi huyo anafafanua kuwa kwa miaka ya nyuma, utaratibu ulikuwa tofauti. Kilichokuwa kinafanyika ni kwamba wananchi walikuwa wakipigakura kwenye vituo vyao, kisha kuwekwa kwenye masanduku na kwenda kuhesabiwa sehemu tofauti.
Anaeleza kuwa kwenye kuhesabu kura siyo kila wakala alikuwa akihusishwa, isipokuwa wachache waliokuwa na dhamana ya kufanya hivyo.
Ramadhan anabainisha kuwa hapo ndipo malalamiko mengi yalikuwa yakianzia na kwamba NEC imeliona hilo na kulifanyia kazi ili kupunguza malalamiko kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Mabadiliko ya mfumo
“Mwaka huu kila kituo kitahesabu kura za wagombea wote wa udiwani na ubunge mbele ya mawakala walioteuliwa na vyama vinavyoshiriki uchaguzi. Matokeo yatakayoridhiwa na wawakilishi hao ndiyo yatakayotambuliwa. La muhimu inabidi wakubaliane wote kwa kauli moja.
Kama kutakuwapo atakayekuwa na shaka, anaruhusiwa kuripoti ili tume ifanye uchunguzi na kujiridhisha, kabla haijatoa uamuzi wa mwisho,” anabainisha Ramadhan.
Upigaji kura utakavyokuwa
Mkurugenzi huyo wa NEC anaeleza kuwa tayari tume yake imeanza kuelimisha wananchi wanaotumia mtandao wa intaneti kuhusu taratibu zitakavyokuwa siku ya upigaji kura, baada ya kuainisha mlolongo wa matukio ambayo kila mwananchi atatakiwa kuyafuata kabla hajamchagua anayempa dhamana ya uongozi kwa miaka mitano ijayo.
Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa NEC, Dk Sisti Cariah anauhakikishia umma akisema: “Kila Mtanzania aliyejiandikisha na atakayejitokeza kupiga kura, atapiga kura na kwamba jitihada za kuingiza taarifa za watu wote wanaostahili kwenye kumbukumbu za tume hiyo zinaendelea kabla mpigakura hajakabidhiwa karatasi tatu za kura.
Anaeleza kuwa hakuna taarifa itakayopotea kwani zinahifadhiwa eneo maalumu na kwamba hata janga lolote likitokea zitaendelea kuwa salama ili kutoathiri Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
“Tunavyo vituo vitatu vya kutunzia taarifa (data centers). Vimewekwa maeneo tofauti kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa takwimu zimehifadhika hata kama kimoja kati yao kitapata hitilafu itakayosababisha kukosekana kwa kinachohitajika kwa wakati husika. Janga kama moto au mafuriko yakitokea na kuathiri kituo kimoja, viwili vilivyobaki vitatumika,” alisema Dk Cariah wakati wa ziara ya waandishi wa habari kwenye kituo cha hifadhi kilichoko Bohari Kuu ya Serikali.
Waliojiandikisha mara mbili kupiga kura
Dk Cariah anafafanua kwamba hata watu 52,078 waliobainika kujiandikisha zaidi ya mara moja, wataruhusiwa kupigakura kwenye kituo kimoja kati ya walivyoenda kujiandikisha na kusisitiza kwamba kila mwananchi mwenye sifa, atashiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Alieleza pia kuwa upigaji kura utafanyika kuanzia saa 2:00 asubuhi mpaka saa 10:00 alasiri na kudokeza kwamba muda huo wa mwisho utakapofika, askari polisi atasimama nyuma ya mtu wa mwisho aliyepo kwenye foleni na kwenda naye mpaka atakapopiga kura yake na kuondoka.
“Baada ya hapo watabaki watu wanaoruhusiwa tu kwenye chumba cha kupigia kura. Watazihesabu na kisha kubandika matokeo nje ya kituo husika. Upigaji hautokuwa wa kielektroniki kama wengi wanavyodhani. Itakuwa kawaida tu,” alisema Dk Cariah.
Vituo na utangazaji wa matokeo
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva anasema kwamba ili kuondoa uwezekano wa kufanyika kwa hujuma za aina yoyote, uchaguzi wa mwaka huu umeratibiwa kwa namna ambayo utakuwa wa wazi zaidi ili kuondoa shaka ya aina yoyote.
“Kutakuwa na vituo vingi zaidi mwaka huu tofauti na ilivyokuwa 2010. Hii ni kutokana na kubadilika kwa mipaka,” anasema Jaji Lubuva.
Kituo kimoja watu 450
Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, wakati wa uandikishaji vilitumika vituo 37, 848 lakini wakati wa upigaji kura vitaongezeka ili wote waliojiandikisha kupata fursa ya kupiga kura kwa sababu tofauti na uandikishaji, zoezi la kupiga kura ni la siku moja tu tena kwa saa zisizozidi tisa.
Anasema ongezeko la vituo hivyo linalenga kuwahudumia Watanzania wote 23, 782, 558 waliojiandikisha kushiriki uchaguzi wa mwaka huu akibainisha kuwa kwa mkakati ulioandaliwa, kila kituo kitatakiwa kuhudumia wapigakura wasiozidi 450 kwa saa tisa za siku hiyo, zitakazotumika kuamua mustakabali wa uongozi wa Tanzania kwa miaka mitano ijayo.
“Baada ya kupiga kura na matokeo kubandikwa, litabaki jukumu la mamlaka husika kutangaza mshindi.” “NEC itatangaza matokeo ya rais, wakati wakurugenzi wa halmashauri watashughulika na matokeo ya ubunge pamoja na udiwani,” anasema Jaji Lubuva
Ili kuepusha uwezekano wa kuwapo kwa madai ya matokeo kuchezewa, Jaji Lubuva anasisitiza kwamba tume imejipanga vilivyo kumtangaza mshindi ndani ya muda uliopangwa kisheria.
Anaendelea kusema: “Sheria inataka mshindi wa urais atangazwe ndani ya siku saba, baada ya uchaguzi, lakini sisi tumepanga kutangaza matokeo ndani ya siku tatu hadi nne, ili taratibu nyingine ziendelee na wananchi waachane na habari za uchaguzi na kuelekeza nguvu zao kwenye kulijenga taifa kimaendeleo.”
Lubuva anatoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 25 ili kila mmoja afanye uamuzi utakaochangia kupatikana kwa viongozi bora.
Anakumbusha kwamba mwaka 2010 waliojiandikisha walikuwa 20 milioni, lakini waliojitokeza kupigakura walikuwa milioni 10 pekee, akisema kuwa hilo si jambo zuri kwa utekelezaji wa demokrasia nchini.
“Kwa uhakika mpigakura hatatumia muda mwingi kwenye vituo vya kupigia kura, ni suala la kila Mtanzania kuhakikisha anatenga muda wake kwa kuandaa ratiba itakayompa fursa ya kutumia dakika chache kushiriki Uchaguzi Mkuu mwaka huu na kuchangia mabadiliko ya uongozi kutoka kwa rais anayemaliza muda wake na kuusimika uongozi mpya wa awamu ya tano,” anahitimisha Jaji Lubuva.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unafanyika wakati taifa likijiandaa kuondoka kwenye kundi la nchi maskini duniani ili kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, hali inayoongeza umuhimu wa ushiriki wa wananchi kwenye hatua hiyo ya demokrasia.
Ni muhimu na haki ya kila aliyejiandikisha kujitokeza kumchagua ampendaye kwa Tanzania ya kesho unayoitarajia.
/Mwananchi.

No comments :

Post a Comment