Mgombea wa urais kupitia CCM Dk John Magufuli akiwahutubia wakazi wa Mtwara mjini kwenye Uwanja wa Mashujaa jana. Picha na Adam Mzee wa CCM
- Mgombea huyo anayetumia kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’, amekuwa akisisitiza zaidi mabadiliko na kutangaza vita dhidi ya watendaji wazembe, wanaofanya kazi kwa mazoea akiwataka wajiondoe endapo ataingia Ikulu.
Alitimiza siku hizo 10 kwa mkutano mkubwa uliofanyika kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi.
Katika utekelezaji wa ilani ya CCM, Dk Magufuli amekuwa akiahidi baadhi ya vitu kama; elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, kuboresha huduma za afya kwa kujenga zahanati na hospitali kila kijiji, kata, wilaya na mkoa,
kukuza soko la mazao ya kilimo na ujenzi wa barabara za lami nchini.
Dk Magufuli anasema pia kuwa atakachokiangalia ni pensheni kwa wazee, mikopo ya Sh50 milioni kwa kina mama na vijana kwa kila kata, ujenzi wa viwanda, usambazaji wa huduma za umeme, maji na kuboresha masilahi ya wafanyakazi wote nchini na vyombo vya ulinzi na usalama.
Kwa kipindi hicho cha siku 10 kutoka Wilaya ya Mpanda Vijijini hadi Songea Mjini, mwandishi wetu ambaye ameambatana na mgombea huyo ameangalia kwa ufupi baadhi ya mafanikio na changamoto za kisera katika kampeni za Dk Magufuli.
Kuendana na ilani
Waziri huyo wa Ujenzi amekuwa makini kwenye kuahidi miradi mikubwa ya mabilioni ya fedha kama ujenzi wa daraja la Mto Ruhuhu, Barabara za Njombe – Makete, Tabora – Ipole – Koga – Mpanda, reli ya kisasa kutoka Mtwara – Songea – Mbamba Bay na matawi ya kwenda machimbo ya Mchuchuma na Liganga mkoani Mbeya.
Utoaji wa ahadi hizo umemfanya kuaminiwa na wananchi ambao wamekuwa wakitumia rekodi yake ya utendaji katika wizara alizowahi kuongoza miaka 20 iliyopita ikiwamo ya Ujenzi.
“Ninaamini anayosema atayatekeleza kwa sababu hata zile ahadi za barabara amezitekeleza kikamilifu. Ni mkali anasimamia mambo,” anasema Esau Bukila, mkazi wa Kijiji cha Lituhi, wilayani Nyasa.
Utoaji wa maagizo
Hata hivyo, ahadi hizo na sifa za utendaji za Dk Magufuli, wakati mwingine zimekuwa zikiambatana na maagizo ya moja kwa moja kwa watendaji husika hasa kwa wale wa Wizara ya Ujenzi ambayo anaisimamia licha ya kuwa yupo kwenye kampeni.
Akiwa Mbalizi, Mbeya Vijijini na Makongorosi wilayani Chunya, mgombea huyo alimwagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), atangaze haraka zabuni ya ujenzi wa barabara ya kilomita moja ya Mbalizi na Makongorosi.
“Mkuu wa Mkoa (Abbas Kandoro), nenda kamweleze meneja wa mkoa wa Tanroads ndani ya wiki moja aanze kutekeleza ujenzi wa hii barabara.
Mwambie aanze, nitazungumza na Ofisa Mkuu kule Dar es Salaam leo hii fedha zije aanze kufanya kazi lakini mengine nitayafanya nikiteuliwa,” alisema Dk Magufuli na kufafanua kuwa anaagiza kwa kuwa bado “ana kauwaziri wa ujenzi hata kama ni mgombea.”
Kuwafikia wananchi wengi
Ndani ya siku hizo, Dk Magufuli amekuwa akijitahidi kuhutubia karibu kila eneo analokuta wananchi wamejikusanya au wamemzuia asipite mara nyingi hadi awahutubie licha ya kutokuwapo kwenye ratiba ya mkutano.
Mwenyewe amekuwa akisema; “ameamua kufanya kampeni kwa kutumia barabara ili ayajue matatizo kwa kutaabika na wananchi.”
Hata hivyo, mtindo huo umekuwa ukigharimu utunzaji wa muda na wakati mwingine kumuathiri hadi ufanisi wa sauti kwa kuwa muda mwingi anautumia kuhutubia.
Utii wa kusimama katika kila mkusanyiko ulichangia kukausha sauti yake baada ya kuhutubia mikutano isiyopungua 12 ikilinganishwa na wastani wa mikutano mitano kwa siku wakati wa safari ya Vwawa - Chunya na kupunguza ufanisi wa kampeni za Kyela, Rungwe na Mbeya mjini siku iliyofuatia.
Kuunganisha makundi
Ni dhahiri Dk Magufuli anatafuta njia madhubuti ya kuwanadi wagombea ubunge wa chama hicho kwa wananchi lakini pia kuwaunganisha baadhi ya makada waliogawanyika baada ya mtifuano wa kura za maoni za uteuzi wa wabunge.
Katika mkutano amekuwa akiwanadi wabunge wa majimbo husika na haraka kuwaomba wananchi “wawasamehe saba mara 70 kama kuna makosa wamefanya” ili wapigie kura CCM kuanzia urais hadi udiwani.
Mfumo huo, umeonekana kuwavutia makada wengi wa chama hicho tawala lakini ili kuwapoza, Dk Magufuli amekuwa akiahidi kuletewa majina ya makada wote walioshindwa kura za maoni ili awapatie kazi akiwa rais.
Ahadi za vyeo hivyo huenda zikaonekana lulu ya kuwaunganisha lakini hatari iwapo hatatimiza ahadi zake.
Kukisafisha chama
Mbali na kuunganisha makundi ndani ya CCM, Dk Magufuli anafanya kazi kubwa ya kuirudisha imani ya Watanzania kwa CCM baada ya chama hicho kukumbwa na kashfa za utendaji mbovu na ufisadi.
Amekuwa akiwasihi wananchi kutoihukumu CCM kwa sababu ya waovu wachache ambao aliahidi kuwa akiingia madarakani, atawasafisha.
Amekuwa akiwataka Watanzania kutokimbilia mabadiliko yasiyo na mipango kwa shauku ya kuing’oa CCM ili kuyatimiza badala yake wampe urais ili akate kiu yao ndani ya CCM.
“Wapo watu wanasema CCM imeoza tu hata mngechagua nani, nataka niwaambie, hasa vijana, tusifanye mabadiliko kwa jazba yakatuletea madhara kwa sababu mifano hai tunayo duniani,” alisema Dk Magufuli mjini Mbinga na kutoa mifano ya mapinduzi ya Libya yalivyoiacha nchi hiyo kwenye machafuko.
“Hivi jamani kitanda kikiwa na kunguni unachoma kitanda? Hapana, unachofanya ni kuwaua kunguni ili ulale kwa amani na raha mustarehe.”
Pamoja na kukisafisha chama, kauli za Dk Magufuli wakati mwingine zinatafsiriwa na upinzani kama njia ya kutengeneza hofu ya mabadiliko miongoni mwa wananchi.
Vyanzo vya mapato
Mara nyingi Dk Magufuli amekuwa akieleza kuwa Serikali yake itapunguza sherehe zisizo na tija kama siku ya maziwa, maji au nyama ili kutunza fedha za umma, lakini undani katika vyanzo vingine hasa vya kodi umekuwa ukisikika kwa wastani.
“Wapo watu watasema hizo ni siasa tu atatoa wapi wa fedha? Nchi hii, tajiri ina makaa ya mawe, ina maziwa 21, bahari kubwa mpaka watu wanaiba tu pesa, madini ya kila aina, wanyama, mifugo, hatuwezi tukashindwa, naomba mnipe urais niwafanyie kazi,” anaeleza Dk Magufuli.
Anasema fedha ziko pia katika maeneo ya utalii, kuwabana wasiolipa kodi na kwamba wakubwa na wadogo wote walipe kodi na kuziba kwa kiasi kikubwa mianya ya rushwa kwa kuongeza ufanisi wa kazi.
Vijembe
Licha ya mgombea huyo kutangaza mara kadhaa kuwa atafanya kampeni safi zisizomtukana mtu yeyote, baadhi ya makada wanaomnadi wamekuwa wakimwangusha kwa kutumia jukwaa hilo kupiga vijembe na kutumia lugha za maudhi kujibu mapigo ya upande wa pili wa upinzani hasa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akihutubia wakazi wa Songea Mjini, mgombea huyo alisema: “Hatutamtukana mgombea yeyote. Sisi tutafanya kampeni za kistaarabu kwa sababu tunahitaji kura za Watanzania wote na hivi ndivyo ninavyotaka uongozi wangu uwe.”
Lakini dakika sita tu baada ya kauli hiyo, Dk Magufuli alimwachia jukwaa mjumbe wa kamati ya kampeni, Mwigulu Nchemba ambaye tangu sekunde ya kwanza hadi ya mwisho alikuwa akirusha vijembe akiomba “kuweka kumbukumbu na mambo sawa kwa Watanzania” ili watakapokuja upinzani kuwadanganya wawe na majibu.
Vijembe hivyo vilivyoanzia mkoani Mbeya kwa kuwaponda mgombea wa urais wa Chadema kupitia Ukawa, Edward Lowassa na Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye viliendelea juzi ikiwa ni majibu ya vile vilivyotolewa siku ya uzinduzi wa kampeni za Ukawa.
Pia, kada mwingine Amon Mpanju naye kwa siku tatu zilizopita ameonekana kuwa mtambo wa vijembe kwa Ukawa akieleza kuwa rais anayefaa ni Dk Magufuli wengine ni maigizo na mambo mengine ambayo siyo rahisi kuandikika.
‘Mimi ni maji moto kuunguza mafisadi’
Jana, akiwa Newala Mjini, Dk Magufuli aliwaomba Watanzania wamchague kwa kuwa yeye ni maji ya moto ya kuwaunguza mafisadi wanaotafuna fedha za umma na kuchelewesha maendeleo.
Akiwa katika Uwanja wa CCM – Sabasaba, Dk Magufuli alisema hakuna haja ya kuichukia Serikali kwa sababu ya mafisadi wachache aliowafananisha na kunguni kitandani ni rahisi kuwaondoa.
Huku akishangiliwa na umati ulijitokeza mahali hapo saa tatu asubuhi alisema: “Mimi ni maji ya moto kwa mafisadi nipeni urais muone nitakavyowaunguza.”
Katika mwendelezo wa ahadi zake mkoani Mtwara, msisitizo mkubwa aliuweka zaidi katika namna atakavyokuza uchumi wa eneo hilo kwa kutumia gesi asilia na kuongeza thamani ya zao la korosho kwa kujenga viwanda. Aliahidi pia kujenga Barabara ya Masasi – Newala – Mtwara kwa kiwango cha lami.
“Nipeni tu urais tuwaletee maji kwanza huyo waziri wa maji nitakayemteua, hatashinda Dar es Salaam akisherehekea wiki ya maji. Katika uongozi wangu sipendi ubabaishaji. Nikisema A basi ni A na nikisema mti unakuwa mti ndiyo maana wale mafisadi walipoona nimeteuliwa walikimbia wenyewe,” alisema na kushangiliwa.
Mgombea huyo ambaye yupo katika siku ya 11 ya kampeni zake, alipofika katika Kijiji cha Lidumbe, Newala saa 4.02 asubuhi, alijumuika na wanakijiji kuomboleza msiba wa Zainabu Abdallah aliyefariki juzi na kutoa ubani wa Sh400,000.
Mmoja wa ndugu wa marehemu huyo, Sofia Litonji alimwambia mwandishi wetu kuwa amefurahishwa na kitendo cha Dk Magufuli kuwapatia pole kwa kuwa siyo kawaida kiongozi wa ngazi yake kufanya hivyo.
Mtwara Mjini
Akiwa Mtwara Mjini, alipokewa na maelfu ya wakazi wa ambao aliwaahidi kuwa rasilimali ya gesi asilia iliyogundulika katika eneo hilo itatumika kuwanufaisha wao kwanza na taifa kwa ujumla kwa kujenga viwanda vikubwa na kuzalisha ajira.
Aliingia Mtwara Mjini saa 9.10 alasiri na kupokewa na msafara wa bodaboda hadi katika Uwanja wa Mashujaa.
Huku akionekana mwenye furaha kubwa, Dk Magufuli alisema: “Awamu ya nne imeshaanza kujenga viwanda hapa ikiwamo Kiwanda cha Saruji cha Dangote, katika utawala wangu nitatandika viwanda kote hapahapa Mtwara.
Sehemu kubwa ya hotuba zake tangu alipoingia mkoani hapa amekuwa akizungumzia gesi.
Itakumbukwa kuwa wakazi wa mkoa huo waliitikisa Serikali mwaka 2013 wakiigomea isijenge bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa madai kuwa ikisafirishwa hawatanufaika nayo na kubaki maskini.
Hata hivyo, akiwa Ziwani, Mtwara Vijijini moja ya maeneo inakopatikana gesi hiyo, wananchi walimpokea kwa shangwe naye kuwaambia: “nina deni la kuwaletea maendeleo.”
/Mwananchi.
No comments :
Post a Comment