WAFUASI wa Chama cha Wananchi CUF Kisiwani Pemba, wakimsikiliza mgombea urais wa chama hicho Mhe: maalim Seif Sharif Hamad katika mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Tibirinzi Chake chake, (Picha na Haji Nassor, Pemba
WAANDISHI wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari , wakiwa kazini katika mkutano wa hadhara wa kampeni wa chama cha wananchi CUF, uliofanyika uwanja wa Tibirinzi Chake chake Pemba, (Picha na Haji Nassor, Pemba).
KIKUNDI cha wasanii kutoka wilaya ya Wete wakiwaburudisha viongozi na wanachama wa chama cha wananchi CUF, waliohudhuria kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni ya mgombea urais uliofanyika uwanja wa Tibirinzi Chake chake kisiwani Pemba, (Picha na Haji Nassor, Pemba).
VIONGOZI wa chama cha maendeleo na Demokrasia CHADEMA waliohudhuria katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni ya chama cha wananchi CUF (UKAWA), uliofanyika uwanja wa Tibirinzi Chake chake Pemba, (Picha na Haji Nassor Pemba).
NAIBU Katibu Mkuu wa chama cha wananchi CUF Nassor Ahmed Mazrui akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kampeni wa kumnadi mgombea urais kupitia chama cha wananchi CUF, (Picha na Haji Nassor Pemba).
MGOMBEA urais wa chama cha wananchi CUF maalim SEIF Sharif Hamad akizungumza na wafuasi wa chama hicho katika mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika katika kiwanja cha Tibirinzi Chake chake Kisiwani Pemba,(Picha na Haji nassor, Pemba).
Na Hassan Hamad OMKR
Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar atahakikisha kuwa serikali yake itakuwa na utawala unaojali uhuru wa nchi, haki za kila Mzanzibari na kujali maridhiano ya Wazanzibari.
Aidha amesema serikali yake itapambana vikali na vitendo vya rushwa ya aina zote, ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za nchi, bila ya kujali cheo au ukaribu wa mtu kwa serikali.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo leo wakati akinadi sera za Chama hicho kwenye ufunguzi wa kampeni za Urais wa Zanzibar, uliofanyika viwanja vya Tibirinzi Chake Chake Pemba.
Amesema vitendo vya rushwa na ufisadi vimekuwa vikididimiza uchumi na maendeleo ya wananchi, na kwamba hatokubali kuona vitendo hivyo vinaendelea.
Amefahamisha kuwa katika kuhakikisha kuwa vitendo vya rushwa vinaepukwa, serikali atakayoiongoza iwapo atapata ridhaa ya wananchi katika uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, ataimarisha maslahi ya wafanyakazi wa serikali pamoja na kuwalipa stahiki zao.
Ameongeza kuwa lengo la serikali yake ni kuwaunganisha wazanzibari na kuwapatia haki zao bila ubaguzi wa aina yoyote, ili wananchi wajisikie kuwa na uhuru ndani ya nchi yao.
Akizungumzia maendeleo ya kiuchumi, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema ataimarisha miundombinu ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuufanyia matengenezo makubwa uwanja wa ndege wa Pemba, ili ndege kubwa za mizigo na watalii ziweze kutua.
Amesema kufanya hivyo kutavutia wageni wengi kuingia katika kisiwa cha Pemba, hatua ambayo itaimarisha sekta ya utalii ambapo serikali itahamasisha ujenzi wa hoteli kubwa za kisasa.
Katika hatua nyengine Maalim Seif amesema anakusudia kuviunganisha visiwa vya Unguja na Pemba kwa kujenga bandari mpya katika eneo la Mkokotoni na Mkoani, na hatimaye boti za kisasa zitatumika kurahisisha usafiri wa baharini baina ya Pemba na Unguja.
Ameeleza kuwa wakulima na wafanyabiashara watanufaika na hatua hiyo, kwa vile itarahisisha mawasiliano, na kwamba watakuwa na uwezo wa kwenda na kurudi Unguja na Pemba kupeleka bidhaa zao.
Nae mratibu wa Kampeni za CUF kwa upande wa Pemba Mhe. Hamad Massoud Hamad, amemuhakikishia mgombea huyo kuwa CUF kimejipanga vizuri kuweza kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu ujao.
Kwa upande wake Mgombea wa uwakilishi jimbo la Malindi Ismail Jussa Ladhu, amewataka wananchi wa Pemba kujipanga ili kuweza kushinda majimbo yote 18 ya Pemba.
Amesema kwa Upande wa Unguja chama hicho pia kimejipanga kuhakikisha kuwa kinapata idadi kama hiyo ya majimbo ili kujiwekea mazingira bora katika baraza la Mawaziri na Baraza la Wawakilishi.
Akizungumzia ugawaji mpya wa majimbo, Mhe. Jussa amesema mgao huo haukukiathiri chama hicho, na badala yake umekijengea mazingira bora zaidi ya kuongeza idadi ya majimbo na kura za urais.
Msaidizi meneja Kampeni wa CUF Mansoor Yussuf Himid amewaambia wananchi wa Pemba kuwa ameshinda pingamizi yake aliyowekewa na CCM na sasa ni mgombea halali wa uwakilishi katika Jimbo la Chukwani, na kuwahakikishia wananchi hao atapata ushindi katika jimbo hilo.
Amesema katika jitihada za kujikwamua kiuchumi, Zanzibar inahitaji kiongozi mwenye dhamira njema na Zanzibar, mkweli na asiyeyumba, na kwamba Maalim Seif anazo sifa hizo bali kinachohitajika ni ushirikiano wa Wazanzibari, ili waweze kumchagua kwa asilimia kubwa.
No comments :
Post a Comment