Paul Sarwatt
Toleo la 420
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) katika Mkoa wa Arusha kiko njia panda kutokana na hatua ya baadhi ya wagombea katika majimbo ya uchaguzi kwa nafasi za udiwani na ubunge waliokuwa wafuasi wa mgombea urais wa umoja wa vyama vinavyounda Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, kususa kumwombea kura mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, wakati wa kampeni.Moja ya majimbo ambayo tayari wagombea wake wamekubaliana kwa pamoja kususa kumwombea kura Dk. Magufuli ni Monduli, mkoani Arusha ambako ni nyumbani kwa Lowassa.
Toleo la 420
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) katika Mkoa wa Arusha kiko njia panda kutokana na hatua ya baadhi ya wagombea katika majimbo ya uchaguzi kwa nafasi za udiwani na ubunge waliokuwa wafuasi wa mgombea urais wa umoja wa vyama vinavyounda Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, kususa kumwombea kura mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, wakati wa kampeni.Moja ya majimbo ambayo tayari wagombea wake wamekubaliana kwa pamoja kususa kumwombea kura Dk. Magufuli ni Monduli, mkoani Arusha ambako ni nyumbani kwa Lowassa.
Hali hiyo ya mgomo baridi dhidi ya Magufuli inatajwa pia kuwapo katika majimbo ya Arusha Mjini na Arumeru Mashariki ambako wagombea wa CCM kwa nafasi za udiwani na ubunge wanadaiwa kuwa wafuasi wa Lowassa wakati wa harakati zake za kusaka nafasi ya urais kupitia CCM.
Lowassa ambaye alihudumu katika serikali kwa muda mrefu alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 20 (1995-2015), kabla ya kustaafu na kugombea urais kwa tiketi ya CCM ambapo vikao vya juu vya chama hicho tawala viliondoa jina lake na baadaye kuhamia Chadema ambako ndiye mgombea wa urais, akiungwa rasmi mkono na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF) na NLD.Taarifa zilizopatikana kutoka Monduli na baadaye kuthibitishwa na vyanzo vya uhakika vya habari vya gazeti hili, zinadai kuwa mgombea ubunge katika jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Namelok Sokoine, ndiye aliyetoa maelekezo kwa wagombea udiwani wasuse kumpigia kampeni Dk. Magufuli.
Namelok ambaye hata hivyo taarifa zinaonyesha kuwa hakuhudhuria mkutano huo, anadaiwa kutoa maelekezo hayo kupitia kwa Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Elisante Kimaro na mmoja wa wagombea, Diwani Kimaay.
Namelok ambaye ni mtoto wa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Sokoine, amepitishwa na CCM kugombea ubunge katika jimbo hilo dhidi ya mgombea wa Chadema kwa mwavuli wa Ukawa, Julius Kalanga.
Kikao cha wagombea
Taarifa zilizopatikana kutoka Monduli zinadai kuwa Agosti 19, mwaka huu, wagombea wa udiwani kutoka kata 20 za jimbo hilo walikutana katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za CCM za wilaya hiyo.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinadai kuwa pamoja na mambo mengine, wagombea hao walijadili kwa kina ajenda ya jinsi ya kuendesha kampeni na mgombea gani wamuunge mkono kati ya Lowassa na Magufuli.
Mmoja wa wagombea udiwani aliyehudhuria kikao hicho aliyeomba jina lake lihifadhiwe, alieleza kuwa wagombea wote walikubaliana kwa pamoja kuwa hatua ya kumpigia kampeni mgombea wa CCM, Dk. Magufuli, katika kata zao na jimbo hilo ni kumsaliti Lowassa ambaye kwa pamoja, wanamheshimu na bado wanampenda.
Kwa mujibu wa mgombea huyo hatua hiyo ya kususia kampeni za Magufuli zimelenga kuwaaminisha wananchi wa Monduli, kuwa bado wanamuunga mkono Lowassa katika harakati zake za kisiasa pamoja na kwamba mwanasiasa huyo amehamia upinzani.
“Katika maeneo mengi wananchi wamekuwa wanamhoji Namelok na wagombea wengine wa udiwani kwa nini bado wako CCM na hawajahamia Ukawa? Kutokana na hali hiyo tulikubaliana kwamba kwa mazingira ya kisiasa na hali iliyopo, si rahisi kumnadi Dk. Magufuli na wapiga kura wa jimbo hili hawatatuelewa” alieleza mgombea huyo.
Aidha taarifa zingine zinadai kuwa hatua ya Namelok na wenzake kufikia uamuzi huo pia inalenga kumridhisha Lowassa na kambi yake kuwa bado wanamuunga mkono, baada ya mpango na mazungumzo ya muda mrefu ya kuwashawishi kuhamia Ukawa kukwama.
Raia Mwema inazo taarifa kuwa Namelok alikuwa akutane na Lowassa nyumbani kwake Monduli, kati Agosti 15 na 16 mwaka huu, lakini kikao hicho kilishindikana baada ya Namelok kuzima simu yake kwa siku mbili mfululizo lengo likiwa kumkwepa Lowassa.
Inadaiwa kuwa Namelok ambaye aliibuliwa na kuingia katika siasa kwa ushawishi wa Lowassa, amekwama kumfuata Ukawa kutokana na sababu zinazotajwa kuwa ni kulinda maslahi ya kibiashara yanayotokana na zabuni za serikali.
Kauli ya Katibu CCM
Juhudi za kumpata Namelok hazikuweza kufanikiwa kupitia simu yake ambayo iliiita bila ya kujibiwa kwa siku mbili mfululizo mwishoni mwa wiki, lakini akijibu tuhuma hizo Katibu wa CCM Wilaya ya Monduli, Elisante Kimaro, alikanusha akisema si taarifa za kweli.
“Kwanza nikuombe kwa dhati kuwa kwa maslahi ya chama na wagombea usiandike habari hiyo, itatuletea mtafaruku hapa jimboni kwa kuwa tunaelekea kuanza kampeni na wapinzani wetu wataitumia kama mtaji,” alisema Kimaro.
Hata hivyo Kimaro alifafanua kuwa hawana sababu ya kutomfanyia kampeni Magufuli na kikao kilichofanyika Jumatano kililenga kuweka mkakati wa kuhakikisha CCM kinashinda katika kata zote 20 za jimbo hilo.
“Tuna wanachama 67,000 katika wilaya yetu, wapiga kura waliojiandikisha ni 79,000 na waliopiga kura za maoni za CCM 46,000 hivyo kwa takwimu hizi utaona kuwa tuna nafasi kubwa ya kuibuka washindi,” alijigamba.
Kwa upande wake mmoja wa wagombea aliyeshiriki kikao hicho, Diwani Kimaay, alikiri kuwa bado wanamheshimu Lowassa kutokana na mchango wa miaka 20 katika kuliongoza jimbo hilo na kama mmoja wa viongozi juu serikalini aliyetokea Monduli.
“Hata kama Mzee Lowassa amehamia Ukawa hatuna sababu ya kumchukia, ni mwana-Monduli mwenzetu, ni Mtanzania mwenzetu, tunamheshimu na bado tutaendelea kumheshimu,” alisema.
Kuhusu kususia kampeni za Magufuli mgombea huyo alisema: “Dk. Magufuli ni mgombea wa CCM ana timu yake ya kampeni waliopangwa kufanya kazi ya kumnadi na pia atajiombea kura mwenyewe”.
Baada ya kubanwa kuwa yeye ni mgombea wa CCM na kwa utaratibu wa chama anatakiwa kumpigia kampeni Magufuli katika ngazi ya kata yake, Kimaay alijibu: “Tutamfanyia kampeni pale itakapobidi,” na kukata simu yake.
Wachunguzi wa masuala ya kisiasa mkoani hapa wanabashiri kutokana na mgongano huo, CCM iko katika hatari ya kupoteza jimbo hilo ambalo ilikuwa ngome yake kwa muda mrefu kwa Ukawa.
Jimbo la Arusha
Katika Jimbo la Arusha Mjini kuna mazingira ya kisiasa yanyofanana na Jimbo la Monduli baada ya vikao vya juu vya CCM kumpitissha mfanyabiashara maarufu wa Arusha, Philemon Mollel (Monaban), kuwa mgombea wake.
Mfanyabiashara huyo ametajwa mara nyingi kuwa ni “mfuasi” wa Lowassa na ameshiriki katika harakati za awali za kisiasa za mgombea huyo wa urais kupitia Ukawa, kabla ya kukatwa jina na vikao vya juu vya CCM mapema mwezi Juni, mwaka huu.
Kwa mujibu wa msimamizi wa uchaguzi katika Jimbo la Arusha Mjini, Mollel anatarajiwa kupambana na Mbunge anayetetea kiti chake, Godbless Lema (Chadema) na Estomih Mallah (ACT-Wazalendo).
Hata hivyo duru za kisiasa zinaonyesha kuwa uwezekano wa Mollel kushinda ni mdogo kutokana na msingi kuwa hata yeye mwenyewe “hana morali” ya kufanya kampeni kutokana na kile kinachotajwa kuwa ni mapenzi yake ya kisiasa kwa Lowassa.
“Wana CCM wengi wameshangazwa na uamuzi wa vikao vya juu vya CCM kuhusu uteuzi wa huyo mgombea ambaye anafahamika dhahiri kuwa ni mfuasi wa karibu wa Edward Lowassa,” alieleza mmoja wa viongozi wa CCM wa Wilaya ya Arusha Mjini.
Aidha dosari nyingine kwa CCM ni hatua ya waliokuwa wagombea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini walioshindwa katika kura za maoni kugoma kumuunga mkono mgombea huyo katika kikao cha pamoja, kilichofanyika Jumanne ya Agosti 18, mwaka huu.
Katika kikao hicho wagombea saba walioitwa ofisi za CCM walikataa kumuunga mkono Mollel wakati wa kampeni wakidai kuwa mfanyabiashara huyo alikiuka kanuni na sheria za uchaguzi kwa kutumia fedha na kuanza kampeni miaka mitatu iliyopita.
“Kutokana na mazingira hayo ni dhahiri kuwa katika Jimbo la Arusha Mjini, mgombea anayewakilisha Ukawa (Lema) atakuwa na kazi nyepesi sana kutokana na upungufu wa mshindani wake,” alieleza kiongozi huyo wa CCM.
Hata hivyo Mollel alikanusha kuhusishwa na mgombea wa urais wa Ukawa na kueleza kuwa taarifa hizo ni za uwongo na chanzo chake ni wagombea aliowashinda katika mchakato wa kura za maoni.
“Ni kweli Lowassa ni rafiki yangu lakini si katika medani hii ya siasa, mimi ni mwana CCM, nimedhamiria kwa dhati kugombea kwa ridhaa yangu, na nitasimama hadi mwisho kukipigania chama change,” alisema mfanyabiashara huyo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Arusha Mjini, Ferouz Bano, aliimbia Raia Mwema kuwa chama chake kimefanya uchunguzi wa kutosha na kujiridhisha kuwa mgombea wao hana shaka na anaaminika, tofauti na taarifa hizo zilizosambaa mitaani.
“CCM ina vyanzo vya kutosha vya kupata taarifa za uhakika, na ni kwamba mgombea wetu wa ubunge hana mashaka na madai yanayotolewa tumeyachunguza na kujiridhisha kuwa hayana msingi,” alisema.
Jimbo la Arumeru Mashariki
Katika Jimbo la Arumeru Mashariki, mgombea wa CCM John Pallangyo (maarufu kama JohnD) atakabiliana na Joshua Nassari (Chadema) na taarifa zinaeleza kwamba mgombea huyo naye anahusishwa na Lowassa.
“Huyo kuna wakati alikuwa anahudhuria vikao vya kisiasa nyumbani kwa Lowassa wakati akitafuta tiketi ya urais kupitia CCM, lakini baada ya Lowassa kuhama bado haijafahamika wazi msimamo wake,” kilieleza chanzo chetu kutoka wilayani humo.
Hata hivyo inaelezwa kutokana na hali hiyo ya mpasuko unaoikabili CCM baada ya mchakato wa kura za maoni ambapo mgombea huyo anadaiwa kushinda kwa mizengwe, wachambuzi wa masuala ya kisasa wanampa nafasi kubwa mgombea wa Chadema, Joshua Nassari, kushinda.
Majimbo ambayo CCM inaweza kutoa ushindani katika Mkoa wa Arusha ni pamoja na Longido, Karatu, Ngorongoro na Arumeru Magharibi ambako chama hicho kina wagombea wasiohusishwa na mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.
Kwa mujibu wa taarifa ya wasimamizi wa uchaguzi kutoka katika majimbo hayo wagombea waliopitishwa ni Dk. Steven Kiruswa (CCM), Onesmo Nangole (Chadema) kwa Jimbo la Longido, William ole Nasha (CCM) na Elias Ngorissa (Chadema) – Jimbo la Ngorongoro, Dk.Willbard Lorri (CCM) na Willy Qambalo (Chadema) – Jimbo la Karatu na Loyi Thomas Sabaya (CCM), Gibson Meseyeki (Chadema) kwa Jimbo la Arumeru Magharibi.
No comments :
Post a Comment