Dar es Salaam. Mgombea wa urais kupitia CCM, Dk John Magufuli ameahidi kulibadili jiji la Dar es Salaam kwa kujenga barabara za lami na kutatua tatizo sugu la foleni kupitia ujenzi wa madaraja na barabara za juu maarufu kama ‘flyovers’.
Dk Magufuli amefanya kampeni katika jimbo la Segerea leo, amewaomba wakazi wa Dar es Salaam wampatie kura Oktoba 25 ili aweze kutekeleza miradi hiyo mikubwa itakayoenda sanjari na ujenzi wa barabara zitakazopunguza foleni.
Akiwahutubia wakazi wa Vingunguti wilayani Ilala, Dk Magufuli amesema kuna baadhi ya watu watahoji alikuwa wapi kipindi cha nyuma kutekeleza miradi hiyo lakini ukweli ni kwamba Serikali zilizopita zilikuwa na kazi ya kuunganisha mikoa yote na Dar es Salaam.
“Vingunguti barabara zenu zitawekwa lami na nyingine nyingi tu ambazo zitasaidia kupunguza foleni ndiyo maana juzi mmeona tumesaini mkataba wa Sh100 bilioni kwa ajili ya kujenga ‘flyovers’ pale Tazara na muda mfupi mtamwona mkandarasi kutoka Japan akianza kujenga.
“Kwa hiyo watu wa Vingunguti mtaamua mnataka kupita juu au chini na nina uhakika watani zangu Wazaramo wataenda kupiga ngoma juu ya ‘flyover’,” amesema Magufuli.
Dk Magufuli amesema atajenga makutano ya kisasa eneo la Ubungo kwa kujenga barabara za ghorofa mbili na tayari fedha za mradi huo zipo zaidi ya Sh70 bilioni chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia (WB).
Dk Magufuli hakuacha vijembe kwa wapinzani wake akiwananga kuwa mabadiliko hayaji kwa kuzunguka mikoni bali kutafuta njia madhubuti za kuwaletea wananchi maendeleo.
Mkazi wa Vingunguti, Salma Hassan amesema kero kubwa katika eneo lao ni ukosefu wa maji safi na salama, elimu duni kwa watoto wao na barabara za mitaa.
No comments :
Post a Comment