Mgombea wa Urais kupitia chama cha Chadema, Edward Lowassa (wa tatu kushoto) akiwaongoza viongozi wa Ukawa kuzindua ilani ya chama hicho katika Viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Kushoto ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, mgombea mwenza, Juma Duni Haji, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Sharif Hamad na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe. Picha na Maktaba.
Hivi sasa mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, wamejikuta pamoja katika kampeni za vyama vya upinzani kupitia Ukawa.
Wote walikuwa katika chama tawala, na wote wameshika nafasi za juu katika Taifa letu. Wakati wa kura za maoni ndani ya CCM, tulimsikia Sumaye akisema kwamba akipitishwa Lowassa, atakihama chama hicho.
Aliamini mgombea huyo hakuwa na sifa. Aliamini chama kitakachompitisha Lowassa, kitakuwa kimepoteza sifa ya kuwa chama makini, na yeye atakuwa mbali kabisa na chama hicho.
Mbali na yote yanayosemwa juu ya Lowassa, mazuri na mabaya, hatujasikia akisema hatakuwa tayari kufanya kazi na mtu yeyote yule. Je, hii ni sifa yake kubwa? Tulisikia waliosema kwamba wakiingia madarakani baadhi ya watu wajiandae kuikimbia nchi. Bahati nzuri watu hawa hawakupitishwa!
Lowassa yuko kimya juu ya jambo hili. Tumemsikia akisema kwamba hatalipiza kisasi. Tunaweza kusema kwa hili, Sumaye na Lowassa, wanatofautiana kabisa. Sumaye, alisema wazi wazi kwamba akichaguliwa Lowassa, yeye anahama CCM.
Sasa, Sumaye, yuleyule, ameamua kuikimbia CCM si kwa chama hicho kumpitisha Lowassa, bali kinyume chake. Kusema kweli ni kama CCM, walisikia kilio cha Sumaye na kuamua kumtupilia mbali Lowassa na kumpitisha John Magufuli.
Siasa haina adui, rafiki
Sote tulitegemea, mtu ambaye angeshangilia na kufurahia uteuzi huo ni Sumaye, lakini imekuwa tofauti. Sumaye, ameamua kumfuata adui yake. Pia, kweli, sote tunajua kwamba katika siasa, hakuna rafiki na adui wa kudumu. Aliyeitwa fisadi akiwa CCM, sasa ni shujaa wa Ukawa. Tumeshuhudia Sumaye akipanda jukwaani kumnadi Lowassa.
Kwa hili nauliza, tucheke au tulie? Au niseme kuwa haya sasa tumeshayazoea. Tumeshuhudia baadhi ya wanachama wa CCM, waliokuwa mabingwa wa kutupa vijembe kwa wapinzani na kupinga kila pendekezo la upinzani hata lenye faida kwa Taifa, leo hii wanapaza sauti ya ‘People’s power’.
Leo hii wanaeleza mabaya ya CCM na kuimba sifa za Ukawa. Hivi huu si unafiki? Wenyewe wanasema ni siasa! Sisi tunasema hao ni wasakatonge; wanayatumikia matumbo yao na familia zao. Hawana muda na uhai wa Taifa letu. Tukiwachagua hawa, tutakuwa tunajikaanga wenyewe.
Tumesikia wengine wakilalamika kwamba wamekaa kwenye nafasi moja kwa muda wa miaka 10. Wanakuja wengine wanapanda, wao wanabaki palepale. Nao wanataka tuwaamini, kwa nini hatukushuhudia wakiachia ngazi ili kuonyesha hasira yao ya kuwa kwenye nafasi moja kwa miaka yote hiyo? Kama wangefanya hivyo huko nyuma, leo hii wangeheshimika katika jamii. Wanapoyasema haya leo hii baada ya kuhama chama, tunaona ni sawa na kubwabwaja.
Ni kipindi kigumu
Kinyume na wale wanaoihama CCM kwa lengo la kutaka kugombea kupitia Ukawa, Sumaye, amehamia Ukawa kuiongezea nguvu, kama alivyoelezea yeye mwenyewe. Ameamua kukimbilia huko wakati pazia la Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC) kuhusu wagombea likiwa limeshafungwa. Hawezi kugombea udiwani, ubunge au urais, labda akiteuliwa hapo baadaye.
Tunajilazimisha kumwamini Sumaye, kwamba anajiunga na upinzani kuuongezea nguvu, maana sasa hivi hawezi kugombea. Maneno ya mitaani kwamba yeye ni sawa na spea, endapo likatokea la kutokea, basi yeye anachukua nafasi.
Haya ni matusi kwa Ukawa. Mbona wanajitosheleza? Mgombea mwenza ni jembe, sote tunajua hivyo, na bado wana watu wengi wenye uwezo. Haiwezekani kwamba muda wote walikuwa wakisubiri kukamata dola kwa kusaidiwa na wageni.
Tunaweza kujituliza kwa msemo wa hakuna rafiki na adui wa kudumu katika siasa. Lakini kwa mtu aliye makini ni lazima afikiri zaidi ya hapo. Taifa letu linapitia kipindi kigumu. Ni mara ya kwanza mawaziri wakuu wawili, mawaziri wa Serikali iliyo madarakani, wenyeviti wa CCM na wanachama mashuhuri, kukihama chama tawala na kujiunga na upinzani, ni kitu kipya.
Tunapata ujumbe gani? Ni mabadiliko? Ni upinzani kuwa na nguvu? Je, wimbi hili la CCM kuhamia upinzani linakwenda kuleta mabadiliko au kutengeneza CCM B, kama wenyewe wanavyosema na kama alivyosema Profesa Ibrahim Lipumba, kwamba hakuna cha Ukawa, bali Lowassa, anaanzisha CCM B?
Wazalendo wa Tanzania, hawawezi kusumbuliwa na CCM B, maana sote ni Watanzania. Kinachogomba ni sera, Ilani ya uchaguzi na utekelezaji. Kinachogomba ni mifumo, itikadi na falsafa ya kuliongoza Taifa letu. Wengine wanaupinga ubeberu na wengine wanaukumbatia ubeberu.
Tunawajua ambao itikadi yao ni ukuwadi wa soko huria na utandawazi. Tunawajua ambao itikadi yao ni uwekezaji hata kama maana yake ni kuiuza nchi. Tunawajua ambao hadi leo hii wanalaani kuzaliwa weusi, kuzungumza Kiswahili na kuishi Afrika, wangetamani kuishi Amerika na Ulaya.
Pia, tunawajua kabisa wale ambao bado wanazingatia falsafa ya mwasisi wa Taifa hili. Hawa wanatamani kuona Taifa letu linajitegemea na kujiendesha kwa siasa ya Ujamaa. Wale wanaoamini katika Umoja wa Afrika na ile falsafa ya binadamu wote ni sawa.
Hivyo kwa mabadiliko na kuijenga Tanzania mpya, jambo la msingi si CCM A, CCM B, au upinzani. Ni lazima kukubaliana itikadi ipi tunataka. Na hili haliwezi kutimia bila kuwa na Katiba ya wananchi. Kilio chetu si juu ya Lowassa na Sumaye kukimbilia Ukawa. Kilio kikubwa ni kuingia kwenye Uchaguzi Ukuu wa 2015 bila katiba mpya.
Inawezekana tulio CCM na upinzani, tunafikiria ushabiki, vijembe na matusi. Hii ni bahati mbaya na wala mwendo huu hauwezi kutusaidia chochote.
Tuko kwenye nyakati mpya, vijana ni wengi kuliko wazee na vijana wameaanza kupenda na kujali siasa. Mazoea yanakwisha, tunaanza kipindi kipya. Wakati wa ngonjera na nyimbo za ukombozi umepita. Tunahitaji kusikia sera, ilani, itikadi, dira, Katiba Mpya, mfumo wa kurithisha madaraka kwa vijana na mpango mzima wa kuijenga Tanzania mpya.
/Mtanzania.
No comments :
Post a Comment