Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kupitia hotuba mbalimbali za wagombea hao tangu kuanza kwa kampeni Agosti 24 (kwa CCM) na Agosti 29 kwa mgombea wa Chadema anayewakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), unaonyesha kuwa wote wawili watakuwa wakali na kuongeza umakini zaidi katika kuhakikisha kuwa mawaziri wanaosimamia wizara zinazobeba hoja zao kuu katika kampeni wanatimiza malengo. Mbali na Chadema, Ukawa huundwa pia na Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD.
Katika uchunguzi huo ambao pia umehusisha rejea za ilani za CCM na Ukawa kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka huu, inaonekana kuwa Magufuli amepania kufanya mambo mengi yenye nia ya kuwakwamua Watanzania kutoka walipo sasa katika kila nyanja. Lowassa anayo mengi pia aliyoahidi hadi sasa kupitia ilani ya Chadema na Ukawa na pia mengineyo yatokanayo na maono yake binafsi.
Hata hivyo, uchunguzi zaidi unaonyesha kuwa wote wawili wamejikita katika kuzungumzia namna watakavyoleata mabadiliko kwenye maeneo ya afya, elimu, ujenzi, maji, nishati na madini, uchumi na pia utawala wa sheria.
Kadhalika, inafahamika kuwa wote wawili wamejijengea rekodi nzuri katika kuongoza wizara mbalimbali.
Lowassa aliwahi kujijengea heshima kubwa kwa nyakati tofauti alipokuwa katika wizara inayoshughulikia ardhi na baadaye maji na mifugo huku Dk. Magufuli akiacha kumbukumbu nzuri za uchapaji kazi makini wakati akisimimamia mifugo na uvuvi na hata sasa anaposhikilia nafasi ya kuwa Waziri wa Ujenzi. Zaidi ya yote, Lowassa ameshatangaza kuwa na serikali itakayokuwa na mawaziri watakaofanya kazi kwa 'spidi 120'. Dk. Magufuli ameshasema vilevile kuwa kamwe hatakubali kuwa na waziri 'legelege' na kwamba, ni bora wale wote atakaowateua kwa nafasi za uwaziri wakatae mapema wakijiona kuwa ni legelege kabla hawajaumbuka kwa kufutwa kazi kungali mapema.
Kwa sababu hiyo, Nipashe imebaini kuwa ikitokea mmoja wao akawa mshindi wa nafasi ya urais, mawaziri takriban nane watakuwa na kibarua kizito katika kuhakikisha kuwa wizara zao zinatimiza malengo watakayopewa.
1. WAZIRI WA MAJI
Hakika, yeyote atyakayepewa kuongoza wizara hii atakuwa na kibarua kigumu. Akilegalega, aweza akajikuta aking'olewa madarakani ndani ya siku chache tu baada ya uteuzi. Hili linatokana na ukweli kuwa Dk. Magufuli na Lowassa wamekuwa wakiahidi makubwa kuhusiana na maji katika kampeni zao.
Magufuli amekuwa akisema wazi kuwa serikali yake haitaruhusu matumizi mabaya ya rasilimali fedha kwenye Wizara ya Maji na kwa kuanzia, amesema atafutilia mbali sherehe na maadhimisho mbalimbali ambavyo kwa pamoja huteketeza mamilioni ya fedha kila mwaka. Magufuli anazitaja baadhi ya shughuli atakazozifuta ili kutoa fursa ya kushughulikia kwa dhati matatizo ya maji ni 'Maadhimisho ya Wiki ya Maji' pamoja na semina na makongamano kuhusu maji. Badala yake, amesema akishazuia shughuli hizo anazoita kuwa ni za ulaji na tena zisizokuwa na faida kwa wananchi ambao hawapati maji, serikali yake itaelekeza nguvu katika uchimbaji wa visima na pia kusambaza huduma ya maji kwa wananchi.
Lowassa anaahidi kuwapatia maji safi na salama wananchi wa maeneo yote nchini, akiahidi kuanza kuhakikisha kuwa wananchi wanatunza na kulinda vyanzo vya maji, kuweka mazingira rafiki na yatakayowahakikishia maji Watanzania walio wengi. Kadhalika, timu ya kampeni ya Lowassa imekuwa ikikumbushia mara kadhaa juu ya namna alivyosimamia maji kwa umakini wakati akiwa waziri kiasi cha kuvunja kwa mafanikio makubwa mkataba na kampuni moja ya kigeni uliokuwa ukiliumiza taifa badala ya kuwaneemesha kwa maji wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
2. WAZIRI WA UJENZI
Hili ni eneo analolijua sana Magufuli na hata sasa angali akiongoza Wizara ya Ujenzi. Kote anakopita, Magufuli amekuwa akiahidi kuimarisha miundombinu ya barabara, na hasa zile za kiwango cha lami.
Kadhalika, Ilani ya CCM imeanisha barabara 35 zenye urefu wa kilomita 4,190.3 kujengwa, zikiwamo zilizopo katika hatua mbalimbali za ujenzi wa kiwango cha lami, huku barabara 42 zenye urefu wa kilomita 5,807.1 zikiwa zimefanyiwa upembuzi na usanifu na baadhi ya maeneo ujenzi kwa kiwango cha lami unaendelea.
Pia yametajwa madaraja kumi ya Kilombero, Mwatisi, Malagalasi, Kigamboni, Nangoo, Ruhekei na Mbutu, Rusumo, Mabatini, Sibiti, Ruhuhu na Kavuu.
“Nawahakikishia mkinichagua nitatandaza lami kwenye barabara kuu, wilaya na mitaa, Waziri nitakayemteua ni lazima afanye kazi kushinda nilivyofanya mimi... akishindwa kufikia lengo nitamuondoa," amesema Magufuli katika moja ya mikutano yake ya kampeni.
Mgombea wa Ukawa, Lowassa, ameahidi kujenga barabara kwa kiwango cha lami, changarawe na kwa viwango vinavyotakiwa ili kurahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi. Kadhalika, amezungumzia pia dhamira ya serikali atakayoiongoza kumaliza kero ya msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam, njia mojawapo ikiwa ni kuwekeza zaidi katika barabara.
3. WAZIRI WA AFYA
Waziri mwingine atakayekuwa na kazi ngumu ni Waziri wa Afya. Serikali ya Magufuli imeahidi kujenga zahanati kila kijiji, vituo vya afya kila kata, hospitali za wilaya kwa kila wilaya na Hospitali za Rufaa kwa kila mkoa.
Pia kuhakikisha kuwa dawa zinapatikana kwa kuwa imezoeleka wananchi kwenda kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali na kuishiwa kupewa cheti pekee na kutakiwa kwenda kununua dawa kwenye maduka binafsi ambayo ni mali ya watumishi wa sekta ya afya.
“Najua hospitali yenu hapa ina shida ya dawa... sasa nitakayemteua kuwa Waziri wa Afya halafu hospitali zikose dawa (nchini) sitamchekea. Ataondoka siku hiyo hiyo. Nipeni kura nyingi niwe rais nifanye kazi ya kusimamia rasilimali za Watanzania,” amesema na kuibua shangwe kubwa wakati akiwahutubia wananchi wa Makambako mkoani Njombe.
Lowassa ameahidi kuwa akichaguliwa na kuingia madarakani atahakikisha kuwa Watanzania wengi zaidi wanapata nafasi ya kujiunga na bima za afya za malipo nafuu, kuimarisha afya ya msingi pamoja na kinga na kuendeleza programu mbalimbali za afya hata baada ya wafadhili kuondoka.
Lowassa anaongeza kuwa serikali yake itahakikisha kuna uwiano na upatikanaji wa watumishi wa afya katika kada mbalimbali ili kuleta tija na huduma stahiki ikiwa ni pamoja na kusomesa kwa gharama ya serikali wataalamu bobezi (specialists) katika fani mbalimbali za afya.
Ameahidi vilevile kuwa serikali yake itawalipa posho za kujikimu wataalamu walio mafunzoni kwa vitendo ili kuwavutia na kuhakikisha kuwa mwishowe wanabaki katika sekta ya afya na kuhakikisha wananchi wengi wanapata huduma kwa haraka.
Lowassa amesema kwa kushirikiana na sekta binafsi, ataimarisha miundombinu ya afya ikiwa ni pamoja na kujenga hospitali za kisasa na kuboresha mifumo ya rufaa ili kusogeza huduma za afya karibu na jamii, kuanzisha utalii wa huduma za afya na pia kuepukana na tiba za nje ya nchi.
Kadhalika, akiwa katika Jimbo la Bumbuli jana, Lowassa aliahidi kumaliza tatizo la ukosefu wa dawa kwenye hospitali za serikali ndani ya siku 100 baada ya kushinda na kuapishwa kuwa rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
4. WAZIRI WA ELIMU
Waziri katika eneo hili atakuwa na kazi kubwa ikiwa urais utatwaliwa na Magufuli au Lowassa. Ni kwa sababu wote wawili wamekuwa wakitumia ajenda hii kuvutia wapiga kura wao. Magufuli kupitia CCM amesema kuwa atafuta karo kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi kidato cha nne na kusimamia ubora wa taaluma inayotolewa kwa kuhakikisha majengo muhimu na maabara zenye vifaa zinakuwapo. Hivi sasa, ada ni Sh 20,000 kwa shule za sekondari ya kutwa, Sh. 70,000 kwa sekondari za bweni na pia kuna rundo la michango ambayo ukubwa wake hutokana na aina ya shule na mahala ilipo.
"Nitakuwa mkali na nitafanya kazi kwa karibu na mawaziri wangu. Sitataka njoo kesho au bla bla nyinginezo," alisema Magufuli katika moja ya mikutano yake.
Serikali itakayoundwa na Lowassa wa Ukawa imeahidi kutoa elimu bure pia, lakini kuanzia chekechea hadi chuo kikuu. Inadai kuwa hakuna Mtanzania atakayeachwa nyuma na pia itaanzishwa Tume au Baraza la Taifa la Ushauri wa Elimu, lengo likiwa ni kujumuisha wadau wote kwa nia ya kuimarisha elimu ya sekondari, teknolojia, ustadi na ufundi na kwamba, elimu iwe itakayowajengea uwezo wahitimu ili kujiajiri kushindana vilivyo katika soko la ajira.
“Iwapo mtanichagua tutaimarisha vyuo vya ufundi stadi ili kuandaa vijana kuweza kujiajiri, kubadilisha malengo ya Jeshi la Kujenga Taifa ili lijikite katika kutoa mafunzo ya ufundi na uzalendo, kuimarisha miundombinu ya elimu ikiwa ni pamoja na shule za kata, pamoja na kusimamia ubora wa viwango vya elimu,” Lowassa amesema katika moja ya mikutano yake.
Lowassa pia ameahidi (akiwa Bumbuli jana) kuwa akishinda, atamaliza kero zitokanazo na malimbikozo ya madai ya walimu ndani ya siku 100 baada ya kuapishwa.
5. WAZIRI WA KAZI, AJIRA
Waziri mwingine atakayekuwa na kazi ya ziada kwa Magufuli na Lowassa ni Waziri wa Kazi na Ajira. Ni kwa sababu wote wawili wamekuwa wakiwaahidi wananchi juu ya kuhakikisha kuwa wanaongeza fursa za ajira nchini na mwishowe kupunguza tatizo hilo.
Magufuli amekuwa akisisitiza kuwa ataimarisha viwanda katika kila mkoa ili kutoa ufumbuzi kwa tatizo la kazi na ajira na kwamba, atahakikisha vilevile kuwa mishahara ya watumishi wa umma wakiwamo walimu na madaktari inaboreshwa. Kadhalika, Magufuli anayetumia kauli mbiu ya 'hapa kazi tu' amekuwa akiahidi kuwashughulikia watumishi wote wa umma wanaoendekeza uvivu. Yote haya ni majukumu yaliyo chini ya Wizara ya Kazi, kwa kushirikiana na Wizara ya Utumishi na pia Wizara ya Viwanda.
Lowassa amekuwa akisisitiza pia suala la ajira kwa vijana, ambalo kwa muda mrefu amelitaja kuwa ni kama 'bomu la kutegwa' linalosubiri wakati wake ufike ili kulipuka. Miongoni mwa mikakati ya Lowassa katika kukabiliana na tatizo hili ni kuongeza ajira kupitia viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ikiwa ni pamoja na kukaribisha wawekezaji wengi na pia kuwa na matumizi sahihi ya rasilimali ya gesi iliyogundulika kusini mwa nchi.
Ni wazi kwamba yeyote atakayepewa jukumu la kuongoza wizara hii chini ya Lowassa, atalazimika kufanya kazi ya ziada ili kutimiza malengo yatokanayo na ahadi ya muda mrefu ya 'bosi' wake kwani vinginevyo, kibarua chake kitaota mbawa kungali asubuhi.
6. WAZIRI WA NISHATI NA MADINI
Dk. Magufuli haachi kuzungumzia eneo hili. Ni kwa sababu limo katika ilani za chama chake ambacho kinaeleza wazi kuwa lengo kuu ni kuhakikisha kuwa vijiji vyote vinafikiwa na umeme. Kupitia miradi ya usambazaji wa umeme vijijini, Magufuli amekuwa akisisitiza kuwa wananchi wengi zaidi watapata nishati hiyo na mwishowe kuongeza kasi ya maendeleo. Ni wazi kuwa ulegelege wowote kwa mtu atakayepewa dhamana na Magufuli kuongoza wizara hii, atajikuta akiondolewa mara moja kwani ni kinyume cha ahadi za mgombea huyo na pia CCM ambayo hadi sasa imefanikisha miradi mingi ya umeme kwa mafanikio.
Katika eneo hili, Lowassa anayeongozwa na kauli mbiu yake ya 'mabadiliko' amekuwa akiahidi kukuza uchumi wa nchi kupitia rasilimali zilizopo zikiwamo za gesi na mafuta. Amepania kupitia mikataba ya gesi na mafuta ili inufaishe zaidi taifa. Ili kutekeleza yote haya, waziri atakyekabidhiwa dhamana atakuwa na kazi ya ziada.
7. WAZIRI WA FEDHA
Mmoja kati ya watu watakaokuwa na kibarua kigumu zaidi kwa serikali ya Lowassa au Dk. Magufuli ni yule atakayepewa kuongoza wizara hii. Ni kwa sababu huu ndiyo moyo wa kila serikali. Lowassa amesema atahakikisha kuwa mapato ya serikali yanaongezeka, ununuzi wa magari ya kifahari kama Toyota Land Cruiser (mashangingi) unakomeshwa na mwishowe fedha zitakazopatikana zitumike kuboresha huduma za jamii kama elimu. Kadhalika, Lowassa anasema vilevile kuwa akiingia madarakani atahakikisha inaaznishwa benki maalum kuwakopesha 'marafiki' zake amabo ni madereva wa bodaboda, mamalishe na wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Wamachinga.
Lowassa amaesisitiza vilevile kuwa ushuru wa 'kinyonyaji' kwa mazao ya wakulima ataufuta kwa nia ya kuhakikisha kuwa wakulima wananufaika na jasho lao. Kwa ahadi hizo, mtu atakayekuwa na dhamana ya wizara ya fedha atakuwa na kibarua cha ziada kufikia malengo huku pia akiepuka makusanyo yatokanayo na ushuru kwa wa mazao ya wakulima.
Kwa Dk. Magufuli pia siyo lelemama. Katika kampeni zake, Magufuli amesisitiza kuwa atakomesha kina mamalishe, bodaboda na wamachinga kunyanyaswa kwa kodi na ushuru mdogomdogo na badala yake atahakikisha kuwa mianya ya kodi inazibwa na ma[pato yanaongezeka mara mbili kutoka kiwango kinachokusanywa sasa kwa mwezi. Kama hiyo haitoshi, Magufuli amesema kuwa serikali ya awamu ya tano atakayoiongoza itaongeza fursa kwa wajasiriamali wadogo kupata mikopo na pia kuwezesha vitendea kazi kwa wachimbaji wadogo wa madini kama dhahabu na pia wafugaji na wavuvi. Waziri wa fedha atakuwa na kazi ngumu kuhakikisha kuwa malengo yote yanatimizwa.
8. WAZIRI WA SHERIA/KATIBA
Ikiwa Magufuli au Lowassa watashinda urais, Waziri katika wizara hii atakuwa na kibarua kizito. Ni kwa sababu katika mikutano yake ya kampeni, Lowassa amesema wazi kuwa atahakikisha kuwa anfanyia kazi suala la kina Sheikh Farid kushikiliwa na mahabusu kwa kesi inayohusiana na ugaidi.
Lowassa amegusia pia suala la mwanamuziki Babu Seya anayetumikia kifungo cha maisha. Kadhalika, Lowassa ameahidi vilevile kuwa serikali yake itapitia mikataba yote ya mafuta na gesi na kuifumua ikibidi ili mwishowe iwe na manufaa kwa Watanzania na siyo kwa kampuni za kigeni zinazokuja kuwekeza nchini na vigogo wachache walio serikalini.
Majukumu haya yote yako chini ya Wizara inayoshughulikia sheria na hivyo, ni wazi kwamba atakayekabidhiwa dhamana chini ya mwavuli wa Ukawa atakuwa na kazi nzito.
Kadhalika, ikiwa Dk. Magufuli ataingia ikulu kumrithi Rais Kikwete baada ya Oktoba 25, mtu atakayemteua kushika wizara hii atakuwa na kibarua kizito kuhakikisha kuwa anatimiza ndoto za Watanzania zitokanazo na ahadi wakati huu wa kampeni.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment