ZIKIWA zimebaki siku nane kuanzia sasa kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu, mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amemaliza mikutano yake ya kampeni katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa kuwasisitiza wanachama wake kuhakikisha wanalinda kura zao.
Baada ya kumaliza ziara zake katika kanda hiyo, Lowassa, anayeungwa mkono na vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), leo anatarajia kuanza mikutano mkoani Mbeya.
Mkoa wa Mbeya na Mwanza ni maeneo yenye watu wengi waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura baada ya Dar es Salaam.
Kambi ya Chadema iliyokuwa kanda hiyo kwa takribani siku tano ikiongozwa na Lowassa, ilimaliza mikutano yao kwenye kanda hiyo huku ujumbe mkubwa ukiwa ni kulinda kura.
Jana asubuhi Lowassa akiongozana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru kutoka kwenye Hoteli ya Gold Crest, walikuta umati mkubwa ukiwa nje ya hoteli hiyo ukiwasubiri.
Kutokana na hali hiyo, Mbowe alilazimika kuwasalimia watu hao na kuwahoji kama watapiga na kulinda kura zao.
Kutokana na swali hilo, umma huo ulijibu kuwa utazilinda, huku baadhi yao wakisema kama wapo wa kuondoka kituoni, ni hao ambao hawataki walinde kura zao.
Baada ya hali hiyo, Mbowe, alisema ni vyema vyombo vya dola vikatambua kuwa watu hawako tayari kupoteza haki yao, hivyo ni vyema wakaachwa walinde kura zao.
Kutokana na kile kinachoonekana ni wasiwasi wa kuibiwa kura unaowafanya watake wananchi kulinda kura, juzi Lowassa, aliionya Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), akisema isipokuwa makini itavuruga uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Kauli ya Lowassa ilikuja siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa takwimu za watu waliojiandikisha kupiga kura zilitofautiana na zile za NEC.
Alisema watu waliojiandikisha katika daftari la wapiga kura kwa Tanzania Bara pekee ni milioni 28, huku Zanzibar wakiwa 500,000, huku zile za NEC zikionyesha waliojiandikisha Bara ni milioni 22.7 na Zanzibar ni 503,193.
Siku hiyohiyo alipotoa takwimu hizo, Ikulu ilitoa ufafanuzi ikisema takwimu sahihi ni zile zilizotolewa na NEC.
/MTANZANIA.
No comments :
Post a Comment