Mgombea urais kupitia CCM Dk.John Magufuli akiwa na mpinzani wake kupitia Chadema Edward Lowassa wakifanya kampeni katika mikoa tofauti.
Mkoani Morogoro. Dk Magufuli aliahidi kuwanyang’anya ardhi vigogo wote waliohodhi ardhi bila kuiendeleza, akisema atawagawia wakulima na wafugaji.
Akihutubia wakazi wa Mtimbira wilayani Malinyi jana, Dk Magufuli alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza maeneo ya shughuli za kilimo na ufugaji na kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji iliyokithiri mkoani hapa.
Mgombea huyo alisema migogoro hiyo imechangiwa na kukosekana kwa eneo la kutosha kuziwezesha jamii hizo mbili kufanya shughuli zao.
Alisema hali halisi inaonyesha kuna ongezeko kubwa la matumizi ya ardhi inayohitajika na binadamu na mifugo huku eneo la ardhi likiwa ni lile lile.
Alisema wakati nchi inapata uhuru walikuwapo watu milioni 9 tu, lakini leo idadi hiyo inakaribia milioni 50 huku eneo likibaki kuwa kilomita 949,000 za mraba.
Dk Magufuli alisema wakati nchi inapata uhuru, kulikuwa na ng’ombe milioni 10, wakati hivi sasa wamefikia milioni 23.
Alisema mbuzi hawakufikia milioni moja, lakini sasa ni wamefika 14, kondoo ni milioni 6, na mbwa milioni 4, jamboambalo alisema linaloongeza mahitaji ya ardhi.
“Ila wapo watu wakubwa wengine wapo serikalini wana maelfu ya ekari ambazo hawazilimi, hawayafugii na wala hawaziendelezi, wameyahodhi tu. Nikipata urais nitawanyang’anya na kuwagawia wafugaji wanaohitaji kuchunga ng’ombe na wakulima wanaohitaji kulima,” alisema Dk Magufuli huku akishangiliwa.
Kauli hiyo aliirudia karibu mikutano yote aliyoifanya jana, ukiwamo wa Ifakara ambako aliwataka vigogo wanaomiliki hadi ekari 1,000 kwa mtu mmoja waanze kuzifanyia kazi mapema kwa kuwa serikali yake haitakuwa na wananchi wa daraja la kwanza wala la chini.
Dk Magufuli ambaye ameingia katika duru ya pili ya kampeni zake mikoani baada ya mapumziko ya kikazi ya siku mbili, alisema anatambua uwepo wa mgogoro wa mpaka wa pori na makazi ya wananchi wa bonde la Lamsa uliosababishwa na kutotenda haki na kwamba akiingia Magogoni atashughulikia haraka iwezekanavyo.
Akiwa Mahenge, mgombea huyo ambaye ni Waziri wa Ujenzi, aliendelea kuahidi ujenzi wa barabara ya Kivukoni hadi Mahenge yenye kilomita 67 kwa kiwango cha lami na kubainisha kuwa Serikali ilishaanza kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya kuunganisha mkoa wa Morogoro na Ruvuma kupitia Wilaya ya Malinyi hadi Songea.
Alisema barabara hiyo ya lami itakayoanzia Mikumi kupitia Ifakara, Lupilo hadi Songea itajengwa na makandarasi wanne au watano ili waimalize kwa haraka.
Aliahidi pia kuwa Serikali yake itaendeleza ujenzi wa daraja la Mto Kilombero linalogharimu Sh53.6 bilioni na kwamba hadi mwakani litakuwa limeshakamilika.
Dk Magufuli aliwaambia wananchi wa eneo hilo kuwa atawezesha kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vya mchele, nyama na maziwa.
“Tutaanzisha viwanda vya kuchambua mchele kwa sababu nimepita huku kila mahali ni mchele tu na hadi bei ipo chini kwa sababu mtu akija huku kununua anakulalia kwa sababu barabara ni mbaya,” alisema.
Katika mipango hiyo ya kukuza kilimo cha mpunga, alieleza kuwa ataanzisha soko la kimataifa la mchele litakalofanikisha uuzaji wa zao hilo hadi barani Ulaya.
Alirejea tena kauli yake kuwa anataka kuwa Rais wa Watanzania wote, Rais wa maendeleo, Rais wa kubadilisha nchi na kupiga vita rushwa.
Lowassa na ushuru wa tumbaku
Mkoani Tabora, Lowassa aliwaambia maelfu ya watu waliofurika kwenye Uwanja wa Town School kuwa
atakapoingia Ikulu, wakulima hawatalipa tena ushuru wa tumbaku.
“Nitahakikisha hakuna mkulima anayelipa ushuru wala kodi kwa zao la tumbaku ili kuhamasisha kilimo,” alisema Lowassa, ambaye alilazimika kuhutubia kwa dakika nane tu baada ya kuchelewa kufika mjini hapa.
“Nitaruhusu wakulima kuuza mazao yao nje ya nchi bila kikwazo chochote,” alisema Lowassa akizungumzia zao hilo ambalo kilimo chake kimekuwa kikidhibiwa na Serikali.
Lowassa alirudia kauli yake kuwa ameamua kugombea urais kwa kuwa anajua wananchi wana imani naye na kwamba alijipima na kujiona anatosha kuchukua nafasi hiyo ya juu katika siasa.
“Watanzania wana imani na mimi na ninatosha,” alisema Waziri Mkuu huyo wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne.
“Nimekuja kuwaomba mnichague kuwa Rais wa Tanzania. Nimejipima nikaona ninatosha ninaweza na nina sababu. Nimejipima na kuona Watanzania wengi wana imani na mimi.”
Aliwataka wananchi kuhakikisha wanalinda kura, akisema anaifahamu CCM kuwa ina tabia ya kuiba kura.
“Tunakwenda ikulu kwa kura,” aliongeza Lowassa huku akiwataka waliojiandikisha kupiga kura kunyosha mikono juu na kusisitiza kuwa anataka kuwa Rais ili kubadilisha nchi.
Lowassa, ambaye alisindikizwa na wananchi kwa maandamano mpaka Hoteli ya Orien ya mjini hapa baada ya mkutano wake kumaliza, aliamua kusimamisha msafara wake na kuwaomba wananchi watawanyike.
Lowassa alichelewa kufika uwanjani hapo kutokana na kuchelewa kumaliza mkutano wa kampeni uliofanyika wilayani Urambo alitokea wilayani Kaliua ambako nako pia alikuwa na mkutano wa kampeni
Wananchi waliohudhuria mkutano huo walishindwa kujizuia baada ya chopa iliyombeba Lowassa kutua Uwanja wa Town School na baadhi kutaka kuifuata kwa lengo la kumuona mgombea huyo, hali ambayo iliwapa wakati mgumu walinzi kuwazuia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema mabadiliko yatakayotokea Oktoba 25 mwaka huu ni mpango wa Mungu, na si wa viongozi wa chama hicho.
“Tunahitaji umoja wa kitaifa na kupata kura ya kila mtu ili kuiondoa CCM madarakani,” alisema Mbowe.
Naye Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye alisema ili Tanzania isonge mbele inahitaji mabadiliko na wakati ni sasa.
“Binafsi nina ujuzi na Serikali na nimekuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10. Nchi haikuwa na vita, hata Ukawa tukiingia madarakani, nchi haiwezi kuwa na vita. Msitishike na kauli zao (CCM) kwamba Ukawa tukichukua nchi kutakuwa na vita.
“Machafuko yatatokea kama CCM ikikataa mabadiliko ambayo yatafanywa na wananchi kwa kutokichagua chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu,” alisema Sumaye.
/Mwananchi.
No comments :
Post a Comment