Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, September 2, 2015

Magufuli, Lowassa wapishana Ruvuma.

Wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na John Pombe Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jana waligongana mkoani Ruvuma huku wakijinadi kwa kishindo kwa nia ya kushawishi wananchi wawachague katika uchaguzi mkuu wa mwezi ujao.
 
Mbali na wagombea hao wanaovutia umati katika mikutano yao ya kampeni, mgombea mwenza wa Chadema, Juma Duni Haji, yuko mkoani Lindi ambao ni moja ya mikoa ya Kanda ya Kusini, kumnadi Lowassa, yeye (Duni) na wagombea ubunge na udiwani wa Ukawa.
 
Mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan, anaendelea kuchanja mbuga mkoani Dodoma, akielekeza mashambulizi yake kutokea eneo la kaskazini mwa Tanzania kuelekea katika Kanda ya Kati.
 
Katika mikutano yao ya jana, Magufuli alikuwa kwenye Jimbo la Namtumbo, mkoani Ruvuma huku Lowassa akiwa pia mkoani humo, katika Jimbo la Peramiho.  
 
Awali, baada ya kuzindua kampeni za chama chake kwa kishindo jijini Dar es Salaam, Magufuli alielekea mkoani Katavi na kufanya mikutano ya kampeni katika majimbo ya Mpanda Mjini, Mpanda Vijijini na Mlele. Kutoka hapo, alikwenda mkoani Rukwa na kumwaga sera zake katika majimbo ya Nkasi Kaskazini, Nkasi Kusini, Sumbawanga Mjini, Kwela na  Kalambo.Safari za kampeni ya Magufuli ziliendelea katika mkoa wa Mbeya ambako alihutubia wananchi kwenye majimbo ya Momba, Ileje, Chunya, Mbalizi, Vwawa, Rugwe, Kyela, Mbeya Mjini, Mbeya Vijijini, Busokelo, Mbozi, Tunduma, Lupa na Songwe. 
 
Katika mkoa wa Njombe, alifanya mikutano katika majimbo ya Njombe Kaskazini, Makete, Njombe Kusini, Ludewa na Wang’ingombe. 
 
Kabla ya kufika Namtumbo jana, alipitia katika majimbo ya Madaba, Mbinga, Nyasa, Peramiho, Songea Mjini, Songea Vijijini, Namtumbo, Tunduru na wakati tunakwenda mitamboni jana jioni, Mgombea huyo wa CCM alianza kampeni zake mkoani  Mtwara.
 
Safari ya mgombea wake mwenza, Samia, ilianzia mkoani Kilimanjaro katika majimbo ya Mwanga, Same Mashariki, Same Magharibi, Vunjo, Moshi Vijijini na Moshi Mjini. 
 
Alipoingia mkoani Arusha, aliendesha kampeni za chama chake katika majimbo ya Longido, Monduli, Karatu, Arumeru Mashariki na Arumeru Magharibi, kabla hajatua mkoani Manyara alikohutubia kwenye majimbo ya Mbuku, Babati Mjini, Babati Vijijini na Hanan’g.
 
Mkoani  Singida, Samia alihutubia katika majimbo ya Singida Mashariki, Iramba, Manyoni na Singida Mjini na baadaye alielekea Dodoma ambako kabla ya kuhutubia katika Jimbo la Kibakwe jana, alihutubia pia kwenye majimbo ya Dodoma Mjini, Kongwa, Chilonwa, Mpwapwa, Mtera na Bahi.
 
Lowassa na timu yake walipomaliza kuzindua kampeni zao zilizovutia umati jijini Dar es Salaam Jumapili, alielekea Iringa alikofanya kampeni katika majimbo ya Mufindi, Kilolo, na Iringa Mjini.
 
Baadaye alielekea mkoani Njombe na kunadi sera zake Makambako na Jimbo la Njombe Mjini. Kabla ya kuhutubia kwenye Jimbo la Songea Mjini mkoani Ruvuma jana, Lowassa alifanya kampeni zake katika jimbo la Madaba mkoani humo.
 
 Mgombea mwenza wa Lowassa, Duni, alianzia kampeni zake Dar es Salaam na kuelekea mkoani Mtwara alikohutubia katika majimbo ya Newala, Mtwara Mjini, Lulindi, Nanyumbu na Masasi. 
 
Jana alikuwa kwenye Jimbo la Lindi Mjini mkoani Lindi, akitokea katika majimbo ya Liwale, Nachingwea na Ruangwa.
 
LOWASSA WA UKAWA
Akijinadi kwa wananchi katika jimbo la Madaba Wilaya ya Songea Vijijini mkoani Ruvuma jana, Lowassa alisema iwapo wananchi watampa ridhaa, serikali yake itahakikisha haikopi mazao kwa wakulima.
 
Lowassa alitoa kauli hiyo wakati akijibu malalamiko ya wananchi kuwa serikali imekopa mazao yao na kuwasababishia maisha magumu kwa kukosa fedha.
 
“CCM waache kelele wajibu hoja kwa nini wananchi ni maskini, sipendi umaskini kama wana hoja wajibu,” alisisitiza  Lowassa huku akishangiliwa.
 
Aliwataka wana-CCM ambao bado wanang’ang’ania kuendelea kubaki ndani ya chama hicho wahame na kumchagua kwa sababu nyumba yao inaungua moto.
 
Alisema CCM lazima watambue kuwa wananchi wamechoka kudanganywa na kupewa ahadi zisizotekelezeka na kwamba mwaka 2015 ni  lazima mabadiliko yafanyike.
 
Kuhusu kupiga kura, aliwahadharisha wananchi kuwa makini na CCM kwa madai kuwa baadhi ya makada wake ni wataalam wa wizi wa kura.
 
AWAPA NAFASI WANANCHI
Tofauti na maeneo mengine, Lowassa aliendesha kampeni kwa kuwapa nafasi wananchi waliohudhuria mkutano huo kuelezea kero zinazowakabili katika eneo lao.
 
Wakazi wa Kijiji cha Madaba waliopata fursa hiyo, walimwelezea Lowassa kuwa wanakabiliwa na tatizo la uporaji wa ardhi unaofanywa na baadhi ya viongozi wa vijiji, ukosefu wa maji na ushuru wa mazao.
 
KUFUMUA MIKATABA YA MADINI
Lowassa, alisema kama atakuwa rais wa awamu ya tano, mikataba yote ya madini nchini itapitiwa upya.
Kauli hiyo aliitoa kwenye mkutano wa kampeni katika jimbo la Songea Mjini katika uwanja wa Shule ya Msingi Matalawe.
 
Alisema lengo la kuipitia mikataba hiyo siyo kuwafukuza wawekezaji bali kutaka kuona madini hayo yanawanufaisha wananchi.
 
Pia, alisema deni la Taifa litahakikiwa ili kubaini fedha hizo zilitumikaje.
 
Kuhusu kilimo, alisema wakulima wataruhusiwa kuuza mazao yao yakiwamo mahindi sehemu yoyote na kwamba kazi ya serikali haitakuwa kununua mahindi.
 
“Wakulima wataruhusiwa kuuza mahindi kokote, akitaka kuuza Kenya au DRC ni yeye mwenyewe,” alisema.
 
VITUKO
Wakati wa mkutano huo, baadhi ya vijana walikuwa wamebeba mfano wa jeneza likiwa na maandishi yanayosomeka Balali na Babu Seya waachiwe huru.
 
Aidha, jeneza hilo lilikuwa na maandishi ya CCM kuzaliwa mwaka 1961 na kuzikwa 25/10/2015.
Kulikuwa na mabango yaliyokuwa na mabango mbalimbali likiwamo ‘Lowassa zuia wizi wa makaa ya mawe, tuletee umeme wa uhakika.
 
SUMAYE 
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, akisema kama kipindi cha miaka mitano kikimaliza bila ya Lowassa kutekeleza ahadi zake, wananchi warudi CCM.
 
“Ikiisha miaka mitano anayoyasema Lowassa kama hayajatekeleza ahadi si mtarudi CCM, lakini nawahakikishia hamtarudi huko,” alisema.
 
 
HAMISI MGEJA 
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, alidai kuwa ahadi ya Sh. milioni 50 kwa kila kijiji inayotolewa na mgombea urais wa chama tawala, Dk. John Magufuli na mgombea mwenza wake, Samia Suluhu haiwezi kutekelezeka.
 
Akimnadi Lowassa katika mkutano huo,  Mgeja,  ambaye alijiunga na Chadema hivi karibuni, alisema ahadi hiyo haiwezi kutekelezeka kwa zaidi vijiji ya 13,000 kwa Sh. bilioni 600.
 
“Tunachojiuliza watazipataje hizo fedha wakati  hata madeni ya walimu hawajalipa.. huu ni uongo wa mchana,” alisema.
 
Alisema tatizo linaloitafuna CCM ni mfumo mbovu wa rais wa nchi kuwa mwenyekiti wa chama ambao unasababisha ashindwe kuhojiwa mambo yanapokwenda kombo ndani ya chama na serikali.
 
Mgeja alisema viongozi wa CCM ni lazima watambue kuwa Tanzania na ikulu siyo mali ya chama hicho na kwamba hatma ya Tanzania kwa sasa ipo mikononi mwa wananchi wenyewe ambao wameamua kufanya mabadiliko baada ya kuchoshwa nacho.
 
LAWRENCE MASHA
Kwa upande wake, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, alisema si kosa kuhama CCM, bali ni kosa kushindwa kulala usingizi kwa sababu ya kujidanganya mwenyewe.
 
“Ni kosa pale unapojidanganya wewe na familia, tulikuwa CCM, lakini dhamira ilikuwa inatusuta kwa sababu ni chama ambacho hakiwezi kuleta mabadiliko,” alisema.
 
Masha ambaye amehama CCM na kujiunga Chadema, aliwaambia vijana kuwa mwaka 2015 ni mwaka wa kufanya mabadiliko kwa kuchagua Ukawa na siyo CCM kwa madai kuwa watu wake ni wale wale.
 
MAGUFULI WA CCM
Wakati huo huo, mgombea ubunge wa jimbo la Namtumbo, Edwin Ngonyani, jana alitoa mpya, baada ya kupiga magoti wakati Magufuli akimnadi kwa wananchi. 
 
 Dk. Magufuli baada ya kumaliza kumwaga sera na kujinadi kwa wakazi wa Namtumbo, alianza  kumuombea kura kwa wananchi huku mgombea huyo akipiga magoti.
 
“Simama... nakukabidhi ilani ya CCM, kitabu hiki kimebeba mambo mengi sana, kisome, kichambue na uwaeleze wananchi... ukawe mtumishi wa watu, ufanye kazi sana, Namtumbo iwe utumbo uliokomaa, mimi si mnafiki bali mkweli daima, simamia Ilani huku ukimtanguliza Mungu,” alisema.
 
Awali, Magufuli aliwaomba wakazi hao kuirejesha CCM madarakani kwa kuwa ina mahusiano mazuri na wahisani wanaotoa misaada mingi nchini.
 
“Barabara ya Namtumbo hadi Tunduru hadi Mtambaswala inajengwa na makandarasi wanane kwa mkopo wa Jica (Shirika la Kimaitaifa la Maendeleo Japan) na Benki ya Maendeleo ya Afrika, wametupa mkopo kwa sababu wanatuamini, msichague mtu asiye na tamaa ili wafadhili wasije kukimbilia katikati,” alisema.
 
Magufuli aliendelea kuahidi kuwa serikali yake itaendeleleza uhusiano mzuri kwa nchi jirani, Afrika na Ulaya.
Alisema uhusiano huo umesababisha Tanzania kuaminiwa na ndiyo maana serikali ya Marekani kupitia Malengo ya Millenia (MCC) imejenga barabara ya Songea hadi Namtumbo.
 
Alisema uhusiano huo utasaidia miradi yote iliyoanza kutekelezwa inaendelea na kutumika vizuri katika serikali yake kwa kuwa haitakuwa na mafisadi.
 
MADINI
Alisema atahakikisha serikali yake inaendeleza madini ya Uranium ili yawanufaishe wananchi wote, kuanzia kwenye maeneo yanakochimbwa.
 
MISHAHARA
Aliendelea kuahidi kuboresha maslahi ya  watumishi wa umma na kuwahimiza kufanya kazi kwa bidii.
 
Vilevile, aliwataka Watanzania kukiamini CCM na yeye kutokana na kuwafanyia mengi akiwa waziri.
 
“Sasa nitakuwa rais ambaye naagiza Mawaziri kufanya kazi na watatakiwa kufanya kazi kweli kweli usiku na mchana,” alisema.
 
AKAGUA UJENZI WA BARABARA
Akiwa katika kijiji cha Hulia, Magufuli alishiriki kutengeneza barabara ya Matemanga hadi Hulia yenye urefu wa kilomita 68.2 kwa dakika 10 kisha kuzungumza na makandarasi.
 
TUNDURU
Akiwa Tunduru alirejea ahadi zake za kuboresha huduma za jamii, kusisitiza serikali yake haitakubali ubaguzi na kufanya kazi bila kujali tofauti za vyama vya siasa nchini kwa maslahi ya wananchi.
 
Pia, aliahidi kusimamia bei ya korosho ili wakulima wanufauke na zao hilo.
 
Akiwa Nanyumbu mkoani Mtwara, Magufuli aliahidi kujenga kiwanda cha kubangua korosho ili ziwe na ubora na maganda yake kutumika kutengeza kemikali na kunufaisha wakulima kwa kujiongezea kipato.
 
 Imeandikwa na Moshi Lusonzo (Dar es Salaam), Salome Kitomari na Thobias Mwanakatwe (Ruvuma), Richard Makore (Dodoma) na Suleiman Mpochi (Lindi)   
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment