Aliyekuwa Kada mkongwe wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kingunge Ngombale Mwiru leo ametangaza rasmi kuachana na chama hicho.
Dar es Salaam. Kada mkongwe wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kingunge Ngombale Mwiru leo ametangaza rasmi kuachana na chama hicho na kusema hatajiunga na chama kingine chochote.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kingunge alisema kuwa ukiukwaji na uvunjwaji wa Katiba ya chama, ndiyo sababu kubwa iliyomsukuma kuchukua uamuzi huo.
“Nimeshiriki kwa muda mrefu kuhakikisha kuwa ndani ya CCM kuna demokrasia ambayo kwa sasa inapigwa teke. Katiba kazi yake ni kutuunganisha wote, hivyo hatunabudi kuiheshimu. Lakini viongozi wetu wa sasa wamekuwa wabinafsi na wanafanya mambo wanayoyataka wenyewe tu, na sijui wanayafanya hayo kwa maslahi ya nani?”, alihoji Kingunge.
Kingune amelalamikia namna mchakato wa kumpata mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM ulivyovurugwa mjini Dodoma. Alisema tangu mwaka 1995, utaratibu ulikuwa ni kwa Kamati Kuu ya Chama kuwaita wanachama wote walioomba kugombea urais ili kuwasikiliza na kuwahoji.
Kwa mujibu wa Kingunge, utaratibu huu haukufanyika kwa wagombea wote 38 waliojitokeza kuomba ridhaa ya kugombea urais kwa mwaka huu, hali ambayo ameiita ni ukiukwaji na uvunjwaji wa Katiba kwa makusudi.
“Mwaka 2005, utaratibu huu pia ulitumika. Mgombea mmoja hakuridhika na maamuzi ya Kamati Kuu kukata jina lake. Alikata rufaa kwa Halimashauri Kuu ya chama ambako pia alisikilizwa. Ingawa hakushinda rufaa yake, lakini demokrasia ya kuwasikiliza watu iliheshimiwa tofauti na sasa watu wanafanyiwa vitendo vya udhalilishaji,” alisema Kingunge.
Aidha alisema kuwa uamuzi wake wa kuachana na CCM utawasumbua watu wengi wakiwemo baadhi ya rafiki zake, makada wenzake, ndugu, wazee, na hata vijana, lakini akasisitiza kuwa ni uamuzi ambao ilimlazimu aufanye na kusema kuwa huu ni wakati wa mabadiliko.
No comments :
Post a Comment