dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, October 15, 2015

Lowassa: Chadema imeiva kuingia Ikulu!

Mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Sokoni, wilayani Biharamulo, mkoani Kagera jana. Picha na Emmanuel Herman
By Ibrahim Bakari, Mwananchi
Biharamulo. Mgombea urais wa Chadema na kwa mwavuli wa Ukawa, Edward Lowassa amesema mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amekijengea mizizi imara chama chake na sasa kimeiva kuingia Ikulu Oktoba 25.
Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Soko Jipya, Biharamulo mkoani Kagera, Lowassa alisema chama hicho kwa sasa kiko imara na kinaweza kukamata dola.
Kabla ya kuanza mkutano huo, Lowassa aliwataka wananchi waliofika kumsikiliza kukaa kimya dakika moja kumkumbuka Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye ndiye mwasisi wa Taifa, jana ikiwa ni maadhimisho ya miaka 16 tangu kifo chake.
Akimzungumzia Mbowe, mgombea huyo anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katika ya Wananchi (Ukawa), alisema misingi aliyoijenga Mbowe imekiwekea heshima chama hicho na sasa kinakwenda kuchukua dola.
Katika mkutano huo Lowassa alipiga chagizo la kampeni zake la “mabadilikoo.... ambalo wafuasi wake huitikia Lowassaaaa” lakini upande mmoja kwenye mkutano huo ulikaa kimya na kusema: “Hawa huku itakuwa CCM, mbona hamjibu? Lakini ninawataka wote pamoja na wanaCCM mnipe kura kwani hata mimi nilikuwa mwanaCCM, nipeni kura za kutosha.”
Alirejea kauli yake kuwa ataibadilisha Tanzania kuwa ya viwanda, kutatua tatizo la ajira kwa vijana pamoja na kuongeza mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana watakaojiunga na JKT na kuondoa umaskini.
Akihutubia katika mkutano huo, Mbowe alisema wameandaa ilani ambayo itatekelezwa mara moja watakapoingia madarakani.
Alitumia nafasi hiyo kusifu ujio wa waliokuwa viongozi wa CCM, Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye aliyekuwa mshauri wa rais mambo ya siasa, Kingunge Ngombale – Mwiru kuwa umeleta baraka ndani ya Chadema na sasa ndicho kichocheo cha mabadiliko.
“Ujio wao ni baraka kwa Chadema, tutatumia uzoefu wao kujenga Serikali ya kizalendo na uzoefu wao ni muhimu katika ujenzi wa Tanzania mpya,” alisema Mbowe.
Akizungumzia mchakato wa Katiba, Mbowe alirejea kusema kuwa wataisimamia rasimu ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba iliyokuwa ikiwalenga zaidi wananchi na kwamba kikubwa kitakachoangaliwa ni maadili ya uongozi, rasilimali, uwajibikaji na ugatuzi wa madaraka.
Katika mkutano huo, Kingunge alisema kwa sasa ni wakati muhimu kwa Watanzania kubadilika kwani nusu karne imetosha na sasa ni wakati wa upinzani.
Waziri wa zamani wa mambo ya ndani, Lawrence Masha alisema upinzani umejiandaa na hautaki kushinda kwa kubahatisha kuiondoa CCM madarakani.
Mgombea ubunge wa Jimbo hilo, Dk Anthony Mbassa alisema wakazi wa Biharamulo wanakabiliwa na ukosefu wa malisho, matatizo ya maji na huduma za afya.
Wakazi wazungumza
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa mkutano huo, baadhi ya wakazi wa Biharamulo waliainisha matatizo kadhaa yanayowakabili kuwa ni barabara na huduma za afya.
Muuza matunda katika eneo hilo la Soko Jipya, Audax Ngemela alisema tatizo kubwa kwao ni barabara kutoka Bwanga – Biharamulo ambayo alisema inatakiwa kuwa katika kiwango cha lami huku, Ponsian Edward wa Biharamulo akisema kero yao ni mfululizo wa michango shuleni.
“Kwa kweli tunakwazwa na hii michango... ni mingi na inakatisha tamaa. Serikali imesema michango ni Sh20,000 shule za kata lakini hapa inafikia hata Sh180,000, sasa hapa wanatengeneza chuki na Serikali, tunaipenda lakini watendaji wanawaharibia,” alisema.
Mwingine, Jaqueline Mshasha alisema huduma za afya hazitolewi kama Serikali ilivyoagiza kwa mama na mtoto, wazee na wenye magonjwa yasiyotakiwa kulipia zinatozwa fedha.

No comments :

Post a Comment