dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, October 16, 2015

Mita 200 uchaguzi kaa la moto!

Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu.
Mvutano kati ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na mamlaka mbalimbali za serikali kuhusiana na mahala wanakostahili kukaa wafuasi wao baada ya kupiga kura Oktoba 25 umezidi kushika kasi huku baadhi ya wasomi wakitaka kufanyike kikao maalum baina ya pande zote ili kupata muafaka utakaodumisha amani na utulivu uliopo nchini.
 
Hivi karibuni, viongozi wa Ukawa unaoundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD, wamekuwa wakiwahimiza wafuasi wa vyama vyao kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na pia kuhakikisha kuwa hawarejei nyumbani kwao baada ya kupiga kura bali kukaa walau umbali wa mita 200 kutoka kwenye vituo vya kupiga kura ili kuhakikisha kuwa hakuna njama zozote za wizi wa kura za wagombea wao.
 
Viongozi hao wa Ukawa, akiwamo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara), John Mnyika, wamekuwa wakisisitiza kuwa maelekezo yao yanazingatia sheria ya uchaguzi inayowaruhusu kukaa eneo la umbali wa mita 200 kutoka vituo vya kupigia kura, lengo likiwa ni kuepusha wizi wa kura kwani wakizubaa, wanaamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitafanya hila ya kuiba kura zao ili kutimiza kile kilichowahi kukaririwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, kuwa watashinda hata kwa 'bao la mkono'.Hata hivyo, kwa nyakati tofauti, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva na Mkurugenzi wa NEC, Kailima Ramadhani, wamekuwa wakiwapinga viongozi wa Ukawa na kuwataka wananachi waondoke na kurudi nyumbani kwao baada ya kupiga kura kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuepusha vurugu na badala yake kuiacha kazi ya kulinda kura zao mikononi mwa vyombo vya usalama.
 
Sakata hilo lilichukua sura mpya juzi wakati Rais Jakaya Kikwete aliposisitiza kuwa ni marufuku kwa wananchi kukaa jiranbi na vituo vya kupigia kura kwa 'kisingizio' cha kulinda kura na badala yake, akawataka wasikubali kudanganywa na viongozi wa vyama vya siasa bali watii maelekezo kwa kurejea makwao mara tu baada ya kupiga kura zao.
 
Rais Kikwete alisema jukumu la kulinda kura linapaswa kufanywa na mawakala wa kila chama kinachoshiriki uchaguzi na hivyo, kuruhusu wananchi kukaa jirani na vituo vya kupigia kura hakuna sababu ya msingi na kwamba, kufanya hivyo kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani na hilo halitavumiliwa kwani wakaidi watashughulikiwa ipasavyo.
 
Licha ya maelekezo hayo ya Rais Kikwete wakati akizungumza mjini Dodoma juzi, sakata hilo liliendelea tena jana baada ya mgombea urais wa Ukawa, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuitaka NEC izingatie sheria kwani kinyume chake ni wanaweza kuvuruga uchaguzi na kusababisha uvunjifu wa amani usiokuwa na sababu.
 
Akizungumzia suala hilo wakati akihutubia wananchi kwenye Uwanja wa Sabasaba wilayani Magu mkoani Mwanza jana, Lowassa alisema NEC haipaswi kuingiza mambo yasiyokuwamo kwenye sheria.
 
"Naomba wawe makini, wasituharibie uchaguzi wetu na nchi yetu, kwani amani ni muhimu sana katika nchi yetu," alisema.
 
Kwa mara nyingine, Mbowe alisisitiza vilevile kuwa wananchi waende kupiga kura na wahesababu mita 200 kutoka vituoni na kupiga kambi hapo kulinda kura zao.
 
"Nasema hivi, kulala hatulali, nyumbani hatuendi, tutahesabu mita 200 kwa mujibu wa sheria na tutakaa na kulinda kura zetu," alisema.
 
Alisema serikali ya CCM imeanza kuingia hofu ya kuondolewa madarakani na ndiyo maana imetoa amri ya kuwataka waende nyumbani badala ya kuzingatia matakwa ya sheria ya uchaguzi.
 
*Imeandikwa na Mary Geofrey, Richard Makore na Salome Kitomari 
 
CHANZO: NIPASHE


No comments :

Post a Comment