Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Elimu ya juu nchini, Profesa Sylivia Temu, alisema mradi huo unaotekelezwa na serikali kwa ushirikiano na Benki ya Maendeleo Afrika, ni mojawapo ya miradi minne ya afya inayotekelezwa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki ikilenga kutatua changamoto mbalimbali za kiafya.
“Kila nchi ya Afrika Mashariki ina mradi wa aina yake kwenye sekta hii muhimu na kwa upande wetu sisi umejikita katika kukabiliana na magonjwa ya moyo na utakuwa chini ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (Muhas) na utakwenda sambamba na ujenzi wa kampasi mpya ya chuo hicho unaondelea eneo la Mloganzila jijini Dar es Salaam,’’ alisema Temu.Akizungumzia faida za mradi huo, Profesa Temu aliyemwakilisha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema utasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa ya moyo nchini.
Pia alisema utapunguza gharama zinazolikabili taifa kwa sasa kutokana na kusafirisha nje idadi kubwa ya wagonjwa wa moyo kupata matibabu.
“Lakini pia kupitia kituo hiki kitakacho kuwa kikubwa kabisa hapa Afrika Mashariki, tunarajia kwamba tafiti nyingi za masuala ya kiafya hasa kwenye eneo hili la magonjwa ya moyo zitakuwa zikifanyika hapa nchini na pia kupitia Muhas, tutazalisha wataalam wengi wa magonjwa hayo kwa manufaa ya vyuo vingine ndani na nje ya nchi,’’ aliongeza.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Muhas, Profesa Ephata Kaaya, alisema chuo chake kimejipanga kutekeleza mradi huo mkubwa utakaotekelezwa kwa awamu mbili.
Alisema awamu ya kwanza utahusisha mafunzo pamoja na maandalizi ya vifaa huku awamu ya pili ikuhusisha ujenzi kamili wa kituo hicho.
“Tafsiri ya uzinduzi huu ni kwamba Muhas tunapewa heshima ya kusimamia kituo hiki muhimu na hakitahudumia Watanzania pekee, bali nchi zote wanachama wa Afrika Mashariki kutokana na ukweli kwamba na nchi nyingine pia nazo zinaendesha miradi yenye hadhi kama hii ila katika nyanja tofauti za kiafya,’’ alisema.
Meneja Miradi ya Jamii kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika, Hamis Simba, alizitaja baadhi ya sababu zilizosababisha benki hiyo kufadhili mradi ho kuwa ni pamoja na kuvutiwa na mikakati ya Tanzania na nchi za Afrika Mashariki kwa ujumla katika kukabiliana na magonjwa ya moyo.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment