Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, September 12, 2015

Maalim Seif aahidi mafuta, gesi ndani ya siku 100 Zanzibar


Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Hamad
Zanzibar. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa siku 100 za uongozi wake, atahakikisha anaingia mikataba na kampuni za mafuta na gesi asilia ili zianze uchimbaji katika ardhi ya Zanzibar.
Maalim Seif alisema hayo juzi kwenye viwanja vya Tibirinzi mkoani Kusini Pemba alipokuwa akizungumza na wananchi na wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa.
Aliwaomba wananchi wa Unguja na Pemba wampe ridhaa ya kuongoza visiwa vya Zanzibar ili aweze kuwaletea maendeleo na kuahidi kufanya mabadiliko hayo kwenye sekta ya mafuta na gesi ndani ya siku 100.
Alisema kazi ya uongozi ni kuchapa kazi na kuwa na dhamira ya kweli ya kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kuweka misingi ya utawala bora, haki na demokrasia.
Alisema kitu hicho kinawezekana na kikiwezekana, wananchi watakuwa na moyo wa kujitolea katika kufanya kazi za kuendeleza nchi yao.
“Mimi naamini hakuna linaloshindikana kwa uwezo wa mwenyezi Mungu. Tabia ya wananchi wa visiwani wanakuwa na uchungu na wivu na nchi yao, naamini hakuna Mzanzibari asiyeipenda nchi yake, naamini na hiyo ndio tabia ya wananchi wa visiwani ambao wanakuwa na wivu kama mume kwa mkewe,” alisema Maalim huku akishangiliwa kwa kutaja wivu wa mume na mke.
Maalim Seif alisema CCM wamewasaliti Wazanzibari kwa kushindwa kuwatetea ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa mchakato wa kuunda Katiba mpya.
Alisema walipokwenda Dodoma walisahau kero na shida za Wazanzibari walizozipata kwa muda wa miaka 50.
“CCM kwa kweli walitusaliti Wazanzibari kwa sababu wamekwenda kutengeneza Katiba Mpya lakini kufika kule wameufyata kabisaaaa! Sawa sawa…badala ya kuwatetea Wazanzibari wamekwenda kusahau yote na wakaungana na wale watu wasioitakia mema Zanzibar wakaupitisha mfumo wa serikali mbili ambao ni mbaya,” alisema Seif, ambaye aliwahi kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Mkuu huyo wa zamani wa Idara ya Uchumi na Mipango ya CCM alisema akipewa nafasi ya kuwa Rais, ataweka misingi ya utawala bora, atapambana na rushwa kwa kuwadhibiti na kuwashughulikia wala rushwa, kuinua uchumi kwa kushughulikia suala la bandari huru ili kuinua wafanyabiashara wafanye biashara zao kwa uhuru na urahisi zaidi kuliko walivyo sasa.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mansoor Yussuf Himid, ambaye alikuwa mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki (CCM) na ambaye hivi sasa ni mshauri wa Maalim Seif, alisema Wazanzibari wana hamu ya kupata kiongozi ambaye atajali utu, haki na usawa huku akizingatia umoja, upendo na mshikamano.
“Tunamtaka kiongozi ambaye anajua na kuheshimu utu wa mtu atakayewaunganisha Wazanzibari wote bila ya kujali dini, kabila wala rangi ambaye jambo la kuwaunganisha watu ni lazima kwake,” alisema.
“Na mimi naamini ndani ya nafsi yangu kwamba mtu huyo si mwingine zaidi ya Maalim Seif kwa hivyo namuombea kura zenu mumpe ridhaa ili atuongoze katika usawa.”
Alisema Zanzibar pamoja na utajiri wake hakuna ajira zaidi ya zile za mahoteli tu na za vikosi vya SMZ ambazo hutolewa kila inapokaribia uchaguzi, halafu ukimalizika uchaguzi vijana hao hutupwa.
“Ajira tulizo nazo ni mahotelini tu, sasa vijana wangapi watafanya kazi hotelini? Kwani tuna hoteli ngapi?” alihoji Mansoor.
/Mwananchi.

No comments :

Post a Comment